November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kamati ya Bajeti ya SMZ, yaipa kongole NHC

Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online DSM

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi wamepewa kongole na wajumbe wa Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar kwa kuendelea kuwajengea uwezo wa makazi, mashirika nchini ili kutimiza wajibu wao kwa ufanisi mkubwa.

Ameyasema hayo Oktoba 6, 2023 jijini Dar es salaam Mwenyekiti wa kamati Mwanaasha Khamis Juma, mara baada ya kutembelea miradi ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ikiwa ni sehemu ya ziara yao ya siku moja ya kulifahamu vyema shirika hilo. na kujifunza jinsi wanavyotekeleza miradi yao nchini.

Serikali zote mbili kwa maana ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha mashirika hayo yanajengewa uwezo wa kutosha ili kuendelea kutekeleza miradi bora ya makazi kwa ajili ya ustawi wa wananchi na Taifa kwa ujumla.

“Tumejifunza mengi na tayari tumeona kuwa zaidi ya asilimia 95 ya nyumba za majengo haya tayari zimepata soko, tunawapongeza sana kwa kuzingatia kwamba Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) lina ushirikiano mzuri sana na Shirika la Nyumba la Zanzibar (ZHC)”

Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) lilianzishwa kwa Sheria ya Bunge namba 45 ya mwaka 1962. Baadaye NHC iliunganishwa na aliyekuwa Msajili wa Nyumba kwa Sheria namba 2 ya mwaka 1990 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2005 na kulifanya shirika hilo kujiendesha kibiashara.

Malengo ya shirika kwa mujibu wa Mpango Mkakati wake (2015/16-2024/25) ni pamoja na kuwa meneja mahiri wa haki miliki, kuimarisha uwezo wa kiutendaji na udhibiti, kutumia rasilimali watu kikamilifu, kuwa kiongozi katika maendeleo ya miliki, kuhuisha mikataba na mazingira ya kisheria na kujenga taswira ya shirika nchini.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba Zanzibar (ZHC), Mwanaisha Ali Said, amesema shirika hilo lipo katika utekelezaji wa miradi mbali mbali ikiwemo ya makazi ya wananchi wa kipato cha chini Pemba na Unguja.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetenga eneo la hifadhi kwa ajili ya maendeleo, hivyo shirika hilo litatumia fursa hiyo kujenga nyumba za kupangisha na kuwauzia wananchi mbalimbali ili kuleta makazi bora hapa nchini.

Mkurugenzi Mkuu huyo amesema kwa sasa ZHC imeanza kujenga nyumba za kuuza katika eneo la Mombasa kwa ajili ya Wachina.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Hamad Abdallah amesema, ziara hiyo ni mwendelezo wa utekelezaji wa ushirikiano waliousaini miezi kadhaa iliyopita mjini Dodoma.

Pia Abdallah ametoa wito kwa taasisi nyingine kuiga walichofanya kwani hatua hiyo inasaidia kila upande kujifunza mambo mapya kwa ajili ya maboresho makubwa na ustawi bora wa taasisi hizo za umma.

Mwezi Mei, mwaka huu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi Zanzibar zikiwemo taasisi zake za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na Shirika la Nyumba la Zanzibar (ZHC) zilitiliana saini hati ya makubaliano ya ushirikiano katika sekta ya ardhi na nyumba nchini.

Kupitia makubaliano hayo maeneo ya utekelezaji katika ushirikiano huo ni kukusanya, kuchakata na kubadilishana taarifa za ardhi baharini.