April 30, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Masauni awaonya wanaotumia mitandao kutukana viongozi

Na Joyce Kasiki, TimesmajiraonlineDodoma

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhandisi, Hamad Masauni amewaonya watu wenye tabia ya kutumia mitabdao kutukana viongozi wakuu hususan Rais Samia Suluhu Hassan .

Mhandisi Masauni ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi kuelekea miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Amesema wale wote wenye tabia hiyo Serikali haitawafumbia macho na kila atakayebainika sheria itachukuliwa dhidi yake.

Katika hatua nyingine amesema Sekretarieti ya Kuzuia na Kupambana na Usafirishaji Haramu wa Binadamu imefanikiwa kuokoa na kusaidia waathirika 1,338 waliokuwa wakitumikishwa ndani na nje ya nchi, ambapo kati ya hao 1,211 waliokolewa hapa nchini na waathirika 127 walitoka nje ya nchi za Thailand, India, Oman, Yemeni, Kenya, Botswana, Malaysia na Iraq.

“Waathirika wote walipewa huduma muhimu zikiwamo malazi, matibabu, chakula, msaada wa kisheria , urekebishaji na kuunganishwa na familia zao,” amesema.

Pia Waziri Mhandisi Masauni ameeleza kuwa Sekretarieti hiyo imefanikiwa kufanya oparesheni za kusambaratisha mitandao inayojihusisha na usafirishaji haramu wa binadamu, ambapo kupitia oparesheni hizo wahalifu 218 walikamatwa na kesi 131 zilifunguliwa katika mahakama mbalimbali nchini.

Amesema kati ya kesi hizo 107 zimeshatolewa uamuzi na wahalifu 81 walipatikana na hatia ambapo walipewa adhabu ikiwamo kifungo gerezani.

” Wizara kupitia Sekretarieti imefanikiwa kuanzisha Ofisi ya Kuzuia na Kupambana na Usafirishaji Haramu wa Binadamu -Zanzibar ili kuimarisha mapambano dhidi ya biashara haramu ya usafirishaji haramu wa binadamu,” amesema Waziri Masauni.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, Wizara kupitia Sekretarieti imefanikiwa kuanzisha Mfuko wa Kupambana na Usafirishaji Haramu wa Binadamu , ili kuimarisha huduma zitolewazo kwa waathirika hao.

“Mfuko huo ni mahsusi kwa ajili ya kusaidia waathirika tu na unapata fedha kutoka serikalini na kwa wadau mbalimbali wakiwamo watu binafsi, ambapo umeenzishwa kwa mujibu wa kifungu cha 25 cha Sheria ya Kuzuia na Usafirishaji Haramu wa Binadamu Namba 6/2008.”Amesistiza Mhandisi Masauni