November 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Miaka 62 ya Uhuru na ushujaa wa Rais Samia Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote

Na ReubenKagarukiTimesmajiraOmline,Dar

LEO Watanzania wanaadhimisha miaka 62 ya Uhuru wa Tanganyika, ikiwa ni kwa mara ya kwanza maadhimisho hayo kufanyika Tanzania ikiwa imepitisha Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote.

Tangu Tanzania ipate huu, Tanzania haikuwahi kuwa na sheria hiyo, lakini hata wazo hilo lilipoanzishwa miaka 21 iliyopita ilishindikana kupatikana kwa sheria hiyo.

Leo hii ambapo Tanzania inaadhimisha miaka 62 ya Uhuru, jina la Rais Samia Suluhu Hassan, likiwa linaingia tena kwenye vitabu vya kumbukumbu, akiwa ni Rais aliyefanikisha kutungwa kwa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, akiwapiku marais watano waliomtangulia.

Kwa kipindi chote cha miaka 62 ya Uhuru hadi leo, ilikuwa ni safari ndefu kuweza kuandika historia hii, lakini Rais Samia kutokana na uongozi wake thabiti ameweza kufanikisha kutungwa kwa sheria hii, ambayo haikuwa kazi rahisi.

Hilo linawekwa wazi na Kamishna wa TIRA, Dkt. Baghayo Saqware, ambaye anampongeza Rais Samia kutokana na miongozo yake ambayo anatoa, kwani imekuwa ikisaidia sekta ya bima.

“Kama ambavyo mnafahamu Rais Samia amesaini muswada wa Bima ya Afya kwa Wote na sisi kama TIRA, tuko tayari kuendesha na kusimamia biashara ya bima nchini,” alisema Dkt. Saqware.

Dkt. Saqware ametoa kauli hiyo wiki hii wakati wa uzinduzi wa Taarifa wa Taarifa za Utendaji wa Soko la Bima kwa mwaka 2022.

Rais Samia, amesaini muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote kunawafanya Watanzania kuadhimisha Uhuru wakiwa na jambo lingine jipya la kujivunia mkononi mwao.

Uamuzi wa Rais Samia kusaini muswaada huo ulikuja baada Novemba 2, 2023, Bunge kupitisha muswada huo kwa asilimia 100 na kuweka historia, baada ya mkwamo uliokuwepo kwa takribani miaka mitano, tangu ulipofufuliwa upya mwaka 2018.

Mchakato huo wa kupata Bima ya Afya kwa Wote, ulikuwepo miaka 21 iliyopita, lakini ulikwama kupita.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Afya Desemba 4, 2023 imesema muswada huo sasa umeshasainiwa na Rais na kuwa sheria kamili, baada ya kutangazwa kwenye gazeti la Serikali Desemba Mosi, 2023.

Saini ya Rais katika sheria hiyo, inaipa kazi Wizara ya Afya kuanza utungaji wa kanuni kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa sheria hiyo, ambayo itawezesha kila Mtanzania kupata huduma za afya pasipo na kikwazo cha kiuchumi.

Katika kufanikisha hayo Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na masuala ya UKIMWI iliweka msisitizo wa umuhimu wa kuwa na mfuko kwa ajili ya kugharamia bima ya afya kwa watu wasio na uwezo.

Kamati hiyo ilitaka Serikali iusimamie kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora za afya.

Kupitia sheria hiyo kutakuwa na utaratibu wa utambuzi na usajili wa kundi la watu wasio na uwezo, kwa lengo la kuhakikisha wanapata huduma za afya bila kikwazo cha fedha.

Kundi hilo litajumuishwa kwenye skimu ya Bima ya Afya ya Umma kwa namna itakavyoainishwa kwenye kanuni zitakazotungwa hapo baadaye, huku akibainisha vyanzo vya mapato vitakavyotumika kugharamia skimu hiyo.

Akiusoma muswada huo bungeni kwa mara ya mwisho, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema vyanzo vya mapato ya skimu hiyo ni pamoja na sehemu ya mapato yatokanayo na ushuru wa bidhaa.

“Kwenye vinywaji vyenye kaboni, vinywaji vikali, bidhaa za vipodozi, kodi ya michezo ya kubahatisha, ada ya bima za vyombo vya moto na mapato yatokanayo na ushuru wa miamala ya kielektroniki ” alisema Waziri Ummy.

Aliuhakikishia umma wa Watanzania juu ya huduma za matibabu kwa kundi la wananchi wasio na uwezo.

Akizungumza wiki hii kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba, kwenye uzinduzi wa Taarifa wa Taarifa za Utendaji wa Soko la Bima kwa mwaka 2022, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Damas Ndumbaro, alisema;

“Safari ya kuwa na Bima ya Afya ni ya muda mrefu sana, imechukua miaka 21.

Ni kitu ambacho watu wamekisubiri kwa miaka 21, lazima wahakikishe wanakitumia vizuri, kwa sababu bima ya afya kwa wote ni haki za binadamu.”

