Na Jackline Martin,TimesmajiraOnline, Zambia
OKTOBA 23, mwaka huu Rais Samia Suluhu Hassan, alianza ziara ya siku tatu nchini Zambia kufuatia mwaliko wa kitaifa kutoka kwa Rais wa nchi hiyo, Hakainde Hichilema.
Ziara hiyo ambayo lengo lake lilikuwa ni kudumisha uhusiano katika maeneo ya kimkakati ya sekta za uchumi na uwekezaji hususan kwenye uchukuzi, nishati na biashara ilihitimisha Oktoba 25, mwaka huu kwa kuhutubia Bunge la nchi hiyo.
Ziara hiyo ya Rais Samia imekuwa ni mwendelezo wa ziara zake anazozifanya nje ya nchi na zile zinazofanywa na viongozi wa mataifa mbalimbali hapa nchini, ambazo zimekuwa na manufaa makubwa kwa Taifa letu.
Kama zilivyo ziara zingine ambazo zimefanywa na Rais Samia nchi mbalimbali, zira ya Zambia nayo imezidi kfungua fursa kwa nchi yetu.
Katika makala haya, Mwandishi Wetu ambaye alikuwa kwenye msafara wa Rais Samia, nchini Zambia anaeleza baadhi ya mambo ambayo aliyafanya kwenye ziara hiyo kwa manufaa ya nchi yetu.
***Akaribisha wafanyabiashara
Katika ziara hiyo, Rais Samia alisema; “Tumeweka juhudi katika kuiboresha bandari ya Dar es Salaam kuhakikisha inakuwa na ufanisi katika shughuli zake, niziombe jumuiya za wafanyabiashara ninazokwenda kukutana nazo baada ya mikutano huu, zione fursa hii ya pekee,” amesema.
Hata hivyo, aliihakikishia nchi hiyo kuwa, Tanzania itaendelea kuwa mshirika wake kama ilivyowahi kuwa wakati wa mapambano ya uhuru wa mataifa hayo mawili.
Kuhusu sherehe hizo, amesema zitakumbusha juhudi za waasisi wa mataifa ya Afrika walivyojitoa mhanga kuhakikisha uhuru unapatikana.
Naye Rais Hichilema anasema amani na ushirikiano baina ya Tanzania na Zambia ni jukumu la wakuu wa nchi hizo na wananchi wake.
“Hili ni jukumu lisiloepukika, tuna wajibu wa kuhakikisha tunadumisha amani na mahusiano yetu kwa maslahi ya watu wote,” amesema.
Si kwa nchi hizo pekee, anasema hilo linapaswa kusimamamiwa kuhakikisha amani na uhusiano unakuwepo hata katika ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Rais Hichilema ametoa wito kwa viongozi wa nchi mbalimbali duniani kudumisha amani na umoja na kuepuka machafuko, akirejea kile kinachoendelea katika taifa la Israel na Palestina.
***Utekelezaji uondoaji vikwazo vya kibiashara
Akieleza hatua zinazoendelea kufanyika katika kuweka mazingira bora Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt Ashatu Kijaji, anasema tangu Agosti mwaka jana baada ya Rais Hichilema kutembelea Tanzania, mawaziri wa kisekta wameshakutana mara kadhaa na wameondoa baadhi ya vikwazo visivyo vya kikodi.
“Kati ya vikwazo 24 tulivyovianisha Serikali zote mbili tayari tumeshaviondoa nane na vilivyosalia tumekubaliana hadi kufikia Desemba 31 mwaka huu tuwe tumevimaliza vyote na vinavyoendelea kuibuka tutavishughulikia hatua kwa hatua.
Mimi na waziri mwenzangu wa Biashara upande wa Zambia, tuna vikao kwa njia ya mtandao kila wiki na mara moja kwa mwezi tunakutana katika eneo lenye changamoto iwe ni mpakani au kwenye miji mikubwa ambapo biashara zinafanyika iwe kuanzia au kuishia,” anasema Dkt. Ashatu.
