November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Samia apeleka bilioni 4.6/-Kibondo za huduma za afya

Na Allan Vicent, TimesmajiraOnline,Kigoma

SERIKALI ya awamu ya 6 inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imepeleka sh. bil 4.6 Wilayani Kibondo Mkoani Kigoma kujengwa zahanati, vituo vya afya, wodi za wazazi na jengo la dharura ili kuboreshwa huduma za afya.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Diocles Rutema, alipokuwa akizungumza na mwandishi wa gazeti hili aliyetembelea wilaya hiyo hivi karibuni ili kujionea mafanikio ya miaka mitatu ya Rais Samia.

Amemshukuru Rais Samia kwa kuwapatia kiasi hicho cha fedha katika kipindi cha miaka miaka tangu aingie madarakani, kwani kimewezesha kujengwa vituo mbalimbali vya kutolea huduma za afya kwa jamii.

Amebainisha kuwa kujengwa zahanati za kutosha, vituo vya afya, wodi za wazazi, jengo la dharura katika hospitali ya wilaya, nyumba za watumishi na kununuliwa vifaa tiba na madawa ni mambo ambayo yamewafurahisha sana wananchi.

Rutema amefafanua baadhi ya miradi iliyotekelezwa kwa mafanikio makubwa kuwa ni ujenzi wa Kituo cha Afya Bunyambo (sh mil 500), Rugongwe (sh mil 900) na wodi ya wazazi katika zahanati ya Kibuye (sh mil 75).

Mingine ni ujenzi wa nyumba ya watumishi katika Kituo cha Afya Kagezi (sh mil 90), Jengo la Dharura (EMD) katika hospitali ya Wilaya (sh mil 300) na ukarabati wa Chuo cha Maafisa Tabibu, ununuzi wa samani na vitabu (sh mil 463.6).

Mkurugenzi ametaja miradi mingine kuwa ni ujenzi wa Kituo cha Afya Kibondo Mjini (sh mil 500), Kituo cha Afya Kizazi (sh mil 500), ukamilishaji ujenzi wa wodi ya akinamama katika zahanati ya Kumhasha na kuweka samani (sh mil 50).

Miradi mingine ni ukamilishaji zahanati ya Kumwambu na kununua samani zake (sh mil 50) na ukamilishaji zahanati ya Mabamba iliyojengwa kwa nguvu za wananchi (sh mil 50).

Ametaja mradi mwingine kuwa ni ujenzi wa vyoo bora katika vituo 10 vya kutolea huduma za afya vya Mikonko, Kibuye, Mukabuye, Minyinya, Bunyambo, Biturana, Magarama, Samvura, Kibondo Mjini na Kumhama (sh mil 307).

Aidha, vifaa tiba vyenye thamani ya sh. mil 200 vilinunuliwa kwa ajili ya Vituo vya Afya Bunyambo, Kibondo na Nyaruyoba na zahanati mbili za Nyarulanga na Mabamba na zahanati nne za Malolegwa, Lukaya, Kukinama na Kasana zilikamilishwa ujenzi wake kwa gharama ya sh. mil 200.

Rutema alimshukuru Rais pia kwa kuwapatia sh mil 500 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la mionzi na ukarabati wa Hospitali ya Wilaya na kubainisha kuwa miradi hiyo yote imesaidia kuboreshwa huduma za afya kwa kiasi kikubwa ikiwemo kumaliza msongamano wa wagonjwa katika vituo vya kutolea huduma.