Na Esther Macha, TimesmajiraOnline,Mbeya
MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jijini Mbeya(MBEYA-UWSA), imeeleza kuwa kukatika kwa umeme pamoja na uwepo wa miinuko kwa baadhi ya maeneo ni chanzo cha changamoto inayoikabili sekta ya maji katika kutoa huduma kwa wananchi jijini humo.
Takribani asimilia 70 ya maji kwenye chanzo cha maji cha Nzovwe,Iyela ni ya chemchem lakini gharama yake inakuja kwenye kusukuma na pampu ili waweze kuhudumia wananchi.
Mtambo mwingine upo eneo la Swaya na miradi yote ni mikubwa ambayo inahitaji nishati ya umeme katika usukumaji wa maji na ikitokea changamoto ya kukatika umeme huduma hiyo huwa inaathiriwa kwa wastani wa asilimia 40.
Kauli hiyo imetolewa kwa waandishi wa habari na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa wa mamlaka hiyo ambaye pia ni Mkurugenzi wa uzalishaji maji na usambazaji maji safi mkoani Mbeya Mhandisi,Barnabas Konga wakati akitoa taarifa ya maadhimisho ya wiki ya maji ambayo yameanza Machi 16 mpaka Machi 22,mwaka huu.
Ambapo amesema mamlaka hiyo imekuwa ikiratibu maadhimisho hayo kila mwaka katika kutekeleza azimio la Umoja wa Mataifa namba 47 na kwa mwaka huu itaadhimisha kwa kufanya shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa jijini Mbeya na Mbeya Vijijini.
Mhandisi Konga amesema kuwa katika kufanya utatuzi wa changamoto hiyo ya umeme wamekuwa wakifanya mawasiliano na watu wa Tanesco na kuongeza kuwa kwa baadhi ya maeneo ya Nzovwe wamekuwa wakifuatilia kwa ukaribu na hawatarajii kuungua kwa mitambo na kukatika kwa umeme.
“Sehemu zingine kama Nsalaga na Uyole wamekuwa wakiathiriwa sana hivyo tunashukuru mipango ya serikali ambayo inafanyika kupitia bwawa la Mwalimu Nyerere ambalo limeanza kuingiza Megawaiti kwenye gredi ya Taifa na tushaona nafuu,”amesema.
Pia ameeleza kuwa umeme ukikatika na kurudi wakati mwingine inaleta athari kwenye mitambo baadhi ya vifaa kuungua na kuanza kutafuta na kuleta usumbufu kwa wananchi ambapo wanatakiwa wapate huduma masaa 24.
Konga ameitaja baadhi ya miradi inayotekelezwa katika kipindi cha miaka mitatu ni upatikanaji wa maji kwa Jiji la Mbeya na Mji wa Mbalizi ni lita milioni 38.5 kwa siku mahitaji yakiwa lita milioni 90 kwa siku.
Baada ya maboresho mamlaka inatekeleza miradi yenye thamani ya bilioni10 inayotoa lita milioni 66.5 kwa siku.
Aidha miradi iliyotekelezwa ni pamoja na mradi wa Mwashali uliogharimu milioni 400 ukihudumia watu 6,000,mradi wa Nzovwe lsyesye umegharimu milioni 930 ukihudumia wakazi 30,000.
Mradi mwingine ni wa UVIKO-19 wenye thamani ya milioni 758 ukihudumia watu 55,000 ambapo mradi wa Shongo Mbalizi uliogharimu bilioni 3.345 ukihudumia watu 80,000.
Huku mradi mwingine ni pamoja na mradi wa Ilunga wenye thamani ya bilioni 4.8 utakaohudumia watu 110,000 ambapo miradi yote kwa pamoja inagharimu bilioni 10 huku mradi wa Kiwira utakaoghaimu bilioni 250 utamaliza kabisa changamoto ya maji mkoani Mbeya.
Mhandisi Leonidas Deogratius Meneja mradi wa Mwasenkwa amesema mradi huo wenye thamani ya bilioni 5.2 utanufaisha wananchi 42,000,utazalisha lita milioni 2.6.
Akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea miradi ya Mwasenkwa na Ilungu , Ofisa Uhusiano wa Mamlaka ya MajiSafi na Usafi wa Mazingira Jijini Mbeya,Neema Stanton amesema inatekeleza miradi mbalimbali ya maji ikiwemo ya muda mfupi na muda mrefu.
Aminaeli Julius ni Ofisa Habari wa mamlaka hiyo amewataka wananchi kutoa taarifa pindi wanapokutana na changamoto ya maji ili mamlaka iweze kutatua kwa wakati.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa