November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NECTA yatangaza watahiniwa mtihani wa darasa la 4

Na Mwandishi wetu Timesmajira Online

BARAZA la Mitihani Tanzania (NECTA) limesema jumla ya wanafunzi 1,692,802 wamesajiliwa kufanya upimaji wa kitaifa wa darasa la nne Octoba 25 hadi 26 huku 759,573 wakiwa wa kidato cha pili wakitarajiwa kufanya Oktoba 30, hadi Novemba 09, mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Octoba 24,mwaka huu Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania(NECTA), Dkt.Said Mohamed amesema kwa darasa la nne jumla ya shule za msingi 19,284 wanatarajia kufanya mtihani huo kuanzia kesho na kesho kutwa.

Ambapo kati ya idadi hiyo ya wanafunzi waliosajiliwa kufanya mtihani huo wavulana ni 828,591 sawa na asilimia 48.95 na wasichana ni 864,211 sawa na asilimia 51.05.

“Kati ya wanafunzi hao, 1,605,379 sawa na asilimia 94.84 watafanya upimaji huo Kwa lugha ya Kiswahili na wanafunzi 87,423 sawa na asilimia 5.16 watafanya Kwa lugha ya kiingereza ambayo wamekuwa wakitumia kujifunza”amesema.

Amebainisha kuwa wanafunzi wenye mahitaji maalum wapo 6,402 kati yao 1,074 ni wenye uoni hafifu, 93 ni wasioona, 1,240 wenye ulemavu wa kusikia, 2,209 mtindio na 1,786 wenye ulemavu wa viungo vya mwili.

Kwa upande wa kidato cha pili Dkt Mohamed amesema kati ya wanafunzi 759,573 waliosajiliwa kufanya upimaji wa kitaifa wa kidato cha pili mwaka huu kutoka shule za sekondari 5,546, kati yao wavulana ni 353,807 sawa na asilimia 46.58 na wasichana ni 405,766 sawa na asilimia 53,42.

Amesema wanafunzi wenye mahitaji maalumu ni 1,382 kati yao683 ni wenye uoni hafifu, 82 ni wasioona, 290 ulemavu wa kusikia na 309 ulemavu wa viungo vya mwili na 18 ulemavu wa akili.

Katibu huyo amesema maandalizi ya upimaji kwa wanafunzi yamekamilika ikiwa ni pamoja na kusambazwa Kwa karatasi za upimaji na nyaraka zote muhimu zinazohusu upimaji katika halmashauri zote nchini.

Pia amesema upimaji huo kwa darasa la nne ni muhimu kwani unawezesha kujua kiwango cha wanafunzi katika kumudu stadi za juu za kusoma , kuandika na kuhesabu.

Amesema umuhimu wa upimaji kidato cha pili, hupima uwezo na uelewa wa wanafunzi katika yote waliyojifunza Kwa kipindi cha miaka miwili ya masomo yao ya sekondari, upimaji wa kidato cha nne.

Aidha alitoa wito kwa kamati za mitihani za mikoa na halmashauri zihakikishe kuwa usalama wa vituo vya mtihani unaimarishwa kwani vituo hivyo vinatumika kwa mujibu wa mwongozo uliotolewa na Baraza mtihani la Tanzania.

Vilevile aliwataka wasimamizi wote walioteuliwa kusimamia upimaji kufanya kazi yao ya usimamizi kwa umakini na uadilifu wa hali ya juu.

“Wasimamizi wanapaswa kuhakikisha kuwa, wanafanya kazi ya usimamizi kwa weledi na kwa kuzingatia kanuni za mitihani na miongozo waliyopewa ili kila mwanafunzi husika apate haki yake,”amesema.

Aidha amesema wasimamizi hao wanapaswa kuhakikisha wanafunzi wenye mahitaji maalumu wanafanya upimaji wao ipasavyo ili wapate haki yao msingi ambazo ni pamoja na kupata mitihani yenye maandishi ya nukta nudu Kwa wanafunzi wasioona na maandishi yaliyokuzwa kwa wanafunzi wenye uoni hafifu.

Kwa upande wa wanafunzi amesema Baraza la mitihani halitarajii kuona mwanafunzi yoyote kujiusisha na vitendo vya udanganyifu na kutoa taadhari kuwa yoyote atakayebainika kufanya udanganyifu matokeo yake yatafutwa kwa mujibu wa kanuni za mitihani.

“Baraza linaamini kuwa walimu wamewaandaa vizuri katika kipindi chote cha miaka miwili ya elimu ya sekondari na miaka minne ya elimu ya msingi,”amesema.

Katibu huyo Mtendaji amewataka wamiliki wa shule kutambua kuwa shule zao ni vituo maalum vya mtihani hivyo hawatakiwi kwa namna yoyote kuingilia majukumu ya wasimamizi wa mitihani katika kipindi chote cha ufanyikaji wa upimaji huo.