Na George Mwigulu, Timesmajira Online,Katavi.
Serikali kupitia Wizara ya Maji imeombwa kulipa fedha za fidia kwa wananchi wa Kata ya Shanwe na Misukumilo Manispaa ya Mpanda Mkoa wa Katavi ambao maeneo yao yamepitiwa na mradi wa maji wa miji 28 wenye thamani ya zaidi ya bilioni 2 katika bwawa la Milala
Ombi hilo limetolewa na wananchi Februari 19 mwaka huu wakati Mkuu wa Mkoa wa Katavi,Mwanamvua Mrindoko akisikiliza kero za wananchi na kuzitatua kupitia utaratibu aliojiwekea.
Rehema Albert,Mkazi wa kata ya Misukumilo amemuomba Mkuu wa Mkoa huyo kuhakikisha fidia zao zinalipwa kwani ni muda mrefu wamefuatilia suala hilo bila kupata majibu ya uhakika.
“Sisi tunaomba tulipwe fidia zetu walizotuambia watatulipa ili tuweze kuondoka kwenye kikao hiki na kama haiwezekani waturudishie maeneo yetu kwa ajili ya kuendelea na kazi zetu za uzalishaji,”amesema Rehema.
Andrew Misonge amesema baada ya madai yao kupelekwa mezani kwa Mkuu wa Mkoa wa Katavi amesema atafuatilia ambapo kwa sasa ni muda mrefu umepita bila kupata mafanikio yoyote licha ya kuhamishwa,nyumba zao kubomoka, tathimini imeshafanwa na siku 90 zimeshapita.
“Kwani sheria inasemaje kuhusu ardhi?,ukiangalia kwa uhalisia kuna wazazi watoto wao tayari wanasoma leo hii wanashindwa kwenda shule kwa sababu ya miundombinu mibovu wamekataa kufanya shughuli yoyote kwenye eneo hilo sasa wanaishije?,”amesema.
Amesema ni mikutano takribani mitano wamefanya kupitia ziara za Mkuu wa Mkoa lakini majibu ni yale yale yanayotolewa kila wakati
“Kimsingi tulifahamu kuwa leo kama siku ya kusuluhisha migogoro kutakuwa na neema kwa wakazi wa kata zote hizi mbili Misukumilo na Shanwe kuwa suala letu litapatiwa ufumbuzi wa majibu ili wananchi turudi kwa furaha lakini tunarudi kwa majozi,”amesisitiza.
Peter Matyampula amesema licha ya tathimini kufanywa na pindi wanapofuatilia majibu yamekuwa mepesi wanayopatiwa na viongozi kwa kuambiwa madai yao yapo ngazi za juu.
Amesema Kamishna wa Ardhi aliwapatia maelezo kwamba fidia watalipwa hadi miezi sita jambo ambalo walikataa kwa maana sheria ya ardhi inasema(hakutaja kifungu cha sheria hiyo) kwamba idara au taasisi yoyote inapotaka kutwaa ardhi kutoka kwa wananchi ni lazima fedha zitengwe za kuwalipa.
Mkuu wa Mkoa wa Katavi,Mwanamvua Mrindoko amesema malalamiko ya wananchi yanayohusu ucheleweshaji wa malipo ya fedha zao za fidia suala hilo la malipo yanatoka Wizara ya Maji na wao kama Mkoa jukumu lao lilikuwa ni kusimamia tathimini la eneo la bwawa la Milala.
Mrindoko amesema serikali ya Mkoa wa Katavi ilishapeleka majendwali kupitia ofisi ya Katibu Tawala Mkoa ambapo kwa sasa iliyobaki ni Wizara ya Maji kukamilisha utaratibu wa malipo ili wananchi waweze kulipwa.
“Kwa maana ya usikilizaji wa kero wa leo hapa Mpanda kama Waziri atakuwa ananisikia basi nimuombe jambo lile katika bwawa la Milala lifanyiwe kwa haraka kwa sababu wananchi hawa wamesubili kwa muda mrefu na wameshatii kupisha mradi kwaio tuwalipe mapema kama serikali ili tuweze kuendele vizuri na ule mradi wa maji wa miji 28,”amesema Mrindoko.
More Stories
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa