November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kijijini, Mbezi Beach eneo hatari jijini Dar

Biashara haramu dawa za kulevya, bangi, pombe haramu, ngono za nipe nikupe sehemu ya maisha ya kawaida, mazito yaanikwa

Na Waandishi Wetu, TimesMajira Online, Dar es Salaam

UKISTAAJABU ya Mussa Utayaona ya Firauni. Msemo huu unakamilisha picha halisi ya maisha ya wakazi wa eneo la Kijijini, lililopo katika Kata ya Kawe, Mtaa wa Mbezi Beach B, Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es salaam.

Ukifika katika eneo hilo dogo la Kijijini na ukashuhudia yanayoendelea unaweza kuamini kwamba wakazi hao wamehalalisha vitendo vya uvunjifu wa sheria kama sehemu ya maisha ya wakazi hao.

Katika eneo hilo, zinaishi kaya takribani 30-40, wakazi wa eneo hilo, wanaishi kwenye vibanda vya mabati ambavyo ndiyo makazi yao ya kudumu na familia zao kwa takriban miaka 30.

Makazi hayo huyatumia kama sehemu zao za kufanyia biashara haramu ambazo wao wamezihalalisha. Biashara zinazofanyika katika eneo hilo ni uuzaji wa dawa za kulevya, bangi, pombe haramu ya gongo, pombe za kienyeji na ngono ya nipe nikupe (kununua).

Kufuatia malalamiko ya wananchi kuhusiana na eneo hilo, gazeti hili lilipiga kambi kwenye eneo hilo kuchunguza yanayoendelea, ambapo wao hawaoni kama ni uvunjifu wa sheria, bali ni biashara halali.

Biashara ya ngono ya nipe nikupe katika eneo hilo inahusisha wanawake na wasichana wenye umri mdogo. Kinachofanyika ni maelewano na baada ya hapo, maisha yanaendelea.

Wakati wakazi wanaoishi eneo la Kijijini wakiwa wameridhika na maisha ya eneo hilo, baadhi ya wananchi waliokuwa na nyumba za kudumu jirani ya Kijijini wamezikimbia na kwenda kuishi kwingineko, kwani eneo hilo sio salama kwa malezi ya watoto na kwenye suala zima la maadili.

Mbali na hilo, pia eneo hilo limeonekana kuwa ni hatarishi kwa watoto chini ya miaka 18. Mbali na lugha chafu zinazozungumzwa na wanaofika kupata huduma, lakini kibaya zaidi watu hao wamesahau kwamba kuna vyombo vya dola.

Baada ya Gazeti Huru la Majira kufika eneo hilo, lilishuhudia na kujiridhisha kufanyika kwa biashara haramu na kujionea jinsi watoto wanaoishi jirani wanavyokabiliwa na tishio kubwa la kimaadili.

Mmoja wa wauza dawa za kulevya anayejulikana kwa jina la Mengi, au baba Bodo, anakiri kufanya biashara hizo, akidai ndiyo inayomuingizia kipato cha kuendesha familia yake.

“Mimi nipo hapa na mke wangu, tunaendesha maisha kupitia biashara hii na sio mimi tu, wakazi wengi wa eneo hili hii ndio biashara yao (kuuza dawa za kulevya),” alisema Bodo.

Naye mfanyabiashara wa nguo za mitumba (jina limehifadhiwa) ni mmoja wa wavutaji wa bangi katika eneo hilo, ambaye alidai kuwa mara nyingi huwa anafika hapo kwa ajili ya kuvuta na baadaye anaondoka.

Anakiri kuwa eneo hilo sio salama kukaa kwa muda mrefu, ndiyo maana anawahi kuondoka.

Mmoja wa wakazi wa eneo hilo aliyehamia Kijijini muda baada ya kukimbia jeshini kwa kosa la kumpiga mtoto mkoani Morogoro, anathibitisha kuwa eneo hilo sio salama.

Akizungumza kwa sharti la jina lake kutochapishwa gazetini, alisema eneo hilo huogopwa na watu wengi wakiwemo askari na wakati mwingine huishia pembezoni.

Kwa mujibu wa mtu huyo, kuna mmoja wa askari aliyewahi kufika eneo hilo kwa lengo la kukamata, wanaojihusisha na biashara hizo haramu, lakini aliuawa.

Mtu anapofika eneo hilo, anakaribishwa kwa kuelezwa huduma zinazopatikana.

