November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Utoaji wa huduma za afya kidigitali kuleta mapinduzi ya mifumo ya afya

Na Mwandishi wetu, timesmajira

MTAALAMU Mshauri wa Ugharamiaji wa Huduma za Afya wa Mradi wa HPSS Tuimarishe Afya unaotekelezwa hapa nchini na Taasisi ya Swiss Tropical and Public Health, kwa ufadhili wa Serikali ya Uswisi, James Kidumba amesema utoaji wa huduma za afya kidigitali umekuwa njia sahihi katika kuleta mapinduzi ya mifumo ya afya kusomana na utaratibu mzuri wa utoaji wa huduma ya afya kwa wananchi.

Akizungumza hayo mwishoni mwa wiki Mtaalam huyo ,amesema taasisi yao imekuwa ikitekeleza mradi wa Health Promotion and Syestem Strengthening (HPSS) chini ya ufadhili wa kutoka serikali ya uswiz alisema miaka ya nyuma kutokana na ukosekanaji wa huduma za afya kidigitali kila mfumo ulikuwa unakuja peke ake lakini baada ya mapinduzi hayo kwa kipindi hiki wadau wengi wameangazia kuleta pamoja mifumo hiyo ili kusomana.

Amesema mara zote maamuzi ya upatikanaji wa huduma bora za afya yanategemea zaidi upatikanaji wa taarifa maalum kwa wakati maalum hivyo uwepo kwa mifumo ya kidigitali inayosomana itasaidia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa taarifa kwa urahisi zaidi.

”Ndani ya Kongamano hili la nne la mkutano wa 10 umetukutanisha na wadau mbalimbali pamoja na watalaam kuleta pamoja jumbe zao ambazo zinabebwa na dhana ya tafiti hivyo kama wadau mwaka huu tafiti zetu zimejikita zaidi katika suala zima la uboreshaji wa mfumo wa upatikanaji wa dawa na vifaa tiba ,katika vituo vya kutolea huduma kupitia mfumo wa ushitindi ambao unahusika uchangiaji au upunguzaji wa nafasi iliyokuwa imeachwa katika upatikanaji wa dawa na Bohari ya Dawa ya Taifa(MSD),”amesema na kuongeza.

”Hivyo katika mkutano huu,tumetoa mapendekezo yetu ya kuzidi kuongeza uboreshaji zaidi ya mfumo hasa katika upande wa utoaji wa huduma kidigitali katika upatikanaji wa dawa kwani kumekuwa na mapinduzi makubwa katika upande wa utoaji wa huduma ya afya kiteknojia kwa miaka mitano kutoka sasa kurudi nyuma,”amesema Kidumba

Amesema mifumo ya kidigitali ikizidi kuimarisha katika utoaji wa huduma za afya itasaidia kurahisisha uwasilishaji wa taarifa kuweza kuwafikia viongozi katika ngazi tofauti tofauti za maamuzi kwa urahisi na kuweza kuzifanyia kazi .

Amesema kwa uwepo wa huduma za kidigitali wanauwezo wa kuja na mipango madhubuti na namna nzuri na rahisi ya kuweza kuwafikia wananchi kwa urahisi zaidi.

Kwa Upande wake Mwakilishi na Mratibu wa Mkoa wa Dar es Salaam Bima ya Afya ya Jamii, Walter Kayombo amesema serikali kupitia ibara ya 83 (i) katika ilani ya Chama cha Mapinduzi imeelekeza wananchi wengi wapate huduma za afya kupitia bima ambapo serikali pia iliamua kutengeneza bima za afya kwa wananchi ambao hawapo katika mfumo rasmi ambao unaitwa CHF ambapo 2022 uliboreshwa na kuitwa ICHF.

Amesema mfumo huo unatumia mfumo wa kidigitali inahusika na utaratibu mzima wa kusajili mgonjwa na upatikanaji wa huduma za afya.”Mfumo huo tangu umeanza tumesajili wananchi wengi na unaendelea vizuri,”amesema na kuongeza”Tumekuwa tunaendelea kuhamasisha wananchi kuendelea kujiunga na mfumo huo ,kwani ni miongoni mwa mfumo unaosaidia watu kwa kiasi kikubwa kwani mwananchi anauwezo wa kupata huduma za afya kuanzia ngazi ya Zahanati hadi taifa,”amesema

Amesema kupitia mkutano huo wamekuwa wakiendelea kusisitiza jamii kupata uelewa zaidi juu ya mfuko huo ili kuweza kupata huduma mahali popote.