November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ubora wa shule Buhigwe warejesha wanafunzi watoro darasani

Na Allan Vicent, TimesMajira Online

MABORESHO makubwa ya miundombinu ya shule za msingi na sekondari yanayoendelea kufanywa na serikali ya awamu ya 6 yameleta neema kubwa Wilayani Buhigwe Mkoani Kigoma baada ya watoto walioacha shule kuamua kurudi darasani.

Hayo yamebainishwa jana na wazazi wa watoto wanaosoma katika shule ya msingi Munyegera iliyoko Wilayani hapa walipokuwa wakizungumza na gazeti hili.

Mzee Muhibha Lugeyeka (75) mkulima, mkazi wa Kijiji cha Munyegera kata ya Munyegera Wilayani humo amesema serikali ya awamu ya 6 imeleta mageuzi makubwa katika sekta ya elimu nchini.

Amebainisha kuwa kitendo cha Rais wa awamu ya 6 Dkt Samia Suluhu Hassan kumwaga mamilioni ya fedha katika wilaya hiyo kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mapya ya kisasa na kuboreshwa ya zamani yote kimezifanya shule zote kuwa na mwonekano bora hivyo kuwa kivutio kwa wanafunzi.

‘Shule yetu ya msingi Munyegera ilikuwa imechakaa sana hali iliyopelekea kuongezeka utoro na baadhi ya watoto kuamua kuacha shule kabisa, lakini sasa wameanza kurudi,’ amesema.

Mama Ashura Kizwizi (40) mkazi wa Kitongoji cha shule katika kata hiyo amesema maboresho makubwa ya miundombinu ya shule hiyo yameleta ari mpya kwa watoto kupenda shule, yamepunguza kwa kiasi kikubwa utoro, yameongeza ufaulu darasani na usafi wa mazingira.

Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Fidel Ntakandi amefafanua kuwa shule hiyo iliyoanzishwa Desemba 31, 1953 madarasa yake yalikuwa yameshachoka sana lakini Mheshimiwa Rais kaibadilisha na kuwa shule ya kisasa yenye mandhari inayovutia sana.

‘Rais ametuletea zaidi ya sh mil 200 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vipya 10 vya madarasa ya kisasa, Ofisi 5 za walimu, matundu 21 ya vyoo na kukarabati madarasa ya zamani yote,’ ameeleza.

Amesema maboresho hayo yameleta neema kubwa kwa shule hiyo kwa kuongeza ufaulu wa watoto darasani, mahudhurio mengi, usajili wa watoto wa kuanza darasa la awali na la kwanza kuongezea mara dufu.

Aidha amebainisha kuwa jumla ya watoto 3 walioacha shule na kukaa nyumbani kwa miaka 4 wameomba kurudi shuleni ili kuendelea na masomo licha ya kuwa na umri mkubwa, tayari wamepokelewa na kuingizwa katika Mfumo wa MEMKWA ambao ni Mpango wa Elimu kwa Walioikosa.

Watoto wanaosoma katika shule hiyo Angela Jackson (darasa la 6) na Ali Mohamed (darasa la 5) wamemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwajengea shule bora na ya kisasa na kuahidi kuwa watasoma kwa bidii ili watimize ndoto zao za maisha.

Naye Alfons Haule ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo amemshukuru Rais Samia kwa kuwaletea zaidi ya sh bil 2 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mapya ya kisasa zaidi ya 90 na kuboreshwa ya zamani katika shule zote ikiwemo ujenzi wa matundu ya vyoo na Ofisi za walimu.

Ameeleza kuwa kuboreshwa kwa shule hizo kumechochea sekta hiyo kupata mafanikio makubwa katika wilaya hiyo.