November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wawili wapoteza maisha kwa “uyoga” wenye sumu

Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Watu wawili wa familia mbili tofauti mkoani Mwanza wamepoteza maisha kutokana na kula chakula(uyoga) kinachodaiwa kuwa na sumu huku wengine 7 wakiendelea na matibabu katika hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando.

Ambapo inadaiwa kuwa watu hao wa familia hizo mbili walienda kununua mboga katika sehemu moja ya magenge yaliopo jirani na makazi yao hata hivyo wamezoea kununua uyoga kutoka kwa mtu mmoja ambaye ndiye amewauzia uyoga huo.

Akizungumza Desemba 18,2023 mkoani hapa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza SACP. Wilbroad Mutafungwa ameeleza kuwa
tukio hilo lilitokea Desemba 17,2023 ambapo Maua Mwilikwa mwenye umri wa miaka 10 mkazi wa Mabatini wilayani Nyamagana mkoani Mwanza alipoteza maisha katika hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando majira ya saa 11 alfajiri.

Huku Thomas Thomas mwenye umri wa miaka 18 mkazi wa Mabatini alifariki katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Sekou-Toure Desemba 17,20203 majira ya saa 8,mchana akiwa anapatiwa matibabu.

“Watu hawa walifikishwa katika hospitali hizo kwa matibabu baada ya kuanza kutapika na kuharisha kutokana na kula mboga aina ya uyoga,waliopoteza maisha wametoka katika familia mbili tofauti,familia ya kwanza ya mzee Zuberi Msabaha(70) mkazi wa Mabatini Kaskazini aliye fariki ni mjukuu wake aitwaye Maua Mwilikwa,”ameeleza SACP.Mutafungwa na kuongeza kuwa

“Familia ya pili ni ya Eva Jonas(47), mkazi wa Mabatini Mashariki ambapo watu 7 walikula mboga hiyo na baada ya muda mfupi walianza kutapika kisha kukimbizwa kituo cha afya cha Polisi Mabatini ambapo baada ya hali zao kutoridhisha walipelekwa katika hospitali ya Sekou-Toure kwa matibabu zaidi na ilipofika tarehe 17.12.2023 Thomas Thomas mtoto wa Eva Jonas alifariki dunia muda wa saa 8, mchana akiwa anaendelea kupatiwa matibabu,”.

Mutafungwa ameeleza kuwa waathiriwa wanaoendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando ni Maua Ibrahimu(56), Eva Jonas (47),Edina Thomas (20),John Thomas (15), Tomision Thomas(13) mwanafunzi wa kidato cha kwanza shule ya sekondari Mtoni, Grelious Simoni (1) na Alfani Selemani (14) mwanafunzi na hali zao zinaendelea vizuri.

Pia ameeleza kuwa jeshi hilo linaendelea na jitihada za kumtafuta mtu aliyewauzia uyoga huo ili aweze kuhojiwa na kueleza aliutoa wapi na kuuzia watu na kusababisha madhara huku akitoa rai kwa wananchi wa Mkoa wa Mwanza kuwa makini na baadhi ya vyakula visivyofaa.