Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza
Viongozi na watendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela wametakiwa kuzingatia matumizi sahihi ya takwimu ili kufanya maamuzi kwa utashi wa kitakwimu kwani serikali imewekeza fedha nyingi katika zoezi la sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022.
Hayo yameelezwa na Mkufunzi wa Mafunzo ya usambazaji na matumizi ya matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 Omary Mdoka kwa viongozi na watendaji wa halmashauri hiyo.
Ambapo amesema takwimu hizo ziwe chachu na muongozo katika kutekeleza miradi mbalimbali, kupanga mipango sambamba na utungaji wa sera.
Meneja Idara ya shughuli za kitakwimu,Mkuu wa sehemu ya Gis kutoka ofisi ya Taifa ya Takwimu Benedict Mugambi akimwakilisha Mtakwimu Mkuu Wa Serikali amesisitiza juu ya matumizi ya matokeo ya sensa katika masuala yote yanayopangwa kutekelezwa kupitia muongozo wa matumizi ya matokeo ya sensa uliotolewa na Rais Samia.
“Kazi yetu sisi ni kuwaonesha namna ambavyo mnaweza kutafsiri matokeo ya sensa na mkayatumia katika mipango mbalimbali,” amesema Benedict.
Akifungua mafunzo hayo Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Hassan Masala amesema kuwa Ilemela imejipanga kuhakikisha mipango na programu zote za maendeleo zinapangwa kwa kuzingatia matokeo ya sensa ya watu na makazi, sensa ya majengo na sensa ya anwani za makazi ya mwaka 2022.
Wakichangia katika mafuzno hayo Wenyeviti wa mitaa ya Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kwa nyakati tofauti wameomba matokeo hayo ya sensa yakasaidie kupatikana ramani sahihi za maeneo yao ili ziweze kusaidia katika matumizi mbalimbali
Mwakilishi wa kundi la walemavu ameomba serikali kupitia ofisi ya Mkuu wa Wilaya kuangalia shule ambazo zina elimu jumuishi ili ziweze kusaidia watoto wenye ulemavu waweze kupatiwa vipaumbele katika kupata elimu ilio bora kwa kundi hilo.
Sambamba na mafunzo hayo, ofisi ya Taifa Ya Takwimu, ilikabidhi ramani ya Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela ikionesha idadi ya watu kwa kata, pamoja na ramani za kwenye kata zikionesha mgawanyiko wa watu na idadi yao kwa kila kata.
Kwa mujibu wa matokeo ya sensa ya mwaka 2022 Wilaya ya Ilemela ina idadi ya watu 509,687 kutoka watu 343,001 mwaka 2012 kati yao watu 241,137 ni wanaume na watu 268,550 ni wanawake.
Aidha, idadi hiyo inaonesha kiwango cha kasi ya ukuaji wa idadi ya watu katika Halmashauri hiyo kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita yaani kutoka mwaka 2012 hadi 2022 ni wastani wa asilimia 32.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi