November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwenge wa uhuru kuzindua mradi wa Bil. 22 Tabora

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Sikonge

MWENGE wa Uhuru umewasili Mkoani Tabora na kuanza kukimbizwa katika halmashauri ya Wilaya ya Sikonge ambapo unatarajiwa kukagua, kuweka mawe ya msingi na kuzindua jumla ya miradi 49 yenye thamani ya sh bil 22.2 Mkoani hapa.

Akizungumza baada ya kupokea mbio hizo kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma Homera, Wilayani hapa, Mkuu wa Mkoa huo Balozi Dkt Batilda Burian amesema mwenge huo utatembelea na kukagua miradi mbalimbali iliyotekelezwa na serikali ya awamu ya sita katika sekta za elimu, afya, maji, mifugo na kilimo.

Alisema miradi ya elimu itakayotembelewa na kuzinduliwa ina thamani ya sh mil 809, miradi ya afya sh bil 1.8, ya barabara sh bil 163, mazingira sh mil 841, kilimo na mifugo sh bil 2, miradi ya kijamii sh mil 143 na miradi ya maji kutoka ziwa Victoria inayoendelea kutekelezwa katika Wilaya za Sikonge, Urambo na Kaliua.

Dkt Batilda alibainisha kuwa katika kutekeleza kauli mbiu ya mbio hizo kwa mwaka huu isemayo ‘Tunza Mazingira, Okoa vyanzo vya Maji kwa Ustawi wa Viumbe na Uchumi wa Taifa’ Mkoa umeanza kuweka nguzo za mipaka katika vyanzo vya maji vyote.

Mikakati mingine ni kuweka mabirika katika miradi ya umwagiliaji maji ili kuepusha mifugo kuharibu vyanzo hivyo ikiwemo kuhamasisha matumizi ya gesi badala ya kuni ili kukomesha ukataji miti ovyo.

Akiongea na wakazi wa Sikonge katika kata ya Tutuo baada ya kutembelea, kukagua na kuzindua miradi 6 yenye thamani ya sh bil 1.7 Kiongozi mwa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Abdallah Shaibu Kaim aliitaka jamii kujiepusha na vitendo vinavyochochea uharibifu wa mazingira.

Alitaja baadhi ya vitendo hivyo kuwa ni ukataji miti ovyo, uchomaji moto misitu na mashamba, shughuli holela za kibinadamu, uchimbaji holela wa madini na utupaji ovyo taka ngumu.

Alibainisha athari zitokanazo na vitendo hivyo kuwa ni pamoja na ukame, mafuriko, uharibifu wa uoto wa asili na misitu, kukosekana kwa mvua za kutosha na mabadiliko ya misimu ya mvua.

Kaim aliitaka jamii kuendelea kuhifadhi na kutunza mazingira yanayowazunguka  ili yawe chachu ya mafanikio katika shughuli zao za kiuchumi huku akionya kuwa yeyote atakayebainika kujihusisha na vitendo hivyo asifumbiwe macho.  

Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt Batilda Salha Burian akipokea mwenge wa uhuru kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma Homera katika uwanja wa shule ya sekondari Kiloli, katika Kata ya Kiloli Wilayani Sikonge Mkoani Tabora jana . Picha na Allan Vicent.