“Karibu sana baba, kuwa na amani, kinywaji na hata ukitaka bangi sema utavuta kwa kujinafasi askari hawezi kuja hapa, ukihitaji chochote utakipata, tunauza bia na pombe za kienyeji.” Hivyo, ndivyo mteja anavyokaribishwa.

Binti mmoja maarufu katika eneo hilo (jina linahifadhiwa) alisema yeye alihamia hapo  muda mrefu na kufanya biashara zake, ikiwemo

kuuza dawa za kulevya.

Alisema, yeye alishafanya uhuni wa kila akiwa eneo hilo, na amekuwa muuzaji mzuri dawa za kulevya.

Kutokana na uzoefu alioupata hapo wa kuuza dawa za kulevya, sasa hivi anatamani ampate mtu wa kumbebesha dawa za kulevya kwenda nje ya nchi ili aweze kupata kipato kikubwa cha kumkwamua kimaisha.

“Mimi nimefanya uhuni hapa nilipo akili zangu Mungu mwenyewe ndiye anajua, nauza bangi na dawa zingine za kulevya na pia najua kumtengenezea mtu ili avute, lakini natamani siku moja mtu anishike mkono anibebeshe madawa, kwani siogopi hata kidogo kutokana na mambo mengi niliyoyafanya,”alisema.

Alisema, eneo hilo halina mwenyewe zaidi ya Serikali kwa hiyo watu walihamia hapo kwa kuambiana, lakini haparuhusiwi kujenga nyumba za kudumu.

Mbali na hivyo pia alisema, wao wamehamia hapo tangu enzi za Rais wa awamu ya tatu, Benjamini Mkapa hadi sasa bado wapo, kwa hiyo wanajulikana kuanzia ngazi ya shina mpaka taifa.

Alisema, wapo hapo wakifanya biashara zao, huku watoto wao wakisoma kwa kutegemea uuzaji wa dawa na pombe, huku wakijenga makwao pindi wanapopata kipato zaidi.

“Hili eneo huwezi kujenga kwa hiyo wengi wao hapa wamejenga makwao, lakini hapa ni eneo la kufanyia biashara na mambo mengine mengi,” alisema dada huyo.

Majirani wa eneo hilo, Mama Halima (siyo jina halisi) ni mkazi wa karibu eneo hilo la Kijijini, ambaye alidai kuwa eneo hilo limekuwa kero kwa watu wengi na hali inayohatarisha maisha ya watoto wao.

Alieleza kuwa wakazi hao ambao ni wavamizi wa eneo la barabara, wamekuwa kero kwa wakazi wa jirani kutokana na watoto wao kuharibiwa na biashara hizo haramu ambazo zimekuwa zikifanywa.

Alieleza kuwa, Halima ni binti yake mwenye umri wa miaka (28), ambaye inadaiwa tabia yake ilianza kubadilika baada ya kujihusisha na makundi ya wakazi wa eneo hilo, ambapo alijifunza kuvuta bangi na unywaji wa gongo.

Mama Halima alieleza kuwa, alianzisha uhusiano wa kimapenzi na kijana anayefahamika kwa jina moja la James, maarufu kama Chindo, ambaye pia ni muuzaji wa bangi.

“Kwa kweli tunaomba Serikali iangalie hili, sisi wakazi halali katika maeneo haya ndiyo tunaoumia, watoto wetu wanaharibikiwa sana kupitia huu mtaa wa Kijijini, kwani wakazi wa Mtaa huo wanajihusisha na biashara ya uuzaji bangi, dawa za kulevya na pombe za aina zote ikiwepo gongo,”alisema.

“Mwanangu Halima aliharibikia hapo, kwani alikuwa anaenda wakawa wanampa bangi na gongo, baadae akazaa mtoto wa kwanza na hao hao

wavuta bangi na mtoto ninamlea mimi.

Haikutosha wamemzalisha tena mtoto wa pili hivi sasa ana mwaka mmoja, huyo mtoto nimekataa yupo naye mwenyewe, lakini hawana pakukaa wanaishi huko huko Kijijini na huyo kijana muuza bangi, unga na gongo,” alisema Mama Halima kwa huzuni kubwa.

Aliongeza kuwa, mbali na vijana hao kumvutisha Halima bangi na kumfundisha gongo, lakini pia wamekuwa wakishirikiana kumuingilia kimwili bila idhini yake, ikiwemo kumlawiti, kutokana na kutojitambua baada ya kulewa.

