Na Mwandishi wetu
MAKAMU Mkuu wa Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili(MUHAS),Prof. Bruno Sunguya ametoa rai kwa taasisi mbalimbali nchini ikiwemo zile zinazofanya tafiti kuendelea kuibua vipaji vya wanasayansi chipukizi wakiwemo wanafunzi wa shule za sekondari mbalimbali ili kuweza kuwajengea uwezo wa kuja kuwa watafiti wakubwa miaka ijayo.
Hayo ameyasema jana kwaniaba ya Waziri wa Elimu Prof.Aldof Mkenda wakati akizungumza katika hafla ya kutoa tuzo kwa wanafunzi waliofanya vizuri katika kuandaa miradi ya kibunifu inayolenga kutatua matatizo kwenye jamii chini ya mwamvuli wa YST.
Amesema kuna umuhimu wa mchango wa taasisi mbalimbali kuhamasisha programu kama hizi katika kuhakikisha zinachachusha na kuchechemua hali ya ubunifu kusaidia wanasayansi hawa chipukizi wanawekewa nguvu.
Amesema uwepo wa Klabu za sayansi katika shule na walimu wa masomo ya sayansi wamekuwa ni miongoni mwa watu ambao wamekuwa wakihamasisha masomo haya sayansi kupendwa zaidi.
Prof. Sunguya amesema miradi kama hiyo inapaswa kuwa mfano wa kuigwa kwani inaonyesha kuna hazina kubwa kwa Tanzania katika kuiendeleza Sayansi,Teknolojia na Hisabati ambapo ni masomo ambayo yanapata msukumo wa kipekee kwa wanasayansi hao chipukizi.
”Ni rai yangu tuendelee kuibua vipaji kama hivi ,kuvipanua zaidi na kuweza kufanya matamasha kama haya katika ngazi za mikoa ili kuweza kupata vipaji zaidi na kupata miradi zaidi ya vijana na kupata vijana ambao wanaweza kuwa washindani katika ngazi za taifa,”amesema.
Amesema mashindano hayo ni muhimu kwa vijana ambao ni wanasayansi chipukizi kwani yanahamasisha fikra,ubunifu hasa kwa upande wa sayansi na teknolojia kwani nchi inapoelekea inahitaji wanasayansi wengi zaidi.
Prof. Sunguya amesema ni muhimu kwa taasisi kuhakikisha wanaona ni namna gani wanaweza kuwataarisha vijana hao wakiwa na umri mdogo ambapo ndio wanakuwa na uwezo unaobadilika.
”Nimeshuhudia bunifu mbalimbali zimefanywa na wanafunzi hawa zipo za Sayansi,Mabadiliko ya tabianchi,Fizikia,Kemia ,Madawa Kilimo,tunawashukuru kampuni zilizojitokeza katika kufanikisha maonesho haya na ugawaji wa tuzo kwa wanafunzi bora waliofanya vizuri katika bunifu zao,”amesema.
Kwa Upande wake Ofisa Uratibu wa Utafiti wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia(COSTECH), Emmanuel Girimwa,amehaidi kuendeleza bunifu zinazofanywa na wanafunzi wa shule za sekondari wanaoibuliwa na Taasisi ya Wanasayansi Chipukizi(YST), kutoka kwenye mikoa mbalimbali nchini.
Girimwa alisema wamebaini kwamba kazi za kibunifu zinazofanywa na wanafunzi hao ni nzuri na muhimu hivyo zinapaswa kuendelezwa.
“Tumeona kazi nzuri ambazo mmezifanya, tuna deni la kulipa kwenu na kama serikali tunawahakikishia kwamba jukumu letu sisi ni kuhakikisha kwamba tunalipa deni hili kwa kazi tulizoziona hapa,” amesema Girimwa.
Kwa upande wake Mwanzilishi mwenza wa shirikisho hilo, Dk Gozibert Kamugisha amesema maonesho hayo yanafanyika ili kutambua mchango mkubwa hasa wa ubunifu na utafiti unaofanywa na wanafunzi mbalimbali wa sekondari.
Amesema ni mwaka wa 13 sasa wanafanya maonesho haya ambayo yamekuwa yakisisitiza teknolojia kwani YST inaibua na kutengeneza wanasayansi wachanga nchini.
Aidha Mwakilishi wa Taasisi ya Karimjee Foundation ambaye ni mdhamini mkuu wa maonesho hayo, Vinoo Somaiya amesema taassi hiyo itatoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wote watakaoshinda.
Amesema lengo la kufanya hayo ni kuendelea kuhamasisha wanafunzi kupenda kusoma masomo ya sayansi na teknolojia na hatimaye kuja kuwa wabunfu.
More Stories
Mzumbe yaanika siri ya shahada udaktari wa heshima kwa Samia
Kujenga ofisi ya kisasa,akipewa ridhaa ya Uenyekiti
Ushiriki wa Rais Samia G20 wainufaisha Tanzania