October 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Katibu Mkuu Wizara ya Afya (Upande wa Ustawi wa Jamii) akizungumza na baadhi ya waandishi wa habari alipotembelea Banda la Shirika la Taifa la Maendeleo(NDC) kwenye Maonesho ya Sabasaba barabara ya Kilwa, jijini Dar es salaam leo.

Mchango wa wanawake watajwa kuifikisha nchi uchumi wa kati

Na Mwandishi Wetu

MCHANGO wa wanawake katika kuanzisha viwanda vidogo vidogo nchini umetajwa kusaidia kukuza uchumi na hivyo mchango wao umewezesha Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zenye uchumi wa kati.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya (Upande wa Ustawi wa Jamii) Dkt. John Jingu, wakati akizungumza na waandishi wa habari alipotembelea Banda la Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC) kwenye Maonesho ya 44 ya Kimataifa ya Biashara yanayoendelea kwenye Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam ili kujionesha shughuli zinazotekelezwa na shirika hilo.

Amesema Serikali imewatengeneza wanawake mazingira ya kuwawezesha kiuchumi kwa kutumia mfuko maalum kwa ajili ya uwezeshaji wanawake kiuchumi, lakini pia kuna fedha ambazo zinatolewa na halmashauri kutoka asilimia 10 ya mapato ya ndani.

“Asilimia nne kwa ajili ya akina mama, asilimia nne kwa ajili vijana na asilimia mbili ni kwa ajili ya watu wenye ulemavu,” amesema.
Dkt. Jingu amesema kuanza mwaka 2015 hadi sasa halmashauri zimetoa takribani ya sh. bilioni 40 kwa ajili ya makundi hayo. “Na akina mama zaidi 800,000 wameishanufaika sana, ukienda kwenye mabanda yao (yaliyopo Sabasaba) utaona kazi kubwa ambayo akina mama hao wamefanya, kuna viwamda vidogo vidogo vinazalisha bidhaa mbalimbali ambapo nyingine zinastahili kuingia kwenye masoko ya kimataifa,” amesema Jingu.

Amesema kuingia kwa Tanzania kwenye uchumi wa kati maana yake mafanikio hayo yametokana na mjumuiko wa shughuli mbalimbali zinazofanywa na Watanzania wote, zikiwemo zinazofanywa na wawekezaji wakubwa kama NDC na wengine.

“Lakini hata hawa wadogo wadogo, akina mama kwa kuanzisha viwanda vidogo vidogo wametoa mchango kubwa kwa sababu wametengeneza ajira, wametengeneza kodi,wanatengeneza soko kwa bidhaa zingine mbalimbali.

Kwa hiyo wakishapata fedha watapeleka watoto shule, watapeleka watoto hospitalini na watanunua bidhaa mbalimbali kwa hiyo uchumi na maisha ya wananchi yanaendelea kuwa mazuri.”

Kwa msingi huo amesema ndiyo maana wanasema tumeingia kwenye uchumi wa kati kutokana na mazingira mazuri ambayo yamewekwa na Serikali kwa kuwawezesha wadau mbalimbali hasa hasa wadogo, wakiwemo akina mama, kwani na wao wametoa mchango mkubwa katika ustawi wa uchumi wa nchi yetu.