January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi Tarime wapongeza mgodi mkakati wa uhifadhi mazingira

Na Raphael Okello,Timesmajira Online,Tarime

BAADHI ya wananchi wa vijiji vya Karende, Mrito, Nyangoto, Gibaso na Kwihacha wameupongeza mgodi wa Mara Mining kwa kuamua kuweka mkakati wa kuhifadhi mazingira kuzunguka mgodi huo.

Kauli hiyo imetolewa kwa nyakati tofauti wakati wa ziara ya kamati ya ulinzi na usalama ilipoitembelea mgodi huo.

Wamesema hatua hiyo itafanya maeneo yao kuwa na hali ya ukijani na kuiomba serikali kusisitiza migodi mingine kufuata mfano huo.

Akizungumza kwa niaba yao Mwenyekiti wa Kijiji cha Kerende Muniko Mgabe anaushukuru mgodi huo kwa dhamira yake ya utunzaji wa mazingira pamoja na kutoa ajira kwa vijana wa eneo hilo huku akisisitiza kuwa suala ni muhimu kwa kila mgodi.

Amesema kutokana na changamoto ya uharibifu wa mazingira unaosababishwa na shughuli za wanadamu katika maeneo ya mgodi utunzaji wa mazingira ni jambo la muhimu.

Mwenyekiti amefafanua kuwa hapa duniani kunahitajika juhudi kubwa katika kunusuru hali hiyo na kwamba mwanadamu Hana budi kufanya analoweza ili uwepo uendelevu wa sayari Dunia.

Kwa Mujibu wa Mwenyekiti huyo bionuai ni muhimu kwa binadamu kwa namna nyingi ambapo mimea hutoa hewa ya oksijeni na kusafisha hewa chafu.

Mgabe anafafanua kuwa mimea hutoa pia chakula, kivuli, vifaa vya ujenzi, dawa, nyuzi za nguo na karatasi huku mizizi ya mimea pia inapunguza mmomonyoko wa udongo na kuzuia mafuriko.

“Mimea, fungi na wadudu hutunza rutuba na kusafisha maji na kwamba kadri bioanuai inavyopungua na husababisha mifumo hiyo kuharibika,”.

Anasema katika nchi zenye matumizi makubwa ya dawa ya kuua wadudu kwa ujumla imehatarisha ustawi wa mimea mingi pamoja na kilimo cha mazao.

Kwa upande wake Mkurugezi wa Mara Mining Investment Josephat Mwita amesema licha ya mgodi huo kuwa na mikakati mizuri ya utunzaji wa mazingira pia umesaidia katika suala la vijana kupata ajira ambapo kwa sasa watu 300 wana ajira za kudumu na ajira za muda.

Vijana wengi walioajiriwa kwenye mgodi huo wanatoka katika vijiji vya Karende, Mrito, Nyangoto, Gibaso na Kwihacha.

Katika kufikia kuwa wachimbaji wa kati mgodi wa Mara Mining wanataka kuanza uchenjuaji dhahabu kwa teknolojia ya juu.

“Mgodi unakamilisha kulipa fidia wakazi hao ambao wapo maeneo ya mgodi huo ambapo
mpaka sasa mgodi umeshalipa asimilia 85% kama fidia kwa wakazi waliokuwa kwenye eneo la mgodi na tunaendelea kulipa ili tukamilishe zoezi hilo,”anasema Mwita.

Amesema wao kama wachimbaji wazawa bado wanakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na ukosefu wa mitaji ya kupanua kazi zao .

Ametaja changamoto nyingine ya watu wasio kuwa waamifu kuvamia eneo hilo kwa kujenga ili walipwe fidia na kuwepo kwa gharama kubwa za kukodi vifaa vya utafiti.