November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

JKT launga mkono juhudi za Serikali kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
 
WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt Stargomena Tax ameiasa jamii kutunza mazingira kwa kupanda miti pamoja na kuifuatilia ili ikue vizuri na kupata matokeo ya upandwaji wa miti hiyo.

Dkt.Tax ameyasema hayo katika zoezi la upandaji miti kuelekea maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano  wa Tanganyika na Zanzibar ,lililofanyika katika Makao Makuu ya JKT Chamwino Mkoani Dodoma.
 
“Ninachopenda kusisitiza  ni kwamba isiwe tunakutana tu kupanda miti na hapa tumeoneshwa mfano kwa hiyo nawapongeza sana JKT kwamba hii miti tunayoiona imestawi imepandwa na JKT ,ninawahakikishia tukija mwakani hii tuliyoipanda leo tutaiona ,

“Hii ni kwa sababu inatunzwa na kwa sababu JKT limeamua kuhakikisha kwamba maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ni kinara katika kuifanya Tanzania kuwa ya kijani na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi .”amesema Dkt.Tax
 
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa JKT ambaye pia ni Mkuu wa Tawi la Utawala  JKT Brigedia Jenerali Hassan Mabena amesema,katika kuhakikisha mazingira yanatunzwa,JKT limeanza kutumia nishati mbadala katika vikosi vyake ili kuzuia matumizi makubwa ya kuni na mkaa na hivyo kupunguza athari za ukataji miti.
 
Aidha amesema JKT limeendelea kupanda miti katika maeneo mbalimbali ya vikosi vyake huku akisema upandaji huo wa miti umekuwa ukiendelea vyema ambapo JKT limekuwa likiandaa vitalu vya miche kwa matumizi ya vikosi na wananchi wanaozunguka maeneo ya vikosi.
 
“Jeshi la Kujenga linaendelea kuotesha na kupanda miti ya aina mbalimbali ikiwemo mikongo na mininga katika maeneo ya vikosi pamoja na kugawa miche kwa wananchi ambapo kwa mwaka 2023,JKT kupitia vikosi vyake limefanikiwa kuotesha na kupanda miti ya kivuli,mbao na matunda ipatayo 75,800.”alisema Brigedia Jenerali Mabena na kuongeza kuwa
“JKT linatarajia kuendelea kupanda miti ya aina mbvalimbali kwa mwaka huu ipatayo 100,000 kwa vikosi vyake vyote.”


Naye Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Khamis Hamza Khamis amesema Ofisi ya Makamu wa Rais bado inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu athari za ukataji miti kwani inaonekana bado jamii haina uelewa wa kutosha kuhusu suala la utunzaji wa mazingira kwa ujumla.
 
Ametumia nafasi hiyo kuipongeza JKT kwa kuanza kutumia nishati mbadala huku akisema huo ni utekelezaji wa melekezo ya Serikali yaliyotaka taasisi zenye watu kuanzia 1000 zianze kutumia nishati mbadala ili kunusuru mazingira.
 
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule naye amelipongeza JKT kwa kutunza mazingira kwa kupanda miti mingi hasa katika chanzo cha maji Mzakwe ambacho ndio tegemeo kwa mkoa wa Dodoma.