Na Raphael Okello, Timesmajira Online Musoma
JESHI la Polisi na Waandishi wa Habari mkoani Mara wamekubaliana kuwa waandishi hao kuhakikisha wanakuwa na vitambulisho pamoja na mavazi maalum pindi wanapokusanya au kutoa taarifa katika makundi michanganyiko.
Hiyo ikiwa ni hatua ya kuimarisha ulinzi na usalama kwa waandishi wakati wakitekeleza majukumu yao katika maeneo hatarishi.
Makubaliano hayo ambayo hayataathiri sheria, kanuni na taratibu ya majukumu ya pande zote ni pamoja na jeshi kutoa mafunzo maalum kwa waandishi wa habari kuhusu mambo muhimu ya kufanya au kuzingatia wanapokuwa eneo hatarishi.
Akizungumza katika mdahalo huo kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara Salim Morcase, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi mkoani humo Thomas Makane amesema midahalo hiyo imeleta chachu mpya katika kuimarisha ulinzi na usalama kwa waandishi na kwamba makubaliano hayo yatazingatiwa na pande zote.
Mbali na hayo pia wamekubaliana kuwa waandishi wote wa habari mkoani humo wajisajili na kutambulika katika Klabu ya Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Mara(MRPC) ili iwe rahisi kupata huduma na ushauri wa kiulinzi kupitia umoja wao.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Musoma Ally Mwendo, ameeleza kuwa makubaliano hayo yatachochea uimarishaji wa demokrasia na uhuru wa upatikanaji wa taarifa.
Mwendo amesisitiza pande zote kuzingatia weledi wao katika kutekeleza majukumu yao kwani waandishi wa habari na jeshi la polisi ni sekta muhimu katika kudumisha amani ya nchi.
Naye Askofu Daniel Ouma, aliwashauri waandishi habari kutumia kalamu zao kutafsiri vyema sheria, sera ya nchi na matamko mbalimbali na kwamba wanapozipotosha jamii pia inaweza kupotoka.
Kwa upande wao, baadhi ya waandishi wa habari walipongeza Muungano wa klabu ya waandishi wa habari Tanzania(UTPC), Shirika la International Media Services (IMS) na MRPC kuratibu na kuiwezesha midahalo hiyo ya ulinzi na
Usalama ambayo hadi sasa imeleta uhusiano kati ya polisi na waandishi wa habari mkoani Mara.
Makubaliano hayo pamoja na mambo mengine yalifikiwa kwa pamoja katika mdahalo wa nne wa ulinzi na usalama uliowashirikisha jeshi la polisi, waandishi wa habari, wanasheria, viongozi wa dini, viongozi kutoka serikalini, viongozi wa kisiasa na asasi za kiraia, mdahalo uliofanyika mwishoni mwa wiki mjini Musoma mkoani Mara.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi