October 9, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

wazazi msiwatenge watoto wenye ulemavu wapeni haki sawa

Na Esther Macha Timesmajira Online, Mbeya

WAKATI Tanzania ikiwa inaelekea kwenye maadhmisho ya siku ya watu wenye ulemavu duniani wazazi na walezi mkoani Mbeya wametakiwa kuacha tabia ya kuwatenga, kuwabagua, kuwaficha watoto wenye ulemavu badala yake wawape nafasi ya kutambulika kwani wanaweza kufanya vitu vikubwa kuliko kama wengine.

Akizungumza wakati wa maadhmisho ya siku ya watu wenye ulemavu na mahafali ya 14 ya shule Jumuishi ya Shirika la Child Support Tanzania (CST) Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mohamed Fakili ambaye ni Katibu Tawala Wilaya ya Mbeya amesema watoto wenye ulemavu wana haki sawa kama walivyo watoto wengine hivyo wazazi hawatakiwi kuwaweka tofauti.

Fakili amesema kuwa walimu wanaolea watoto hao wamekaa ambao watu wengine hawawezi kukaa nao kwani hata akikaa na mmoja hawezi kumsaidia hivyo amewapongeza walimu wa shule hiyo kwa moyo wa kipekee kwa malezi hayo ya watoto wenye ulemavu wa tofauti tofauti kwani si kila mtu anaweza kupata utulivu wa kuwalea.

“Tunashukuru kwa malezi ya watoto hawa mnasaidia jamii kwani wengine wangefikiri kuwa watoto wao hawawezi kupata elimu au kujifunza na kujitambua kuwa sehemu ya jamii ambayo Watanzania wanajiletea maendeleo na kukuza uchumi wa kitanzania,watoto hawa kama watapata msingi mzuri kila mmoja atakuja kuwa na uwezo mzuri wa kujifanyia shughuli zake katika kujiingizia kipato cha familia na taifa,”amesema.

Amesema imani yake ni kwamba kila mzazi aliyefika katika mahafali hayo atakuwa mjumbe mzuri jinsi watoto hao walivyo wamekaa kwa utulivu kutokana na kupata tafsiri kutoka kwa walimu wao hivyo ni vema wasitengwe wala kubaguliwa ,kufichwa wapeni nafasi

“Fanyeni hivyo kwasababu kila mtanzania ana haki sawa nafasi sawa ya kusoma na kushiriki kuchangia maendeleo ya Tanzania ,wapo hapa watoto wetu wanaweza kuwa viongozi wakubwa na wana uwezo mzuri kikubwa tuwape fursa watu wenye ulemavu wanaweza tusiwachukie wala kuwatenga watoto hawa,”amesema.

Pia amesema kuwa kuna wazazi wanaanini kuwa kuzaa mtoto mwenye ulemavu ni ushirikina au umemroga ili upate kipato na ili kumwondoa mtu kwenye mashaka hayo hakikisheni mnawapa fursa.

Emmanuel Mpelumbe ni Ofisa Utawala na Fedha ambaye alimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Child Support Tanzania Noela Msuya amesema kuwa katika jamii kumekuwa na uelewa dunia namna ya kuwahudumia watoto wenye ulemavu .

Mpelumbe amesema kuwa kuna changamoto ya mitaala isiyo rafiki kwa watoto wenye ulemavu katika kufikia malengo yao ya kielimu katika hasa upimaji bado haijawekwa katika ujumuishi.

Mzazi wa mtoto mwenye ulemavu katika shule hiyo , Paskali Ntondwe Mkazi wa Ilemi amesema kuwa anaishukuru shule hiyo kwa malezi mazuri ya watoto wao kwani wanafundishwa kwa hatua na kusema kuwa wazazi wasiwafiche watoto ndani kwa kuogopa kuchekwa na jamii .