November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watumishi wa afya watakaokiuka taratibu kuchukuliwa hatua

Na.Judith Ferdinand, Timesmajira Online,Mwanza

Serikali imetangaza kuwachukulia hatua za kinidhamu watumishi wa afya wanaokiuka taratibu na maadili ya kazi ikiwa ni jitihada za kuboresha sekta hiyo

Kauli hiyo imetolewa Februari 20,mwaka huu na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Daktari Grace Magembe mkoani Mwanza katika ziara yake ya kukagua miradi ya afya,kuzungumza na watumishi wa afya pamoja na kusikiliza changamoto zao.

Mbali na hayo Katibu Mkuu huyo aliendelea na ziara yake wilayani Ukerewe ya kukagua ujenzi wa hospitali yenye hadhi ya rufaa katika Wilaya hiyo pamoja na miradi mingine iliyopo chini ya Wizara ya Afya.

Dkt. Magembe anasistiza kufuata maadili ya kazi katika kuwahudumia wagonjwa ili kupunguza malalamiko juu ya sekta hiyo na atayaeshindikana atachukuliwa hatua za sheria.

“Hatutaonea mtu lakini ukishindikana tutakuchukulia hatua kali wenzangu wa sekta ya afya mnatambua tukikufungia usajili huwezi kufanya kazi sehemu yoyote ndani ya nchi hii au nje ya nchi,”ameeleza Dkt.Magembe.

Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Elikana Balandya ameeleza kuwa ujenzi wa hospital yenye hadhi ya Rufaa ya Mkoa wilayani Ukerewe utakavyosaidia kupunguza mrundikano wa wagonjwa katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Sekou -Toure.

“Ukikuta meli imeisha ondoka itabidi kusubili nyingine ya siku inayofuata kutokana na adha hiyo wananchi wengi walikuwa wakipoteza maisha,tunashukuru serikali kwa maamuzi ya kuwasaidia wananchi wa Ukerewe kwa kujenga hospitali yenye hadhi ya rufaa,”ameeleza Balandya.

Naye Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando Dkt.Fabian Masaga ameelekeza kilio chake kwa serikali juu ya madai ya bima ambapo mpaka sasa wanadai zaidi ya bilioni 20.

“Zaidi ya bilioni 20 tunadai mfuko wa bima ya afya,bado hatujalipwa mpaka sasa hivi tuanomba uweze kutusaidia katika hili,”ameeleza Dkt.Massaga.

Hata hivyo mmoja wa wakazi wa Mkoa wa Mwanza Florentina Innocent ,ameeleza kuwa kuna baadhi ya kauli zinatolewa na wahudumu wa afya ambazo zinamkatisha mtu tamaa.

“Lakini unakuwa unamuuliza mtu swali kwa sababu hujui ila kauli anayokupa inakukatisha tamaa,”ameeleza.