Na Mwandishi Wetu,TimesmajiraOnline
KILIO cha muda mrefu cha Watanzania hasa wanasiasa cha kudai uchaguzi huru pamoja na mambo mengi kimeanza kupata majibu baada ya Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, kuwasilisha bungeni kwa mara ya kwanza miswada mitatu.
Miswada hiyo ni pamoja na muswada Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2023, muswada wa Sheria ya Tume ya Uchaguzi wa mwaka 2023 na muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Vyama vya Siasa wa Mwaka 2023.
Akizungumza Bungeni Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson, alisema miswada hiyo mitano itapelekwa katika kamati mbalimbali za Bunge ikiwemo ya Utawala, Katiba na Sheria.
Miswada hiyo ilishasomwa kwa mara ya kwanza na sasa itaelekezwa katika kamati husika muda utakapofika.
Kupelekwa kwa miswada hiyo, kunahitimisha ahadi ya Serikali ya kufanyia marekebisho sheria za uchaguzi mara baada ya makundi mbalimbali wakiwemo wanasiasa kutoa mapendekezo yao kuhusu sheria hizo.
Novemba 6, 2023, Waziri wa Fedha, Dkt Mwigulu Nchemba akiwasilisha bungeni mapendekezo ya mwongozo wa maandalizi ya mpango na bajeti ya Serikali kwa mwaka 2024/25, alisema Serikali inakadiria kutumia sh. trilioni 47.42 katika mwaka 2024/25.
Alisema shughuli za chaguzi za Serikali za Mitaa na uchaguzi mkuu mwaka 2025 zikizingatiwa.
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unatarajiwa kufanyika mwakani ukifuatiwa na uchaguzi mkuu mwaka 2025.
Kwa miswada hiyo kusomwa Bungeni mara ya kwanza maana yake ni kwamba Serikali ya Rais Samia, imetimiza ahadi yake ya kupelekwa miswada ya sheria Bungeni ili kurekebishwa.
Hatua hiyo itapunguza malalamiko ya kutotendeka kwa haki katika uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa, 2024 na Uchaguzi Mkuu, 2025.
Malalamiko hayo yamekuwa yakitolewa kwa nyakati tofauti na wanasiasa, lakini yalikuwa hayasikilizwa, hadi Rais Samia, alivyoamua kusikiliza kilio hicho na sasa nchi yetu imeanza safari mpya.
Baada ya uamuzi huo wa Serikali ya Samia, wadau wengi wa masuala ya siasa wanaisubiri kwa hamu, mabadiliko hayo wakiwa na matumaini miswada hiyo itajibu kiu ya muda mrefu ya kutaka kuwepo kwa mfumo unaotenda haki kwa kila Mtanzania wakati wa uchaguzi.
Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, anapongeza Serikali ya Rais Samia kwa kwa kupeleka miswada hiyo Bungeni, akisema tuna muda wa miezi mitatu ya kujadili miswada hiyo.
Kwa hiyo Zitto alitoa wito kwa wadau wa demokrasia, wanasiasa, wanaharakati na Watanzania kwa ujumla kushirikiana na Kamati ya Bunge ili kuboresha miswada hiyo.
Anasema huu ni muda wa kushirikisha Serikali, Bunge kuhakikisha tunafikia kwenye mabadiliko hayo.
“Kwa mara ya wanza tunaenda kuwa na Tume ya Uchaguzi inayotokana na mchakato, mambo hayo yanaweza kuhitaji mabadiliko katika baadhi ya vifungu vya Katiba.
Kwa hiyo tukileta mapendekezo ya mabadiliko ya vifungu hivyo, Serikali iendeleze usikivu kama ilivyofanya kwenye miswada hii,” alisema Zitto.
Mmoja wa wanasiasa ambaye hakupenda jina lake lichapishwe gazetini, alisema hatia hiyo inaonesha jinsi Rais Samia anavyoedesha nchi kidemokrasia kwa maana ya kusikiliza wadau.
“Nchi msingi wake ni watu, kama hakutakuwa na manung’uniko maana yake nchi yetu tutaipeleka kwenye mabadiliko na tutatoka na sheria nzuri,” alisema.
Mwenyekiti Taifa wa Chama cha ADC Alliance, Hamad Rashid, alimshukuru Rais Samia kwa utashi wake wa kisiasa kuweza kufikia hatua ya kupatikana kwa miswada hiyo.
