Dkt. Bashiru atangaza viti vyote vipo wazi, ruksa watangaza nia kuanza leo, Magufuli arejesha fomu, aonya tusibomoane, ataja sababu ya kujitosa
Na Joyce Kasiki, TimesMajira, Dodoma
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza rasmi nafasi za ubunge, udiwani na uwakilishi kwa upande wa Zanzibar kuwa wazi kuanzia leo, hivyo kila mwanachama ni ruksa kupita kwa wakurugenzi wa uchaguzi wa chama hicho kuulizia taratibu za kupata fomu na kutangaza nia, lakini sio kuanza kufanya kampeni.
Kuanza kwa mchakato huo kulitangazwa jijini Dodoma jana na Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Bashiru Ally, wakati akizungumza na wana-CCM mara baada ya kupokea fomu za muomba urais kupitia CCM, Rais John Magufuli.
“Kuanzia kesho Julai mosi (leo) nafasi za ubunge, udiwani na uwakilishi zipo wazi, hivyo kila mmoja anayetaka kuwania nafasi hizo apite kwenye ofisi ya mkurugenzi kuulizia utaratibu, kuhusu fomu zinapatikanaje, lakini sio kufanya kampeni,” amesema Dkt. Bashiru.
Amesema kipenge cha kuchukua fomu kwa wagombea nafasi hizo kitaanza Julai 14 na kufika mwisho Julai 17, hivyo kuanzia sasa ni muda wa kujitambulisha tambulisha, lakini atakayekiuka kanuni Mzee Mangula (Naibu Mwenyekiti CCM Bara, Philip Mangula) yupo, kwani wanataka ushindani wenye utulivu na wa kistaarabu.
Dkt. Bashiru amesema wale waliokuwa wakishika nafasi hizo za ubunge, udiwani na uwakishi wajue nafasi zao zipo wazi kuanzia kesho (leo), lakini hawaruhusiwi kwa mujibu wa kanuni kufanya kampeni.
Fomu za Magufuli
Akizungumza fomu za kutafuta wadhamini muomba urais kupitia CCM, Rais John Magufuli, Dkt. Bashiru amesema amekamilisha utaratibu na fomu hizo tayari amezirejesha.
Alifafanua kwamba katika mikoa yote, Rais Magufuli alipata wadhamini 1,023,911 na kwamba baada ya zoezi hilo Mkutano Mkuu wa CCM utakutana katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma ili kumpigia kura za kumpitisha awe mgombea na baadaye Halmashauri Kuu ya CCM itakutana jijini Dodoma kupitisha jina la mgombea urais.
Tusibomoane
Rais Magufuli amesema kuanzia leo ni ruksa kwa wana-CCM kuanza kupita pita katika maeneo mbalimbali kujionesha maana hiyo ndiyo demokrasia waliojiwekea ndani ya Chama.
“Kwa wale wana CCM ambao watajitokeza kuwania nafasi mbalimbali, kuanzia leo ni ruksa kupita pita katika maeneo, lakini kipindi cha kampeni kisitumike kama kipindi cha kubomoa chama chetu.
Tusianze kubomoana wenyewe kwa wenyewe, tukawe wavumivu, kule Zanzibar kuna wagombea urais 33, lakini atakayechaguliwa ni mmoja tu na Mungu wetu wa mbinguni anamfahamu,” amesema Rais Magufuli na kuongeza;
“Sisi (mwaka 2015) tulikuwa 42, kwa hiyo niwaombe sana wagombea CCM upande wa Zanzibar wawe waangalifu katika kunadi sera zao tusiumizane, tukifanya hivyo tunawapa nafasi washindani wetu.”
Rais Magufuli amesema kazi sio urais tu, kwani kazi zipo. “Tusiumizane, ninaambiwa hata kwenye majimbo mbalimbali mengine wapo 25, mtarogana bure, atakayepitishwa Mungu anamjua.
Tusiumizane, tuvumiliane, tuheshimiane, tupendane na baada ya uchaguzi huyo atakayekuwa amechaguliwa tumbebe. Nafasi zipo nyingi na kwa maana nyingine tukifanikiwa kushinda kutakuwa na nafasi Zanzibar, kutakuwa na nafasi upande huu (bara) tusiumizane.”
Amesema anawaombea na kuwatia moyo wanaotaka kugombea na aliviomba vyama vingine visiwasahau akina mama na vijana na akina baba wazee na akina mama wazee, kwa sababu busara zao zinahitajika.
Awashukuru waliomdhamini
Akizungumza na wana CCM mara baada ya kurejesha fomu zake, Rais Magufuli amesema; “Nimerudisha fomu kwa kutambua kuwa mimi bado ni mtu wenu na bado nataka kuendelea kutumika.
