November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

UWT Tabora wanogesha mafanikio ya miaka mitatu ya Rais Samia

Na Allan Vicent, TimesmajiraOnline,Tabora

UMOJA wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoani Tabora wameeleza kufurahishwa na kazi nzuri ilivyofanywa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika miaka mitatu ya utawala wake na kuahidi kuzunguka katika Wilaya zote ili kuyasema mazuri yote aliyoyafanya kwa wananchi.

Wameeleza hayo juzi walipokuwa wakiongea na mwandishi wa gazeti hili aliyetaka kujua mikakati ya Umoja huo kuelekea kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu wa mwakani wa Rais, Wabunge na Madiwani

Katibu wa UWT Mkoa, Rhoda Madaha, amesema kuwa miaka 3 ya Rais Samia imeletea neema kubwa sana kwa wananchi katika sekta zote ikiwemo elimu, afya, maji, nishati na miundombinu ya barabara.

Amebainisha kuwa kasi, weledi na ubunifu wake vimewezesha miradi mikubwa ya kimkakati kutekelezwa kwa ufanisi mkubwa na kutoa fursa za ajira kwa wananchi wengi, alitaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni reli ya kisasa (SGR) na bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda kuja Tanzania.

Miradi mingine ni Bwawa la Kuzalisha Umeme la Mwalimu Nyerere (Stiglers Gorge) ambalo tayari limeanza kuongeza nguvu ya umeme nchini baada ya kinu cha kwanza kuwashwa, matokeo chanya yameanza kuonekana na mgao sasa umeisha.

Madaha ameeleza kuwa mama ametekeleza miradi mingi ya maji katika Mikoa yote hapa nchini na mingine inaendelea kutekelezwa ikiwemo Mradi wa Ziwa Viktoria na Mradi wa Miji 28, miradi hii imewafuta machozi akinamama.

Amesisitiza kuwa akinamama walikuwa wanahangaika sana kufuata maji umbali mrefu lakini mama amemaliza kero hiyo, sasa maji yameendelea kusogezwa karibu zaidi na wananchi ili kumtua mama ndoo kichwani.

‘Wamepita viongozi wengi, lakini kwa uthubutu huu wa mama yetu, tunamuunga mkono kwa asilimia 100, tutazunguka Mkoa mzima kuyasema mazuri yote aliyoyafanya na tutahamasisha wanawake wote wamuunge mkono’, amebainisha.

Naye Mwenyekiti wa UWT Mkoa, Mwanne Mchemba amesema kuwa Rais Samia amefanya mambo makubwa sana, hawawezi kukaa kimya, hivyo akaahidi kuwa mwakani watatembea nyumba kwa nyumba, mtaa kwa mtaa, kitongoji kwa kitongoji, kijiji kwa kijiji, kata kwa kata na tarafa kwa tarafa ili kumwombea kura.

Ameeleza kuwa chini ya Uongozi wa Rais Samia nchi ipo katika mikono salama, akinamama wanajivunia kuwa na Kiongozi mwanamke, mchapakazi mahiri na wa viwango, hivyo wakaahidi kumuunga mkono na kumpa kura za kishindo.

Aidha Mchemba amewataka wanawake wote wa Mkoa huo kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na ule wa mwakani ili kuwapigia kura wagombea wote wa CCM huku akiwaomba wale wote wenye sifa na uwezo wajitokeze kugombea pia.