November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wizara yaahidi kuboresha, kuimarisha michezo

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Ikiwa ni saa kadhaa baada ya kumalizika kwa mashindano ya mbio zilizojipatia umaarufu kuliko mbio za nyikani, “Kili Marathon 2024”, Uongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ukiongozwa na Katibu Mkuu wake Balozi Dkt. Samwel Shelukindo umewapongeza wanariadha wa Wizara walioshiriki mbio hizo na kuahidi kuboresha mazingira ya michezo wizarani.

Akiongea na wanamichezo hao jana mjini Moshi, baada ya kumalizika kwa mashindano ya Kili Marathon 2024, Dkt. Shelukindo alisema kuwa michezo ni afya, hivyo watumishi wanapaswa kujituma kufanya mazoezi mara kwa mara siyo tu kwa ajili ya kuimarisha afya zao bali kuwawezesha pia kushiriki michezo mbalimbali ndani na Nje ya nchi.

“Natambua kuwa ndani ya Wizara yetu kuna watumishi wenye vipaji tofauti, nawasihi pamoja na ufinyu wa muda mlionao mjitahidi kufanya mazoezi ili muweze kumudu ushindani wa michezo mbalimbali na kuipaisha Wizara yetu ndani na Nje,” alisema Dkt. Shelukindo

Kwa upande wake, Katibu Mkuu anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Balozi Stephen Mbundi aliwapa hamasa wanamichezo ya kuongeza idadi ya michezo wizarani ili kupanua wigo wa watumish kushiriki na kuitaja michezo hiyo kuwa ni pamoja na mpira wa kikapu, mpira wa tenesi, michezo ya Jadi na ndondi.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara, Balozi Said Shaibu Mussa aliwataka wanamichezo wa Wizara kuendelea kujituma kwa bidii na kuwa na nidhamu ya mazoezi ili kuwawezesha kushinda michezo wanayoshiriki na kuipeperusha bendera ya Wizara vizuri kwenye kila mashindano wanayoshiriki ikiwa pamoja na kuwahimiza kuandaa bonanza za michezo yatakayoshirikisha wadau tofauti ili kuimarisha mahusiano, kukuza diplomasia ya michezo hatimaye kutangaza Wizara.

Awali akiongea katika kikao cha Viongozi na wanamichezo, Mwenyekiti wa Klabu ya Michezo Wizarani (Nje sports Club), Bw. Ismail Hamidu Abdallah aliushukuru Uongozi wa Wizara kwa kuwawezesha na kuwapa motisha wakati wote wanaposhiriki katika michezo mbalimbali.

“Tunawashukuru Viongozi wetu kwa kutuwezesha wanamichezo, kwa kweli kwa ushirikiano tunaoupata kutoka kwenu tunaahidi kuendelea kujituma kwa bidii katika michezo na kuipaisha vyema bendera ya Wizara,” amesema Bw. Ismail

Wanamichezo wa Wizara wamegawanyika katika michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, mpira wa pete kwa wanawake, volleyball, mchezo wa kuvuta kamba pamoja na riadha.