*** Ndumbaro: Inaleta usawa kati ya tajiri, maskini

Dkt. Ndumbaro anasema kila mtu apate huduma sawa. “Tukishakuwa na bima ya afya, uwe tajiri, uwe maskini wote mpo sawa, kwa hiyo utekelezaji wa hii sio tu utekelezaji wa Malengo ya Milenia, lakini kwetu ni utekelezaji wa Ibara ya 13 ya katiba ambayo inasisitiza usawa kwa wote.”

Anawataka wadau wa bima wajitaidi washirikiane na TIRA ili Watanzania wengi waweza kumudu hivyo vifurushi, wakiwemo wananchi wa chini kabisa ili waweze kuzimudu.

***Ni mwarobani ya miili ya waliokufa kuzuiliwa mochwari

Mmoja wa wataalam wa masuala ya bima, James Edward, anasema kusainiwa kwa sheria hiyo kutakuwa mbombozi kwa Watanzania, kwani kuanzia sasa hakuna Mtanzania atakayekufa na mwili wake kuzuiliwa mochwari, kwa ndugu zake kudaiwa fedha za matibabu.

“Huko nyuma kuna watu walikuwa wanafika hospitali hawana hela na baada ya kutibiwa wanapona, ndipo walitakiwa kulipa hela, lakini waliofariki, ndugu walidaiwa fedha na walioshindwa, mwili wa mpendwa wao ulizuiliwa mochwari,” anasema Edward.

Anasema huo ulikuwa udhalilishaji wa familia ya marehemu na hata aliyekufa, lakini hilo Rais Samia amelimaliza kwa kusaini sheria hiyo ya Bima ya Afya kwa Wote.

“Kwanza kwa mujibu wa katiba yetu kila mtu anastahili kupata huduma ya afya, ni kinyume cha sheria kumkatalia mtu huduma, labda tungebadili katiba kwanza,” Anasema .

Ikumbukwe kwamba Rais Samia aliwahi kupiga marufuku hospitali, ambapo baadaye Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Profesa Abeal Makubu, alipiga marufuku watendaji wa hospitali na vituo vya afya vilivyo nchini, kuzuia maiti kuchukuliwa na ndugu.

Mdau mwingine wa sekta ya Bima, Joel Amos, anasema kusainiwa kwa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote kunaleta matumaini makubwa kwa wananchi kwa kuwa utekelezaji wake utawezesha wananchi wote kupata huduma za matibabu bila vikwazo.

Sheria hii tayari imeshasainiwa na Rais Samia Suluhu Hassan baada ya kupitishwa na Bunge la Jamhuri ya Tanzania Novemba mwaka huu na sasa inasubiriwa kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali kwa ajili ya kuanza utekelezaji wake.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, kila mwananchi atakuwa na uhuru wa kuchagua skimu ya bima ya afya na kujiunga nayo ili kumwezesha kupata huduma za matibabu wakati wowote anapohitaji.

Sheria hiyo inaweka Mfumo wa Bima ya Afya kwa Wote ambapo makundi mbalimbali yatajumuishwa ikiwa ni pamoja na Watumishi wa Umma na wa sekta binafsi, waliojiajiri wenyewe katika sekta isiyo rasmi na wananchi wasio na uwezo ambao sheria imeweka utaratibu wa kuwawezesha kuwa na bima ya afya.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro akizungumza na Wajumbe (hawapo pichani) wa Bodi ya Chama cha Wasafirishaji Watalii (TATO).

Kuwepo kwa Sheria hii kuna faida ambazo hazikuweza kupatikana awali kutokana na kuwepo na wachache waliojiunga na kunufaika na hivyo kufanya kuwepo kwa kundi kubwa wasio nufaika.

Sheria hii itawezesha uhakika wa matibu kwa wote; kuimarisha uboreshaji wa huduma katika vituo vya kutolea huduma za afya vya Umma na binafsi, ikiwa ni pamoja na kuimarika kwa upatikanaji wa dawa, vitendanishi na vifaa tiba.

Manufaa mengine ni kuimarika kwa uhimilivu na ustahimilivu wa Skimu za bima ya afya kutoa huduma kwa kuwa wananchi watapaswa kuchangia kabla ya kuugua katika Skimu za Bima ya Afya.

Serikali imeshawekeza kwenye miundombinu ya afya. Lililobaki ni wananchi sasa kuwa na uwezo wa kukuzipata huduma hizo na Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ndio suluhisho.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, anasema lengo la Bima ya Afya kwa Wote ni kuchangiana kwa gharama za matibabu kwa wananchi wote, ikiwemo wale ambao hawana uwezo ambao kwa kiasi kikubwa ndio wanaohangaika kutafuta huduma za matibabu wanapougua.

Waziri Ummy anasema kuwa asilimia 15 tu ya Watanzania ndio wamejiunga na kunufaika na bima afya, ambapo asilimia 99 wamejiunga na bima wakati wakiwa wagonjwa kitu kinachoondoa dhana ya bima, kwani mtu anatakiwa ajiunge kabla ya kuugua.

Kutokana na umuhimu huo wa Bima, Serikali kwa kushirikiana na wadau inaendelea kutoa elimu kwa makundi mbalimbali katika jamii ili kujenga uelewa mpana wa umuhimu wa kila mwananchi kuwa na bima ya afya kama nyenzo itakayomsaidia kupata matibabu wakati wote bila kujali hali yake ya kipato kwa wakati huo.