November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wahitimu chuo Cha maendeleo ya jamii watuma meseji kwa Rais Samia

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Kaliua

VIJANA 195 wa kike na kiume wamehitimu mafunzo ya astahashada katika kozi za Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Jamii, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na Ualimu wa Watoto katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii Kaliua.

Wahitimu wa Chuo hicho kilichoko Wilayani Kaliua Mkoani Tabora wameungana na vijana wenzao kumwomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan kuwapa fursa ya kusaidia jamii katika ngazi za vijiji na kata.

Walisema wakazi wengi wa vijijini bado wanauhitaji mkubwa wa watalaamu wa kuwahamasisha kushiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo, hivyo wakaomba kupewa ajira ili kuchochea kasi ya maendeleo kwa wakazi wa vijijini.

Sarah Salumu (23) mhitimu wa kozi ya Ustawi wa Jamii katika Chuo hicho alipongeza Wakufunzi kwa kuwaandaa vizuri katika mafunzo yao na kubainisha kuwa wako tayari kutumia elimu waliyopata kwa manufaa ya jamii.

Alifafanua kuwa wako tayari kwenda vijijini ili kumsaidia Mheshimiwa Rais kuhamasisha maendeleo ya wananchi, hivyo akaomba serikali kuweka utaratibu mzuri wa kuajiri vijana wanaohitimu mafunzo ya kati ili kusaidia jamii.

Juma Yasin (24) mhitimu wa kozi ya Maendeleo ya Jamii alisema ni ukweli usiopingika kuwa nafasi za ajira ni finyu lakini akaomba serikali iangalie namna ya kuwezesha vijana wanaohitimu mafunzo ya fani mbalimbali kujiajiri ili kuwainua.

‘Meseji yetu kwa Mheshimiwa Rais, mama yetu Dkt Samia Suluhu Hassan, tunaomba fursa ya ajira za vijijini ili tukahamasishe maendeleo ya wananchi, ikishindikana tunaomba atuwezeshe mikopo ili kuanzisha miradi ya kimkakati’, alisema.

Joyce Kamshiwa mhitimu wa kozi ya TEHAMA alisema vijana wanaohitimu fani mbalimbali katika vyuo vya kati ni wengi hivyo akaomba serikali kupanua wigo wa ajira za vijijini ili kusaidia jamii au kuwezesha vikundi vya vijana kujiajiri.

Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Kaliua Abdallah Hamis alisema kuwa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inafanya kazi nzuri sana ya kuwaletea maendeleo wananchi.

Aliomba vijana waliohitimu mafunzo yao katika chuo hicho na vyuo vingine kusaidiwa kupata ajira kwa urahisi katika ngazi za vijiji na kata ili kuharakisha maendeleo ya wananchi.

Alisisitiza kuwa uwepo wa chuo hicho umekuwa msaada mkubwa kwa vijana na jamii kwa ujumla, kimetoa fursa kwa vijana kuonesha umahiri wao katika fani mbalimbali hivyo kuchangia kukua kwa uchumi na kuongeza kipato kwa wananchi.