January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kamati ya Bunge yapongeza Rais Samia

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) imeipongeza Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa Uwekezaji mkubwa katika miradi ya maji eneo la Nzuguni Jijini Dodoma yenye thamani ya takribani Bilioni 5.09 inayotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA).

Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) Deus Sangu wakati wa ziara ya Wajumbe wa Kamati hiyo iliyofanyika Januari 28,2024 katika miradi mitatu ya maji ya uchimbaji na uendelezaji wa visima katika eneo la Nzuguni Mjini Dodoma.

Aidha, Sangu amemhakikishia Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA), Balozi Job Masima kuwa Kamati ya PIC itafanyia kazi kwa haraka suala la fedha za kumalizia awamu ya kwanza ya mradi wa maji Nzuguni, ambao umefikia asilima 96ili wananchi wa Nzuguni na maeneo jirani wapataoelfu 75 waweze kunufaika na mradi kwa asilimia 100.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) Balozi Job Masima amewahakikishia wananchi wa Nzuguni kuwa mradi utakamilika na watapata Majisafi kwa kuwa umefikia hatua nzuri ya utekelezajina tayari wananchi wameanza kupata huduma ya majisafi katika baadhi ya maeneo.

Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dodoma, Katibu Mwenezi wa CCM wa Mkoa Ndugu Jawadu Bakilana amewaomba wananchi kuiamini Serikali yao ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt. Samia  katika utekelezaji wa miradi ya majisafi ambayo inaendelea kutoa huduma kwa wananchi.