Naye Mama Mwana (Siyo jina lake halisi), anakiri kuwepo kwa vitendo hivyo haramu katika eneo hilo na kudai kuwa, hali hiyo imesababisha yeye na familia yake kuhamia mkoa mwingine, baada ya kuona mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miaka 26 mwenye watoto watatu, kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya.

Mama Mwana alidai mazingira hayo yalisababisha mtoto wake huyo, kujiingiza katika unywaji wa pombe haramu ya gongo na kuanza kutumia dawa za kulevya.

“Kwa kweli mimi pia mtoto wangu ni muhanga ambapo imebidi tuhame ili kunusuru wajukuu zangu (watoto wa Ally-muathirika) wasiharibikiwe.

Mtoto wangu ameharibikiwa hapo kijijini na anasema kuwa wakati mwingine akikosa pesa ya kununua dawa hizo za kulevya, anaingiliwa

kinyume cha maumbile ili apatiwe,”alisema.

Mama Mwana anadai kuwa, mbali na vitendo vyote vinavyoendelea eneo la Kijijini, alitoa malalamiko yake Serikali ya Mtaa wa Mbezi Beach B, ambapo anadai kuwa, Mwenyekiti wa Mtaa (wakati huo), aliyefahamika kwa jina la Mama Fatma na Afisa Mtendaji wa Mtaa, aliyefahamika kama, Said Kikuu, hawakuonesha ushirikiano wowote.

Imeelezwa kuwa, chini ya uongozi huo, katika mkutano na wananchi, imedaiwa kuwa, wananchi hao walitoa malalamiko yao juu ya vitendo

vinavyoendelea, lakini viongozi hao waliwataka wananchi hao kila mmoja kusimamia mwenyewe familia yake na aliyeshindwa kumtaka kuhama.

“Kabla sijahama Mbezi Beach, tulikuwa na mkutano na viongozi wa Serikali katika Mtaa wetu, ambao kwa kipindi hicho, Mwenyekiti wa Mtaa alikuwa anafahamika kwa jina la Mama Fatma na Mtendaji wa Mtaa, Said Kikuu.

“Hawa walitujibu kuwa, wao siyo Mahakama wala Polisi, hivyo kila mmoja alinde mtoto wake na atakayeshindwa na kuona kero zimezidi basi ahame,” alisema Mama Mwana akinukuu majibu aliyopewa.

Pia alidai, uongozi wa Serikali ya Mtaa chini ya uongozi mpya, wananchi walitoa malalamiko yao kwa Mwenyekiti wa Mtaa wa Mbezi Beach B, Asha George na kuamuru wakazi hao kuvunjiwa vibanda vyao.

Ilielezwa kuwa, Diwani wa Kata ya Kawe, Rutta Rwakatare alizuia zoezi la uvunjwaji wa vibanda hivyo kwa kusimika bendera ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika eneo hili na kudai kuwa hao ni wapiga kura wake.

Aidha, kwa upande wake Jeremiah Nangwanda ( siyo jina halisi) aliiomba Serikali kupitia viongozi wake, kutembelea eneo hilo kujionea biashara hizo na kuzidhibiti.

Alisema, bila ya kufanya hivyo watoto wenye umri chini ya miaka 18 wapo hatarini.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mbezi Beach B, Asha George, alikiri kutambua uwepo wa wakazi wa eneo hilo, huku akidai kuwa amekuwa akipokea malalamiko mengi kutoka kwa baadhi ya wananchi na kwamba yamekuwa wakiyafanyia kazi.

“Ni kweli hao wakazi wa Kijijini nawatambua ni wakazi wangu, kuhusu kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi wengine yanayowahusu, kuna yaliyofanyiwa kazi na mengine bado tunaendelea kuyafanyia kazi,” alisema Aisha.

Diwani wa Kata ya Kawe, Mutta Rwakatare alipoulizwa kuhusiana na malalamiko ya wananchi, kuhusu eneo hilo, alijibu;

“Ni kweli nawafahamu wakazi hao wa eneo la Kijijini, lakini kuhusu ukazi wao wa eneo la barabara mimi sina majibu, kwani ambaye alitakiwa awaondoe hapo ni wenye nyumba za pembezoni yani wale wakazi halali siyo mimi.

Kuhusu biashara haramu zinazofanywa mimi sifahamu chochote na kama zipo, basi ningepokea taarifa kutoka Serikali ya Mtaa, lakini Serikali ya Mtaa haijanipa taarifa hiyo kwa maana yake kuna usalama”, alisema Rwakatare.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, ASP Mtatiro Kitinkwi,  alisema hafahamu lolote kuhusiana na tuhuma hizo.