Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya
JESHI la Polisi Mkoani Mbeya linawashikilia watu watano wa familia moja akiwemo mke wa marehemu kwa tuhuma za kumuua Ally Mazinge (66) mkazi wa Ubaruku wilayani Mbarali, Mkoa wa Mbeya.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei amesema tukio hilo limetokea Juni 26 mwaka huu majira ya saa sita na dakika 40 usiku katika Kitongoji cha Mbuyuni, Kijiji cha Mpakani, Kata ya Ubaruku.
Kamanda Matei amesema watuhumiwa hao walimvizia marehemu akiwa amelala kisha kumkata kwa panga sehemu ya shavu la kulia pamoja na kidevuni.
Matei amewataja watuhumiwa kuwa ni Chausiku Mahmod (50) mke wa marehemu, Idrisa Ally (20), Hawa Ally (20), Salima Ally (19) pamoja na Jumanne Ally(30).
Akieleza zaidi Kamanda Matei amesema chanzo cha tukio hilo kuwa ni tamaa ya mali kwani mke na watoto wa marehemu walipanga kuuza eneo wanaloishi ambalo mnunuzi alipanga kujenga kituo cha mafuta (Filling Station)
Amesema wakati wa uhai wake marehemu aliwakatalia kuuza eneo hilo kwa sababu sehemu ya eneo hilo kuna nyumba ambayo wanaishi, hivyo marehemu alionekana ni kikwazo katika mipango yao.
Upelelezi wa shauri hilo unaendelea na mara baada ya kukamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani.
Hata hivyo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi ,Ulrich Matei ameitaka jamii kuacha tamaa ya mali ambayo kwa kiasi kikubwa husababisha mauaji ya watu wasio kuwa na hatia na badala yake watafute mali kwa kufanya kazi itakayowasaidia kujipatia kipato halali.
Amesema Jeshi la Polisi halitasita kumchukulia hatua za kisheria mtu, watu au kikundi cha watu kitakachojihusisha na uhalifu wa aina yoyote.
More Stories
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi
Mbunge Ndingo:CCM imejidhatiti kuwaletea maendeleo wananchi
SACP Katabazi: Elimu ya usafirishaji wa kemikali bado ni muhimu kwa watanzania