**** Kusainiwa mikataba
Mbali na kushiriku kongamano la wafanyabiashara, kupitia ziara hiyo ya kitaifa ya siku tatu ya Rais Samia, nchini Zambia yeye na mwenyeji wake walishuhudiwa kusainiwa kwa hati sita za ushirikiano na mikataba miwili inayolenga kuboresha uwekezaji na biashara baina ya mataifa hayo mawili.
Wakati wa kusainiwa kwa mikataba hiyo Tanzania iliwakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba, huku Zambia ikiwakilishwa na Waziri wa Mambo ya nje Stanley Kakubo.
Hati za makubaliano zilizosainiwa ni ushirikiano wa nchi hizo kuhusu Mradi wa Usafirishaji Gesi Asilia kutoka Tanzania kwenda Zambia na hati ya makubaliano ya Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania na Wakala wa Maendeleo Zambia.
Mikataba mingine ni ya ushirikiano kati ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Wakala wa Maendeleo Zambia, pamoja na hati ya Makubaliano ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia katika Sayansi, Teknolojia na Ubunifu.
Aidha, kumesainiwa Mkataba wa Utekelezaji kati ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa la Tanzania na Jeshi la Ulinzi la Zambia kuhusu programu ya kubadilishana wanafunzi wa Kozi ya Ukamanda na Unadhimu.
Viongozi hao pia walishuhudiwa kusainiwa Mkataba wa Utekelezaji kati ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jeshi la Ulinzi la Zambia kuhusu programu ya kubadilishana Wakufunzi wa Kozi ya Ukamanda na Unadhimu.
Akizungumza baada ya kushuhudia utiaji saini, Rais Hichilema anasisitiza Serikali yake itafanya kila linalowezekana kuhakikisha makubaliano hayo hayaishii kwenye makaratasi.
“Tumeridhishwa na vitu tulivyovifanya siku zilizopita na tuko tayari kusimamia makubaliano tuliyosaini tunataka yaendelee kuishi.
Hatutaki makubaliano haya yaishie kwenye makaratasi ni lazima yatimizwe kwa lengo la kukuza uchumi wa mataifa yetu, kutengeneza ajira,” alisema na kuongeza;
“Uwekezaji kwenye elimu utatokana na haya makubalinao. Tukifanikiwa kuiboresha reli ya Tazara ambayo ni njia bora nafuu zaidi ya usafirishaji, kupanua bomba la Tazama, kushirikishana kwenye sekta ya madini tutafanikiwa kukuza uchumi wa nchi zetu, tunataka makubaliano haya yalete tija itaakayosaidia kuendeleza sekta nyingine ikiwemo elimu.”
Kwa upande wake Rais Samia alisema kupitia ziara hiyo, Tanzania na Zambia zimepata njia ya kukabiliana na changamoto mbalimbali ambazo utatuzi wake utasaidia kukuza biashara na ushirikiano wa kiuchumi.
“Tumekubaliana Serikali zetu zitaongeza ushirikiano kwa kuwa tumepata utatuzi wa changamoto kadhaa zilizokuwepo hasa katika eneo la biashara, matumaini yetu ni kwamba makubaliano mengine mengi yatasianiwa kwa kuwa tayari tumeshatoa maelekezo kwa watendaji wa Serikali wanafanyia kazi maeneo yaliyobaki,” anasema Rais Samia.
****Zawadi Samia kwa wananchi wa Zambia
Rais Samia Suluhu Hassan ametoa eneo la hekta 20 katika Bandari Kavu ya Kwala iliyopo Mkoa wa Pwani kama kituo cha usafirishaji kwa ajili ya Zambia.
Rais Samia ametoa zawadi hiyo Oktoba 24, 2023 alipohutubia katika sherehe za miaka 59 ya uhuru wa Zambia, zilizofanyika nchini humo.
Anasema uamuzi huo utasaidia kupunguza gharama za biashara katika taifa hilo na utakuza biashara kati ya nchi hizo.
Anasema hiyo ni fursa kwa Zambia kuhifadhi mizigo kwa muda mrefu na itapunguza gharama ya kufanya biashara, lakini itaimarisha biashara kati ya nchi zetu na hii ndiyo zawadi ya Tanzania wakati wanasherehekea uhuru wao.
