Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
Wananchi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela na Jiji la Mwanza wamepatiwa Hati Miliki za Ardhi huku halmashauri zote nchini zikitakiwa kuacha kufanya kazi na makampuni ya upima ambayo hayana uwezo.
Akizungumza wakati wa ziara ya kikazi jijini Mwanza iliyoambatana na ugawaji wa hati miliki kwa wananchi wa halmashauri hizo mbili, Naibu Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angelina Mabula amesema halmashauri zinapaswa kuchunguza na kupitia upya mikataba ya makampuni ya upimaji ambayo hayana uwezo na kuacha kufanya nazo kazi kwani hali hiyo zinasababisha usumbufu kwa wakazi wanotaka kupimiwa maeneo yao.
“Nitoe rai kwa halmashauri zote nchini, tusiingie mikataba na makapuni ambayo hayana uwezo, tunahitaji makampuni yenye uwezo ambayo yanaweza kuendelea kupima huku wananchi wakilipia ila yale ambayo mpaka mwanachi alipie kwanza ndio ardhi ipimwe hayafai, Halmashauri zimeshapewa maelekezo sasa hivi kazi inayofanyika ni kupitia mikataba yao upya na kuivunja,” amesema Dkt.Angeline.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Ofisa Mipango Miji wa Halmashauri hiyo Shukrani Kyando, amesema toka mwezi Aprili mpaka sasa halmashauri hiyo imeandaa hati 1684 ambazo zimeisha sainiwa na Kamishina wa Ardhi na msajili wa Ardhi ameisha zisajili hivyo alimuomba Naibu Waziri huyo kuwakabidhi wananchi hao.
Akimweleza Naibu Waziri, Kyando amesema “Ulitupa maelekezo ya kuandaa hati kwa ajili ya walimu na wafanyakazi ambao wapo tayari kuchangia fedha kwa ajili ya upimaji na hati tumeisha andaa viwanja 525 na walimu zaidi ya 400 wameisha vilipia.”
Ofisa Mipango Miji wa Jiji la Mwanza, Hosiana Kusiga amesema lengo lilikuwa ni kukusanya bilioni 6 katika mwaka wa fedha wa 2019/2020 lakini hadi sasa wamefanikiwa kukusanya zaidi ya bilioni 3 sawa na asilimia 52.9.
Baadhi ya wananchi wa Ilemela na Nyamagana waliopatiwa hati, wamewashauri wananchi wenzao kufuata taratibu na sheria zilizowekwa kwa kuhakikisha wanapimiwa na kumilikishwa viwanja vyao kisha wapatiwe hati ambayo ndio kitu wanachoweza kuringia na kuishi bila hofu wala wasiwasi na kumiliki kwa uhuru ardhi waliojaliwa na Mungu.
More Stories
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato
Wambura asikitishwa na makundi CCM Nyakato