Alisema kwa mara ya kwanza Tanzania inaelekea kupata fursa ya kuona Tume ya Huru ya Uchaguzi inayotoa fursa kwa wajumbe wake kupitia utaratibu angalau wa kuchujwa kabla ya kupelekwa kutangazwa.
Alisema hii ni hatua muhimu ambayo haikutegemewa na hata miaka ya nyuma haikuwepo, lakini kwa namna ambavyo Rais Samia amekuwa na utashi wa jambo hilo, ameweza kufanya jambo jema.
“Mimi niliyebahatika kuwepo katika awamu zote za Serikali na kwnye vyama vya siasa nimeshuhudia chaguzi mbalimbali kwenye mfumo wa chama kimoja au vyama vingi, lakini kwa hatua hii nimeona namna nzuri ambazo zimeanza kuchukuliwa kuhakikisha demokrasia ya siasa inapatikana,”alisema na kuongeza;
“Tanzania inapiga hatua kubwa katika suala la demokrasia ukizingatia suala zima la Katiba, usalama, amani na utulivu katika nchi yetu, pia nampongeza Rais Samia kwa kuunda kikosi kazi ambacho kimepokea mawazo mbalimbali na michango ya wadau na hatimaye kuyafanyia kazi.”
Kwa upande wake Mbunge wa Viti maalum, Neema Lungangilwa alimpongeza Rais Samia kwa kuunda Kamati ya Kufanya Tathimini ya Vyama vya Siasa nchini na kupokea mapendekezo, ambapo tayari matunda yake yameanza kuonekana.
Alisema Watanzania wanapaswa kutambua kuwa Serikali chini ya Rais Samia imefanyia kazi mapendekezo ya kikosi kazi kwa kiwango kikubwa, ikiwemo katika eneo la usawa wa kijinsia, kuwekwa kwa kifungu kipya ambacho kinasema kila chama cha siasa katika shughuli zake zote kinapaswa kuzingatia usawa wa kijinsia, ikiwemo ujumuishaji wa makundi maalum, vijana, wanawake na watu wenye uhitaji maalum.
Kwa upande wake Joseph Selasini alisema angependa sheria itamke Tume ya Uchaguzi iwe huru.
“Na sio tume ya uchaguzi pekee, Sheria itambue kabisa kuwa ni tume huru na kwa sababu hiyo wajumbe wa tume hiyo watambulike kisheria na sheria iwalinde nje na ndani ya tume,”alisema.
Kuhusu viti maalum, alisema visiwe vya akina mama fulani ambao wamekuwa wakijimilikisha nafasi hizo kama mali zao, kwani mara nyingi kunakuwa na upendeleo mwingi.
“Lazma viti maalum vijulikane, wanapoingia wanakaa muda gani, kwani inaonekana watu hao hawafanyi kazi majimboni,
hivyo ni vema kuweka utaratibu wa akinamama hao kuwa wanachaguliwa kwa mtindo fulani,” alisema Selasini na kuongeza;
“Nampongeza Rais Samia kwa hatua hii amedhubutu, tusilalamike tu, lazima tuunge mkono na kutoa mapendekezo ya kusaidia tusione upande hasi tu, hiki kitu kimeletwa ili kuleta manufaa
kwa nchi yetu, hivyo ni vema kuchangia mawazo yetu,”alisema.
Naye Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Haji Duni alisema, kwa sasa kuna mazuri yaliyorekebishwa katika sheria.
“Nampongeza Rais Samia kuchukua hatua ingawa tuna safari ndefu kwenye sheria ya vyama vingi, pia tuhakikishe kuna udhibiti fedha za uchaguzi,”alisema na kuongeza;
“Tatizo lisilokuwa wazi juu ya sheria ya Polisi ndio tulitegemea sheria ifanyiwa marekebisho, wanachama na wanasiana kufanya mikutano yao kwa amani kwani Jeshi la Polisi linatumia sheria ya Mwaka 1973 ambayo ilikuwa inatazamia chama kimoja”alisema.
Pia alisema kwa ujumla mambo sio mabaya katika sheria hiyo, lakini linapokuja suala la kushinda, Rais ashinde kwa asilimia zaidi ya 50 na sio 38 hakuna sababu ya kuogopa.
More Stories
Mussa: Natamani kuendelea na masomo,nikipata shule ya bweni
Tanzania inavyowahitaji viongozi wanawake aina ya Mwakagenda kuharakisha maendeleo
SCF inavyotambua jitihada za RaisSamia mapambano dhidi ya saratani