December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mama atuhumiwa kuua watoto wake wawili kwa sumu

Na Esther Macha, Timesmajira, Online, Mbeyca

Daines Mwashambo (30)mkazi wa Kijiji cha Mashese Wilaya ya Mbeya Vijijini mkoani Mbeya anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kuwanywesha sumu ya kuulia magugu shambani aina ya “Pare Force ” watoto wake wawili.

Baada ya kutenda kitendo hicho naye alikunywa sumu hiyo kutokana na msongo wa mawazo uliochangiwa na tuhuma dhidi yake juu ya wizi zilizotolewa na Serikali ya Kijiji hicho cha Mashese ambapo tukio hilo lilitokea Machi 5, mwaka huu akiwa nyumbani kwake.

Akizungumza na waandishi wa habari Machi,9 mwaka huu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamshina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi ,Benjamin Kuzaga amewataja watoto hao kuwa ni Semeni Adamson (4) na mdogo wake wa kike Beonis Adamson (2) wote wakazi wa Mashese Wilaya ya Mbeya Vijijini ambao walipoteza maisha wakati wakipatiwa matibabu katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya.

Kamanda Kuzaga amesema kwa sasa mtuhumiwa huyo kwa sasa anaendelea na matibabu katika Hospitali Rufaa ya Mkoa wa Mbeya akiwa chini ya ulinzi wa polisi.

“Tunaatoa wito kwa jamii pindi unapopatwa na tatizo suluhisho lake sio kujichukulia sheria mkononi bali ni kutafuta ushauri au kufuata sheria inavyoelekeza ili kuepuka madhara kwako na jamii inayokuzunguka,”amesisitiza Kuzaga.