Anasema nchi hizo mbili, zitaendelea kuweka mazingira mazuri kuhakikisha kunakuwa na usafiri na usafirishaji rahisi wa watu na bidhaa kutoka taifa moja kwenda lingine.
***Siri ya zawadi hiyo
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji anasema hatua hiyo inalenga kuongeza wigo wa nchi ya Zambia kuitumia Bandari ya Dar es Salaama kwa kuwa wataondokana na gharama za kuhifadhi mizigo na badala yake itahifadhiwa kwenye bandari kavu yao.
“Katika mengi ambayo tumewaletea wenzetu wa Zambia ni taarifa kuhusu maboresho tuliyofanya kwenye bandari yetu kwa lengo la kuongeza ufanisi, tunafahamu kiwango kikubwa cha mizigo inayoingia Zambia inapita kwenye bandari ya Dar es Salaam.
Kuwapatia eneo la kuhifadhi mizigo yao ni wazi kuwa itawapunguzia gharama na huduma za bandari yetu zitakuwa nafuu zaidi kwao,” anasema Dkt. Ashatu.
***Ahutubia Bunge
Aidha, katika ziara hiyo Rais Samia amesema Serikali inatarajia kuongeza siku za usafiri bila viza kwa wananchi wa Zambia wanaoingia nchini kutoka siku 90 za sasa hadi 190.
Kwa mujibu wa Rais Samia Utekelezaji wa hilo, utatoa uhuru wa usafiri kwa Wazambia kuingia nchini na kukaa kwa siku 190 bila kulazimika kununua viza.
Mpango huo ulitangazwa na Rais Samia alipolihutubia Bunge la Zambia, ikiwa ni siku yake ya mwisho yake.
Anasema uamuzi huo tarajiwa unalenga kurahisisha usafiri na usafirishaji wa watu kati ya nchi hizo mbili na hatimaye kufungua milango ya biashara.
“Ninayo furaha ya kulitaarifu Bunge hili, Serikali ya Tanzania inajiandaa kuwezesha usafiri wa watu bila visa kwa kuongeza muda wa watu kuingia nchini bila viza kutoka siku 90 hadi 190,” anasema.
Anasema Tanzania ipo tayari kusaidia ujenzi wa mpaka wa Zombe ili kurahisisha usafiri wa watu na usafirishaji wa bidhaa kati ya mataifa hayo.
Hatua hiyo inalenga kuimarisha mahusiano baina ya nchi hizo na watu wake kwa ujumla. Anasema ni muhimu wabunge wa mataifa hayo ambao ndiyo wawakilishi wa wananchi, kuhakikisha wanapitisha mipango na bajeti zinazowasilishwa na Serikali kwa manufaa ya umma.
“Iwapo wabunge hawatashawishika au wakiamua kufanya siasa dhidi ya mipango hii, wataathiri maendeleo tuliyofikia, Watanzania na Wazambia,” anasema
Kwa mujibu wa Rais Samia, mrejesho unaopatikana kutoka kwa watu mbalimbali ni kwamba mifumo ya kisheria baina ya nchi hizo itakuwa rafiki kwa biashara iwapo mataifa hayo hayataingiza siasa kwenye mipango yao.
Anasema Serikali zinapowasilisha mapendekezo ya kuondoa vikwazo vya kikodi na ushuru, mabunge yanapaswa kujua msaada wao unahitajika.
Anasema mipango ijayo ya Serikali ni kuhakikisha inajengwa miradi mipya ya miundombinu kwa ushirikiano.
Kwa mujibu wa Rais Samia, biashara ya Tanzania na Zambia itakuwa kutokana na juhudi mbalimbali ikiwemo ya kuboreshwa kwa bandari ya Dar es Salaam.
***Uhusiano wa nchi hizo
Rais Samia anasema uhusiano uliopo kati ya mataifa hayo ni historia iliyobebwa na waasisi wake, Mwalimu Julius Nyerere wa Tanzania na Kenneth Kaunda wa Zambia.
“Kuna muendelezo wa uhusiano kati ya nchi hizi mbili kwa kuwa yapo mambo yaliyobaki kama alama, likiwemo bomba la mafuta la Tazama na reli ya Tazara,” anasema.
