Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online, Dar
NAIBU Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mussa Azan Zungu, amewataka wanawake kuchangamkia fursa ya mikopo isiyo na riba inayotarajiwa kuanza kutolewa hivi karibuni na kuachana na mikopo umiza.
Zungu ameyasema hayo leo Jijini Dar es Salaam, wakati akifungua Kongamano la Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Tanzania, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.
Ambapo amesema, mikopo hiyo, awali ilisitishwa na inatarajiwa kurudi tena hivi karibuni kwa utaratibu maalumu, huku akiwasisitiza wanawake hao kutoiacha fursa hiyo.
“Mikopo ambayo iliondolewa itarudi hivi karibuni kwa utaratibu maalumu, hivyo napenda kuwasisitizia wanawake msiache kuitumia fursa hii kwani mikopo yake haina ukomo wa umri kwa wanawake,” amesema Zungu.
Pia, alimtaka Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Jomaary Satura, kupinga vitendo vya uonevu vinavyofanywa na baadhi ya watu dhidi ya wajasiriamali, hususani wanawake isipokuwa wapangwe katika maeneo rasmi ya biashara.
“Nikuombe Mkuu wa Wilaya ya Ilala na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji, kama ulivyosema ndugu yangu Mpogolo, kuwa kuna watu bado wanawanyanyasa hawa wakina mama katika biashara zao, unakuta mama wa watu amebeba tenga la matunda kichwani katembea umbali mrefu alafu mwingine anakuja kumwaga bidhaa zake, hii haifai”, amesema Zungu.
Hata hivyo, Zungu amesisitiza juu ya upendo kwa wanawake hao na kumtaka kila mmoja kuwa na wivu wa maendeleo na mwenzake na si wivu wa mavazi.
“Kikubwa katika yote pendaneni, wanawake ni Jeshi kubwa mno mkipendana inapendeza, kila mmoja amuonee wivu wa maendeleo mwenzake na siyo wivu wa mavazi, mwanamke wa kitanzania huna sababu ya kutamani kijipamba sana kwani nyie mmeumbwa na uzuri wa hasiri”, amesisitiza Zungu.
Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, ambaye pia ni mlezi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, ameyapongeza Majukwaa ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi nchini, kwa ngazi ya Wilaya na mkoa kwa kuendelea kutambua na kuziunga mkono juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Hata hivyo, aliahidi kuwa Serikali itaendelea kutoa ushirikiano katika Majukwaa hayo, ikiwa pamoja na kutatua changamoto zinazowakabili wanawake nchini, huku akiyasisitizia Majukwaa 14 ambayo bado hayajahusisha taarifa zake, Hadi kufikia Februari mwakani yawe yamehusisha.
“Niwapongeze sana kwa maandalizi haya mazuri mliyofanya katika shughuli hii ya leo, lakini pia kwa umoja wenu kuendelea kumpongeza na kutambua jitihada ambazo zinaendelea kufanywa na Rais Dkt Samia. Niwahakikishie kuwa, Serikali kwa ngazi ya Wilaya na Mkoa tutaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwenu.
Pia, changamoto zote mnazokabiliana nazo tutaendelea kuzitatua hadi pale tutakapofanikiwa kuzikomesha, mfano mdogo ni pale Mama anapokuwa ametoka kupika zake chakula kwa ajili ya kwenda kuuza alafu Kuna mtoto wa mama naye anaenda kukimwaga, hii siyo sawa hivyo changamoto ikiwa pamoja na za aina hiyo tunaenda kuzikomesha,” amesema Mpogolo.
Hata hivyo, Mpogolo amewataka wanawake hao kuacha kujihusisha na mikopo yenye riba kubwa maarufu kama ‘Kausha Damu’ huku akiwataka wenyeviti wa Mitaa kutotoa ushirikiano kwa wanaotaka mikopo ya aina hiyo.
Nae, Mwenyekiti wa Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi, Wilaya ya Ilala, Rehema Sanga, amewataka wanawake kuwa na umoja na mshikamano ili kuweza kufika malengo waliyojiwekea.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi