November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rukwa yaweka mikakati ya kukabiliana na udumavu

Na Israel Mwaisaka, TimesMajira Online,
Sumbawanga

SERIKALI mkoani Rukwa imewaomba wadau wa maendeleo wakiwemo wanahabari kushiriki katika mikakati ya kutokomeza udumavu ambao umefikia asilimia 50 na kusababisha athari kubwa kwa watoto waliopo mkoani humo.

Katibu Tawala msaidizi masuala ya Uchumi na uwezeshaji mkoani humo, Salehe Msanda alibainisha hayo Jana Ofisini kwake wakati akizungumza na wanahabari aliokutana nao kwa lengo la kuweka mikakati ya pamoja katika kukabiliana na changamoto hiyo.

Alisema kuwa katika mkoa huo hali ya udumavu imefikia asilimia 50 wakati kiwango cha kitaifa ni asilimia 30.4 huku ukondefu ukiwa ni asilimia 19.4 wakati kitaifa ni asilimia 12.

Katibu tawala msaidizi huyo alisema kuwa pia takwimu zinaonesha kuwa changamoto ya uzito uliopitiliza umefikia asilimia 3.2 wakati kitaifa ni asilimia 3.5 na tatizo la uzito mdogo limefikia asilimia 8.3 huku kitaifa ukiwa ni asilimia 3.2.

Msanda alisema kuwa mkoa wa Rukwa umo Kati ya mikoa Saba inayoongoza kwa kuzalisha mazao ya nafaka pamoja na mazao mengine ya chakula na katika msimu wa kilimo uliopita ulikua ni mkoa wa pili katika uzalishaji wa chakula hapa nchini lakini bado unakabiliwa na udumavu mkubwa.

“Mahudhurio ya wajawazito Kriniki ni zaidi ya asilimia 90, pia chanjo kwa watoto wamekuwa wakipata kwa zaidi ya asilimia 90 lakini kumekuwa na changamoto ya udumavu pamoja na hizo nyinginezo, hivyo mkoa umeandaa mikakati mbali mbali ya kukabiliana na suala hilo” alisema.

Awali mkuu wa mkoa wa Rukwa, Makongoro Nyerere alisema kuwa tatizo la udumavu limekua likiathiri zaidi katika sekta ya Elimu ambapo matokeo ya wanafunzi yamekua mabaya katika mitihani ya kitaifa.

Alisema kuwa katika matokeo ya darasa la Saba yaliyopita zaidi ya wanafunzi 600 waliferi na hii inachangiwa na sababu mbali mbali ikiwemo ni pamoja na udumavu ambao unasababisha ubongo wa watoto kutokukua na kufanya kazi vizuri.

Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa ni lazima wataalamu wa lishe watoe elimu kwa wazazi ili katika siku 1,000 tangu kuzaliwa kwa mtoto aweze kupata chakula bora chenye viinilishe kamili ili vimsaidie mtoto kukua vizuri kwa ubongo wake.

Hata hivyo alisema kuwa mkoa huo utazindua kampeni maalumu kwaajili ya kutoa elimu ya lishe kwani katika mkoa huo vya kula vipo vingi Ila changamoto kubwa ni baadhi ya wakazi wake kutojua namna ya kuandaa na kula vya kula hivyo.