October 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (sekta ya ujenzi), Arch. Elius Mwakalinga (kulia) akiwa katika mkutano na wakandarasi wa Umoja-Kilosa JV wanaojenga barabara ya Rudewa-Kilosa KM 24 mkoani Morogoro.

Mkandarasi apewa siku saba ujenzi wa barabara

Na Penina Malundo, TimesMajira Online

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (sekta ya ujenzi), Mhandisi Elius Mwakalinga amempa siku saba Mkandarasi anayejenga Barabara ya Rudewa-Kilosa, kuja na mpango mkakati wa kuhakikisha barabara hiyo inakamilika kwa wakati.

Ametoa agizo hilo juzi  baada ya agizo la Rais John Magufuli kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 24.

Juzi Rais Magufuli akiwa katika hafla ya kuweka jiwe la msingi ujenzi wa barabara hiyo, licha ya kutoridhishwa na kasi ya ujenzi huo, ametoa muda wa mwezi mmoja kwa mkandarasi huyo kufanya mabadiliko chanya endapo anataka kuendelea na ujenzi wa mradi huo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (sekta ya ujenzi), Arch. Elius Mwakalinga (kulia) akijadiliana jambo na Waziri wa Nishati Mhe. Dk. Medard Kalemani mara baada ya hafla ya uzinduzi wa ujenzi wa barabara ya Rudewa-Kilosa KM 24 mkoani Morogoro kwa kiwango cha lami.

Akizungumza katika kikao cha dharura kati ya Katibu Mkuu Mwakalinga, Wakala wa Barabara nchini (TANROADs) na Mkandarasi Umoja-Kilosa JV, Mhandisi Mwakalinga alimtaka mkandarasi huyo kuhakikisha barabara hiyo inakamilika kwa haraka na kwa ubora uliokusudiwa ili kuiwezesha Serikali kuwa na imani na wakandarasi wazawa.

“Hakikisheni mnajenga imani kwa Serikali yenu ili iwaamini na hivyo muweze kupata miradi mingi ya ujenzi hapa nchini na hivyo kukuza uchumi wa nchi na ajira kwa wazalendo,” amesema mhandisi  Mwakalinga

Amesema nia ya Serikali ni kuwawezesha wakandarasi wazawa kuwa na uwezo na mtaji na hivyo kujenga miradi mingi ya ujenzi ili fedha nyingi inayolipwa kwa wakandarasi kubaki nchini na kuhuisha uchumi na kukuza ajira za Watanzania.

“Kuungana, uaminifu, uzalendo na kuchapakazi kwa bidii, kutaiwezesha Serikali kutoa miradi mingi ya ujenzi kwa wakandarasi wazawa na hivyo kuwajengea uwezo wa kimtaji, utaalamu na uzoefu na kuongeza ajira kwa Watanzania,” amesema Mwakalinga

Muonekano wa sehemu ya barabara ya Rudewa-Kilosa KM 24 mkoani Morogoro ambayo inayoendelea na ujenzi.

Barabara ya Rudewa-Kilosa ni sehemu ya barabara ya Dumila-Kilosa-Mikumi yenye urefu wa Km 142, inayotarajiwa kukamilika Januari mwakani itakapokamilika, barabara hiyo itaunganisha mikoa ya Tanga, Morogoro na Iringa bila kupita mbuga ya wanyama ya Mikumi na hivyo kupunguza ajali katika mbuga hiyo .