Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Korogwe
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imetoa maagizo kwa Wakurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe na Halmashauri ya Mji Korogwe kutokubali kufanya kazi na watumishi wazembe ambao watachelewesha miradi ya maendeleo kukamilika kwa wakati.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya LAAC Esther Bulaya katika majumuisho mara baada ya kutembelea na kukagua majengo yaliyojengwa na yanayoendelea kujengwa kwenye Hospitali ya Wilaya ya Korogwe, Makuyuni pamoja na kukagua soko la kisasa la Kilole lililipo Halmashauri ya Mji Korogwe, na kutoridhishwa na baadhi ya mambo kwenye miradi hiyo.
Ambapo Bulaya ameeleza kuwa miradi kuchelewa kukamilika kunakwamisha wananchi kupata huduma za kijamii.
” Wakurugenzi ninyi ndiyo mna jukumu la kusimamia miradi ya maendeleo na usimamizi wa waliochini yenu,hivyo msikubali watumishi wazembe wakawa kikwazo kwenye miradi,” amesema Bulaya.
Pamoja na mambo mengine, Bulaya ametaka soko la kisasa Kilole lianze kufanya kazi baada ya kukaa miaka saba tangu ujenzi wake kukamilika lakini alifanyi kazi na kusababisha mamilioni ya fedha ikiwemo kodi za Serikali kupotea.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, Goodluck Mwangomango na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Korogwe,Mwashabani Mrope, wamesema watafanyia kazi mapungufu yote yaliyobainika kwenye miradi hiyo kufuatia ziara ya Kamati ya LAAC.
Akisoma taarifa ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Korogwe Makuyuni, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Dkt. Miriam Cheche amesema jumla ya majengo yaliyotarajiwa kujengwa katika eneo hilo ni 22 ambayo yatagharimu kiasi cha bilioni 7.5 kwa makisio ya mwaka wa fedha 2018/19.
“Awamu ya kwanza ya ujenzi ilianza na majengo saba ambayo ni jengo la OPD (Wagonjwa wa Nje),maabara,mionzi, wazazi,Bohari ya Dawa,kufulia na utawala, yalikadiriwa kumamilika kwa gharama ya bilioni 1.8. Awamu ya pili ya ujenzi iliendelea wa majengo matatu ambayo ni jengo la watoto,wodi ya wanaume na wodi ya wanawake ambapo majengo haya yalikadiriwa kumamilika kwa gharama ya milioni 500,”ameeleza Dkt.Cheche na kuongeza:
“Awamu ya tatu ya ujenzi wa majengo manne (4) ambayo ni jengo la kuhifadhia maiti, upasuaji, wodi ya wanawake na
wanaume yalikadiriwa kujengwa kwa gharama ya milioni 800 huku Mkandarasi Shelutete Construction Company Ltd amejenga kwa gharama ya milioni 795, yapo katika hatua za umaliziaji wa kazi ndogo ndogo na bado yapo katika muda wa uangalizi (Retention),”.
Dkt. Cheche amesema majengo yote manne yamezinduliwa na Mkuu wa Wilaya ya Korogwe William Mwakilema mnamo Machi 6, 2024, na yanatumika kutoa huduma husika.
Akisoma taarifa ya ujenzi wa soko la kisasa la Kilole, Mchumi wa Halmashauri ya Mji Korogwe Elinlaa Kivaya amesema halmashauri hiyo ilianza utekelezaji wa ujenzi wa soko Desemba, 2016 na kukamilika Aprili, 2018 kwa Mkataba Na. LGA/126/ULGSP/BLDG/2016/2017/01/2017/18 chini ya mkandarasi MS RAVJI Construction Ltd.
Ambapo ujenzi wa soko hilo unathamani ya bilioni 1.2 ikiwa ni fedha toka Benki ya Dunia (World Bank) chini ya mradi mkubwa wa Uboreshaji wa Majiji na Miji.
“Mradi huu ulihusisha ujenzi wa jengo la soko likiwa na maeneo ya vizimba 56, mabucha 8, vibanda vinne (4) vya mama lishe,vibanda vinne (4) vya wauza mitumba, vyoo,eneo la maegesho, uzio na taa,”ameeleza Kivaya.
Pia ameeleza kuwa hoja ya Mkaguzi wa Nje (CAG) ni moja tu ya mwaka 2018/19 ambayo haijajibiwa kikamilifu mpaka sasa ambayo ni kutokutumika kwa soko la Kilole.
“Sababu ni mwitikio mdogo wa wafanyabiashara kufanyia biashara katika soko hilo kutokana na kuwa pembezoni mwa Mji na kuwepo kwa soko la zamani la Manundu ambalo lipo katikati ya Mji, hivyo watu kuona ni rahisi zaidi kupata mahitaji yao huko,”.
More Stories
AZAKI yawasilisha mapendekezo yao kwa Serikali katika kuboresha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050
CP.Wakilyamba :Uvamizi maeneo ya hifadhi ya taifa katavi haukubaliki
Watu wawili wanaodhaniwa majambazi wapigwa risasi na Polisi