November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Washindi 12 wa NMB MastaBata na wenza wao wapaa Afrika Kusini

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

WASHINDI 12 wa kampeni ya kuhamasisha matumizi yasiyohusisha pesa taslimu iliyoendeshwa na Benki ya NMB kwa miezi mitatu ‘NMB MastaBata – Halipoi’ na wenza wao, wamekabidhiwa tiketi za ndege za safari ya kitalii jijini Cape Town, nchini Afrika Kusini kwa ziara ya siku tano.

NMB MastaBata – Halipoi ni kampeni iliyozinduliwa Oktoba 27 mwaka jana ikiwa na zawadi zenye thamani ya zaidi ya Sh. Mil. 350, ambako kwa miezi mitatu, imezalisha jumla ya washindi 1,492, wakiwemo waliojishindia fedha taslimu, ziara ya kitalii Zanzibar na hawa wanaoenda Afrika Kusini.

Hafla ya makabidhiano ya tiketi kwa washindi hao imefanyika Makao Makuu ya NMB jijini Dar es Salaam, wakikabidhiwa na Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara, Filbert Mponzi, mbele ya Mkuu wa Idara ya Biashara ya Kadi wa benki hiyo, Philbert Casmir.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mponzi alisema kampeni hiyo ilikuwa ni sehemu ya jitihada za benki yake katika kusapoti juhudi za Serikali ya Tanzania za kujenga utamaduni chanya miongoni mwa Watanzania wa kufanya matumizi yasiyohusisha pesa taslimu ‘cashless.’

“Ilikuwa ni miezi mitatu iliyozalisha washindi 1,492 waliojinyakulia zawadi mbalimbali zenye thamani ya Sh. Mil. 350, ambako tulikuwa na washindi wa kila wiki, kila mwezi, papo kwa papo, wa ziara ya utalii Zanzibar na tunahitimisha na hawa wa Afrika Kusini.

“Kupitia NMB MastaBata – Halipoi, tumefundisha wateja wetu na Watanzania utamaduniz wa matumizi salama yasiyo ya pesa taslimu, huku tukiwazawadia. Kwamba licha ya kufanya matumizi hayo kwa faida yao, lakini bado NMB ikawawekea washindi zawadi.

“Zawadi zetu katika msimu huu wa tano zilikuwa kubwa na ni kutokana pia na ukubwa wa benki yetu na dhamira tuliyonayo ya kugusa maisha ya walio wengi miongoni mwa Watanzania, hususani wateja wetu,” alisisitiza Mponzi.

Alibainsiha ya kuwa, mwisho wa NMB MastaBata ndio muendelezo wa kampeni nyingine, ambako kwa sasa wanaendelea kuzawadia washindi wa Kampeni ya Weka na Ushinde, inayoenda sambamba na ufunguzi wa kampeni nafuu zisizo na makato ya mwezi za NMB Pesa.

“NMB Pesa ni akaunti ambayo inafunguliwa kidigitali kwa shilingi 1,000 tu, ambako ndani yake ukiweka kianzio angalau cha Sh. 50,000 unaingia moja kwa moja kwenye droo za kujishindia zawadi mbalimbali, zikiwemo pikipiki za mizigo za matairi matatu ‘toyo.’

“Lakini pia, kupitia NMB Pesa utaweza kupata mikopo ya haraka isiyo na dhamana wala ujazaji wa fomu ya Mshiko Fasta, pamoja na masuluhisho mengine mengi ya kifedha ikiwemo kulipia bili na huduma mbalimbali,” alibainisha Mponzi.

Mponzi alisema washindi hao 12 na wenzao wakiwa Cape Town, watatembelea ‘Table Mountain,’ mbuga za Wanyama na Kisiwa cha Robben kuzuru Gereza la Victor-Vorster alilofungwa aliyekuja kuwa Rais wa Kwanza Mzalendo wa Afrika Kusini, Nelson Mandela.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Kadi NMB, Philbert Casmir, aliwapongeza washindi hao kwa ziara hiyo, huku akiwataka kuwa mabalozi wema wa benki hiyo wakiwa Afrika Kusini na hata kwa jamii ya Watanzania punde watakaporejea nchini.

Kwa niaba ya washindi hao wanaoondoka nchini alfajiri ya Februari 29, Makame Zahoro Ali wa Zanzibar, aliishukuru NMB kwa ubunifu uliozaa kampeni hiyo ya NMB MastaBata, inayompa nafasi ambayo hakuwahi kuiota ya kusafiri nje ya nchi kwa gharama za benki hiyo.

“Nilipopigiwa simu kuwa mimi ni mmoja wa washindi wa kampeni hii, nilihisi kama utapeli, lakini baadaye nikapewa maelekezo ya safari na hatimaye nikaamini kwamba safari ipo na ushindi wangu ni wa kweli. Sikutarajia kabisa kusafiri nje ya nchi, ila NMB imefanikisha hili,” alisema.