Nawashukuru wote walionidhamini Zanzibar na Bara na kwangu hilo ni deni kubwa kwa Watanzania, deni kubwa kwa wana CCM wa mikoa yote walioamua kuja wenyewe kunidhamini ili asisumbuke kuzunguka kila mahali kutafuta wadhamini.”
Amesema watu wengi walitaka kumdhamini, lakini fomu alizopewa hazikutosha na amewaomba dhamana zao waziweke kwenye kura zao iwapo atapitishwa na mikutano inayohusika ili awe mgombea wa urais.
Amesema leo sio siku ya hotuba, hajapitishwa na chama na wakubwa wa mkutano mkuu ndio wa kuamua.
Asema bado tuna changamoto
Rais Magufuli, amesema pamoja na kazi kubwa iliyofanyika katika kipindi cha miaka mitano iliyoisha, lakini bado kuna changamoto nyingi ndani ya taifa letu.
Amesema kwa kipindi cha miaka mitano wakati wakitekeleza ilani, walijiwekea malengo na mipango mingi imetekelezwa. “Wakati tunatekeleza mipango mingi, tumeona kuna mipango mingi inatakiwa kutekelezwa na mingine inatakiwa kuendelea kutekelezwa kama mradi wa Ujenzi wa Treni ya Kisasa (SGR) ambayo inatakiwa kufika Mwanza na Kigoma.
Tuna mpango wa mradi mkubwa wa Umeme Nyerere,” amesema na kuongeza kwamba kazi ya kusambaza umeme katika vijiji vyote nchini unaendelea, ambapo hadi sasa umefika katika vijiji 9,014 na bado vijiji 3,000 ili kila kijiji cha Tanzania kiwe na umeme.
Amesema hata Dodoma wana mpango wa kujenga barabara ya njia nne ya kilometa 110 kwa gharama za sh. bilioni 600 na tayari fedha zipo, ujenzi wa mradi wa kiwanja cha ndege Msaloto kwa sh. bilioni 500, kununua meli itakayotoa huduma kuanzia Kalema na Kalemii.
“Maana yake mizigo inayoenda nchi ya DRC (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo) haitapitia nchi nyingine. Kalemii ipo jimbo kubwa lenye watu zaidi ya milioni 50 na ndiko kunakochimbwa dhahabu na kwa mtu anayepamba uchumi mkubwa wa hii nchi lazima tufungue hii njia,” amesema Rais Magufuli na kuongeza;
“Tumefanya miradi mingi na katika kuitekeleza siamini kama itakamilika kama wao walioianza watashindwa,” amesema Rais Magufuli.
Amesema katika kipindi cha miaka mitano kwa kusaidiwa na wana CCM ameona achukua fomu azirudishe jana halafu asubiri maamuzi mengine ya chama chake.
Amesema anafahamu changamoto za uongozi ni kazi ngumu sana. Alitoa mfano kwamba juzi alipita Kilosa, kuna changamoto nyingine, amefika Dodoma saa 2 usiku amelala masaa matatu.
Mambo yanakwenda vizuri
Rais Magufuli aliwahakikisha wananchi kuwa mambo yanakwenda vizuri, vituna kwamba vitu vilivyokuwa vimeshindikana vimefanyika na kutolea mfano kuwa treni kwa sasa inakwenda hadi Arusha, Kilimanjaro, wamepanua bandari zote, wamenunua meli kila mahali.
“Lengo kubwa ni kuijenga nchi yetu, nchi hii ni tajiri, kilichokuwa kinatusumbua ni ufisadi na wizi, kikipatikane hiki kinakwenda kwingine,”amesema.
Amesema hata wale waliozoe kutunyonya wanashangaa. “Hata Tanzanite imepatikana kwa sababu tumezungusha ukuta. Tumetengeneza mazingira ya kulinda rasilimali ili masikini kama akina Laizer waweze kunufaika,” amesema.
Amesema wamehamia Dodoma wameishazungusha Ikulu ukuta kilometa 27, wanataka kila Mtanzania wa kila eneo afaidike na matunda tuliyopewa na Mwenye Mungu.
“Mipango mikubwa ya kumuenzi mwalimu Nyerere ndiyo imemfanya achukue fomu,”amesema. Amesema wanataka kila mmoja anufaike, ndiyo maana waliachia vijiji 920 vilivyokuwa kwenye hifadhi kwa lengo ni kuona kila mmoja anafaidika na kipande cha ardhi kilichopo ndani ya nchi yetu.
More Stories
Tanga kutumia vituo 5405,kupiga kura leo
NMB yatoa msaada wa vifaa Mufindi
Viongozi wa dini Katavi waomba wananchi kujitokeza kupiga kura