Na Irene Clemence, TimesMajira Online, DSM
TAASISI ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu(MOI), inatoa huduma ya mazoezi tiba bure katika Maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa yanayofanyika katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere Sabasaba.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho hayo Ofisa Habari wa MoI,Patrick Mvungi amesema kuwa mbali na kutoa elimu na ushauri kwa wananchi wanaotembelea banda la taasisi hiyo mwaka huu wanatoa huduma hiyo ya matibabu.
Amesema kwenye maonesho hayo yupo mtaalamu ambaye anatoa ushari na kuelekeza pamoja na kuwafanyia mazoezi kwa kuwaelekeza ili wakiwa majumbani waendelee.
“Tunatoa huduma za mazoezi tiba kwa wagonjwa wenye maumivu ya mgongo na sehemu zingine amabzo zinahitaji huduma ya mazoezi tiba,”amesema Mvungi.
Amesema zaidi ya wananchi 300 wametembelea banda hilo wakihitaji i huduma za kimatibabu huku wenye uhitaji zaidi kuelekezwa kufika MoI kwa ajili ya matibabu zaidi.
Amesema mwitikio wa wananchi kutembelea banda lao ni mkubwa ukilinganisha na mwaka jana hasa wenye maumivu ya mgongo kwa kupata maelekezo kutoka kwa watalaamu kama namna ya kukaa.
“Mtaalamu wa mazoezi tiba amekuwa akifanya kazi kubwa kwa sababu wagonjwa ni wengi wanakuja na tunaamini elimu wanayoipata inawasaidia,”amesema.
Amefafanua kuwa kundi la wazee ndilo limefika kwa wingi kwenye taasisi hiyo kupata elimu na ushauri pamoja na huduma ya mazoezi tiba.
“Kundi kubwa ni la kuanzia miaka 50 kwenda juu ndiyo kundi kubwa wamekuwa wakilalamika wanamaumivu ya mgongo na hawajui tiba yake ni nini,”amesema
Amesema wapo wanaofika kwenye maonesho hayo wakiwa na vipimo vyao kutoka hospitali ambapo husomwa na wataalamu na kuwashauri namna ya kufanya kulingana na tatizo husika.
Ameongeza kuwa pia taasisi hiyo inawataalamu wa viungo bandia kwa kuwatengenezea waliokuwa na shida ya kupata viungo hivyo na kutembea kama kawaida.
More Stories
Watakiwa kushirikiana kutikomeza matatizo ya lishe
CCBRT yazidi kuunga mkono juhudi za Rais Samia
Madaktari bingwa wa Samia watua Rukwa