Na Tito Mselem, Shinyanga
Hayo ameyasema alipofanya ziara yake kwenye mgodi huo mara baada ya kuona matangazo ya kuuzwa kwa mgodi huo kwenye mitandao ya kijamii.
Waziri Biteko amesema, Serikali inaubia wa asilimia 25 katika mgodi wa WDL, haiwezekani utake kuuzwa bila mmbia wake kufahamu kitendo hicho ni kukiuka taratbu na sheria za nchi.
Kutokana na kitendo hicho, Waziri Biteko ameuagiza uongozi wa mgodi huo kufikia Julai 10, mwaka huu wawe wametoa maelezo kwa maandishi kueleza sababu za kutaka kuuza mgodi huo bila mmbia wake ambaye ni Serikali kujua na pia, kutoa taarifa ya kuwapunguza kazi wafanyakazi kisha kuwalipa nusu mshahara.
Amesema, wafanyakazi waliopunguzwa kazi kwa kutumia kigezo cha ugonjwa wa Corona utaratibu uliotumiwa haufai na wao kama Wizara ya Madini hawakubaliani nao kutokana na kulipwa mishahara nusu jambo ambalo linawapa wakati mgumu na kusababisha migogoro isiyo ya lazima.
Aidha, Waziri Biteko amesema, sababu ambazo wanazitoa mgodi huo za kusitisha shughuli za uzalishaji na kutaka kuuza mgodi huo ni kushuka kwa bei ya almasi duniani iliyosababishwa na ugonjwa wa corona, ambapo alieleza kuwa sababu hizo hazina mashiko ila wawe wakweli kama wamefilisika ijulikane.
Waziri Biteko amesema sababu kubwa ambayo ingefanya mgodi huo kufungwa ni kushuka kwa uzalishaji na siyo uendeshaji, huku akihoji kama mgodi hauna fedha za kujiendesha wangesema badala ya kuweka matangazo kwenye mitandao mgodi unauzwa wakati serikali haina taarifa.
Kwa upande wake meneja mkuu wa mgodi huo, Mhandisi Ayoub Mwenda amekiri kuwa hawakutoa taarifa Serikalini juu ya kutaka kuuzwa kwa mgodi huo, huku akieleza kuwa walifunga mgodi huo Aprili 8, mwaka huu kutokana na kushindwa kujiendesha na ameahidi kufuata maelekezo yote ambayo yametolewa na Waziri wa Madini.
Mhandisi Mwenda amesema, walikuwa wanazalisha vizuri kabla ya mlipuko wa ugonjwa wa Corona ambapo kwa mchanga waliokuwa wameuzalisha walikuwa mbele kwa asilimia tatu na almasi walizokuwa wamezikusanya walikuwa mbele kwa asilimia 9.1 kulingana na bajeti yao waliyokuwa wameiweka.
Amesema, tatizo la Corona limeuathiri sana mgodi huo na kusimama kufanya shughuli za uzalishaji kutokana na kushuka bei ya masoko ya nje ambapo kabla ya Corona bei ilikuwa dola 246 kwa karati moja ambapo Machi, mwaka huu waliuza karati moja dola 135 ambayo ilikuwa haiwezi kutosheleza gharama za uzalishaji.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Talaba ameipongeza Wizara ya Madini kwa kazi nzuri wanazozifanya ambapo wamesaidia nchi kuingia katika uchumi wa kati.
More Stories
CRDB yazindua matawi Majimoto, Ilula kuwahudumia wananchi
Lina PG Tour yafufua gofu Moshi
Kampeni ya Sako kwa Bako yawafikia Kanda ya Kati