December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Msajili wa Baraza la Veterinari, Dkt. Bedan Masuruli

Baraza la Vetenari lawaonya Madaktari wa mifugo nchini

Na Oscar Mzuka, Dodoma

BARAZA la Veterinari lililopo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, imetishia kuwafutia usajili madaktari kwenye Daftari ya Mifugo walioko Serikali na madaktari binafsi wanaoshindwa kulipa ada kila mwaka.

Hayo yalisemwa jijini Dodoma jana na Msajili wa Baraza la Veterinari, Dkt. Bedan Masuruli, alipokuwa akizungumzia hatua za kuwafutia usajili madaktari watakaobainika kushindwa kulipa ada kwa makusudi.

Dkt Masuruli amesema hakuna sababu maalum zinazowafanya madaktari hao kushindwa kulipa ada.

Amesema kinachofanyika ni uzembe na kutotii Sheria za Veterinari, hivyo wanatakiwa kuzifuata wakati wa kufanyakazi za mifugo zinazotambuliwa na Serikali.

“Ni aibu  madaktari hao kushindwa kulipa ada ya sh. 3,000 kwa mwaka. Huu ni uzembe na dharau, Serikali haioni sababu ya kutowafutia usajili na hawataruhusiwa kufanya kazi hizo, wanatakiwa kuzingatia sheria,” amesema, Dkt. Masuruli.

Aidha amesema  madaktari kama hao watawekwa hadharani kwa kuwataja majina yao kupitia vyombo vya habari na vilevile kwenye mtandao ya kijamii.

Amefafanua kwamba hatua hiyo itawadhibiti kufanya kazi za mifugo kinyemela sehemu mbambali nchini.