November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ofisi ya Waziri Mkuu kuendelea kushirikiana na wadau wa masuala ya Lishe

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online, Dodoma

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi amekutana na kufanya mazungumzo na wadau wa maendeleo wa Shirika Helen Keller Tanzania ofisini kwake Jijini Dodoma.

Miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa ni pamoja na kuimarisha ushirikiano na wadau hao katika kuhakikisha sekta ya lishe inapewa kipaumbele ili kuwa na Taifa lenye lishe bora kuanzia ngazi ya familia.

Dkt. Yonazi amesema Ofisi ya Waziri Mkuu itaendelea kusirikiana na wadau wa maendeleo kuhakikisha afua za lishe zinaboreshwa kwa wananchi kuhamasishwa kula vyakula vyenye virutubisho kwa kuzingatia mazingira yao yanayowazunguka pamoja na wananchi kupewa elimu ya magonjwa yasiyopewa kipaumbele ili kujikinga kwa ustawi wa Taifa.

“Ipo haja ya kushirikiana pamoja tuhakikishe wananchi tunabadilisha fikra za Jamii kuhusu masuala ya lishe na magonjwa kwa sababu itawasaidia kuacha kuishi kwa mazoea na badala yake wazingatie umuhimu wa kutunza afya zao ili waendelee kuwa sehemu ya uzalishaji katika familia zao na Nchi kwa ujumla,”Amesema Dkt. Yonazi.

Naye Mkurugenzi wa Shirika linalojishughulisha na masuala ya lishe la Helen Keller Tanzania, Dkt. Deogratius Ngoma ameeleza kwamba jukumu lao kubwa ni kujenga uelewa kwa jamii kuhusu vyakula hatarishi vinavyosababisha magonjwa yasiyoambukiza.

Aidha Mtaalam na Mshauri wa Masuala ya lishe Dkt. Theresia Jumbe kutoka Shirika hilo amebainisha kuwa maazimio waliyofikia ni kuendeleza shughuli za uratibu wa masuala ya lishe katika kusimamia na kuchangia utekelezaji wa afua za lishe zilizoainishwa katika mpango jumuishi wa lishe wa Multisectoral Nutrition Action Plan (NMMNAP)

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi akizumgumza katika kikao chake na wadau wa maendeleo kutoka Shirika linalojishughulisha na masuala ya lishe la Helen Keller Tanzania walipotembelea ofisini kwake Jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi (wa tatu kutoka kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Uratibu wa Shughuli za Serikali katika ofisi yake Bw. Paul Sangawe (wa kwanza kushoto) na baadhi ya watendaji katika ofisi yake pamoja na baadhi ya wadau wa maendeleo kutoka Shirika la Helen Keller Tanzania baada ya kikao hicho.
Mkurugenzi wa Shirika linalojishughulisha na masuala ya lishe la Helen Keller Tanzania, Dkt. Deogratius Ngoma akifafanua jambo wakati wa kikao chake na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi alipomtembelea ofisini kwake Jijini Dodoma.