Hata hivyo, ameeleza Serikali hizo mbili, zinafanya juhudi kupunguza changamoto mbalimbali zinazoikumba reli ya Tazara ili kurahisisha usafirishaji.
****Kumaliza vikwazo vya kibiashara
Aidha, katika ziara hiyo Rais Samia na mwenyeji wake, Hichilema walishiriki kongamano la wafanyabiashara wa Tanzania na Zambia.
Kongamani hilo limefungua milango ya kuongeza biashara baina ya mataifa hayo, kwa nchi zote mbili kukubaliana kuondoa vikwazo na urasimu ili kukuza biashara na uwekezaji.
Makubaliano hayo ni pamoja na kuondoa urasimu, kuweka mazingira rahisi ya ufanyaji biashara, kuitumia vyema miundombinu inayounganisha nchi hizo na kuruhusu mwingiliano wa watu.
Kongamano lililowakutanisha wafanyabiashara wa Tanzania na Zambia na kwa pamoja wakakubaliana kuimarisha ushirikiano wa kibiashara baina ya mataifa hayo.
Makubaliano hayo yalitiliwa mkazo na Samia Hichilema walipotuhubia kongamano hilo.
Akizungumzia hilo, Rais Hichilema anasema hakuna sababu ya mataifa hayo kuweka urasimu na vikwazo katika biashara na uwekezaji kwa kuwa maendeleo yanahitaji kwa kiasi kikubwa ushiriki wa sekta binafsi.
“Nimetoka kwenye sekta binafsi nafahamu hizi nchi zina vikwazo vingi kwenye ufanyaji biashara ndiyo maana nasema kwa nafasi niliyonayo sasa tuna kila sababu ya kuviondoa hivyo vikwazo, hilo hatuwezi kufanya peke yetu hivyo tumekubaliana na Rais Samia kushirikiana kuviondoa hasa katika eneo la mpakani kwa kuwa sisi ni ndugu hatupaswi kutengenishwa na mikapa,” anasema.
Anasema Serikali katika nchi zote mbili zinapaswa kuondoa vikwazo vinavyoweza kukwamisha biashara, huku akitaka sekta binafsi kuwa sehemu ya jitihada za kukuza uchumi na siyo kuishia kulaumu.
“Sekta binafsi ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi, sasa kama kuna changamoto na hamshiriki katika kuhakikisha zinapatiwa ufumbuzi na kuishia kuilaumu Serikali haiwezi kuwa na tija,” anasema na kuongeza;
“Tunataka ushirikiano wetu kwenye uchumi na biashara uzidi kuimarika maradufu kama ilivuo katika uhusiano wetu, hili ndilo linasababisha tunaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha tunaweka mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji,” amesema Hichilema.”
Anasema ni muhimu kwa Tanzania na Zambia kuwekeza katika maboresho ya reli ya ushirikiano ya Tazara kwa kuwa ina umuhimu mkubwa katika kukuza biashara baina ya nchi hizo ikitegemewa zaidi kwenye usafirishaji wa bidhaa.
Naye Rais Samia, anasema Serikali yake inafanya kila linalowezekana kusukuma uchumi na hilo linafanyika kwa kuweka mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji.
Rais Samia alitumia fursa hiyo kuinadi Tanzania na kuwakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji wa Zambia kuwekeza nchini humo kwa kuwa Serikali imeweka mazingira wezeshi kwa ajili hiyo.
“Serikali ninayoingoza tuna maono ya kutengeneza uchumi imara na shirikishi kwa Watanzania na wote watakaotaka kuja kuwekeza Tanzania.
Ushirikiano huu tunaozidi kuuimarisha kati yetu na Zambia tunaamini utakuwa kichochea katika kusukuma maendeleo ya kiuchumi kwa mataifa yote mawili,” anasema Rais Samia.
More Stories
Mussa: Natamani kuendelea na masomo,nikipata shule ya bweni
Tanzania inavyowahitaji viongozi wanawake aina ya Mwakagenda kuharakisha maendeleo
SCF inavyotambua jitihada za RaisSamia mapambano dhidi ya saratani