November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jiji la Mbeya laanza kukarabati shule za msingi kongwe

Na Esther Macha, TimesmajiraOnline,Mbeya

HALMASHAURI ya Jiji la Mbeya imeanza kuboresha na kukarabati miundombinu ya Shule kongwe za msingi na Sekondari ili kuendana na hadhi ya Jiji kutokana na uchakavu kufuatia kujengwa kwa miaka mingi.

Kauli hiyo imetolewa na Mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya Dormohamed Issa wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusiana na utekelezaji wa miradi mbalimbali katika sekta ya elimu,afya, miundombinu .

Amesema kuwa maboma 54 wamepelekwa bati na mbao ili ziweze kusaidia kuezeka katika shule za msingi ambazo ni chakavu na tumeanza kwa msingi Ilomba ambayo imejengwa kwa miaka mingi .

“Tumeanza na shule za msingi ambazo ni chakavu na tukianzia na shule ya msingi Ilomba ambako tumepeleka mil.150, ambayo imejengwa mwaka 1954, tukimaliza hii tunaangalia shule nyingine kongwe zilizojengwa miaka mingi na zenye uchakavu “amesema Mstahiki Meya .

Aidha Issa amesema kuwa lengo la ukarabati huo ni kuhakikisha kuwa shule zote kongwe za Jiji la Mbeya zinakuwa na hadhi na kubadilika.

Hata hivyo Issa ameekeza kuwa wameanza na ukarabati wa shule hizo kongwe kutokana na na kujengwa kwa muda mrefu hivyo kuwa uchakavu.

“Tumeanza kwa awamu kwenye ukarabati kwa kuanza na shule ya msingi Ilomba,Sinde, Nzovwe,Mwakibete,,Uyole na Ilomba “amesema Mstahiki Meya huyo wa Jiji.

Kwa upande wake Mwalimu mkuu wa shule ya Msingi Isanga ,Abdilah Mdeck amesema Shule hiyo ilianzishwa mwaka 1975 ina walimu 18 na waliopo 17 ambapo kati hao mmoja yupo masomoni huku idadi ya wanafunzi wakiwa 701 wasichana ni 365 na wavulana 336.

Mdeck alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia shule hiyo fedha kwa ajili ya ukarabati wa shule hiyo ambayo ilikuwa chakavu kutokana na kujengwa kwa muda mrefu ambapo tayari ilishakuwa na uchakavu wa vyumba vya madarasa pamoja vyoo.

“Tunamshukuru Mstahiki Meya wa Jiji letu kwa msukumo mkubwa kuhakikisha shule yetu inapatiwa mil.20 za ukarabati wa vyumba viwili vya madarasa ambavyo tayari vipo hatua za mwisho za umaliziaji ,vyumba vyenye uchakavu ni 11 lakini tumeanza na hivi vyumba viwili kwanza na hii fedha tuliyopewa”amesema Mkuu huyo wa shule.