Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Umeme(EWURA),Kanda ya Ziwa imetoa elimu ya umuhimu wa kuwa na leseni ya ukandarasi wa umeme(ufundi umeme) kwa wanafunzi wanaosoma fani ya umeme zaidi 100 wa Chuo cha Ufundi Stadi(Veta) mkoani Mwanza.
Lengo ni kuhakikisha jamii inaacha kutumia vishoka kwenye ufungaji wa miundombinu ya nishati ya umeme na wanafunzi hao ambao baada ya kuitimu masomo yao kabla ya kuanza kazi mtaani waombe leseni kutoka EWURA ambapo kifungu cha 5(a) cha Sheria ya Umeme, Sura ya 131,inaipa mamlaka ya kutoa leseni kwa watoa huduma mbalimbali katika sekta ya umeme.
Vilevile kifungu cha 8(1)(2)(h) cha Sheria ya Umeme, Sura ya 131 na Kanuni za Umeme (Huduma za Ufungaji wa Mifumo ya Umeme) ya mwaka 2022 Kanuni ya 4(1),mtu yeyote haruhusiwi kufanya shughuli za ufungaji mifumo ya umeme Tanzania Bara bila kuwa na leseni inayotolewa na EWURA.
Akizungumza mara baada ya utoaji wa mafunzo hayo yaliyofanyika Septemba Mosi chuoni hapo, Meneja wa EWURA Kanda ya Ziwa George Mhina, ameeleza kuwa shughuli za ufungaji wa mifumo ya umeme ni moja ya shughuli inayodhibitiwa na mamlaka hiyo,hivyo ili kuondokana na kadhia ya kuingia katika shida za kisheria wameona wapitie kwenye vyuo vinavyotoa mafunzo katika fani ya umeme Kanda ya Ziwa kutoa elimu ya umuhimu wa mafundi hao wa umeme kuwa na leseni.
Mhina ameeleza kuwa mafundi wengi wa umeme unawakuta mtaani baadhi yao wamesoma na kumaliza vizuri na kuwa na vyeti lakini wanafanya kazi bila ya kuwa na leseni kutoka EWURA jambo ambalo kimsingi ni kosa kisheria.
“Kwa nchi nzima kuna mafundi umeme zaidi ya 5000,Kanda ya Ziwa wapo zaidi ya 1200 ambapo kanda hii ina mikoa takribani 5, kwa idadi hiyo ni ndogo ndio maana tunatoa elimu kuhusu umuhimu wa kuwa na leseni,tumeanza kwenda kwenye vyuo ili wakihitimu waweze kuomba leseni na kuepuka mafundi ambao ni vishoka wasio kuwa na leseni wanaoweza kusababisha madhara,”ameeleza Mhina.
Pia ameeleza kuwa lengo ni wawafike wadau wengi zaidi ili wapate leseni na watakapoingia mtaani waweze kufanya kazi kwa kufuata sheria,taratibu,kanuni na kuepuka majanga ambayo yanaweza kujitokeza endapo miundombinu hiyo ya umeme itafungwa na watu wasiokuwa na leseni.
“Kwa sasa umeme umetapakaa sana vijijini REA wanajitahidi kufanya kazi yao wakishirikiana na Tanesco uwekezaji unaendelea kuna miradi mikubwa inafanyika Kanda yetu ya Ziwa na miradi ni mingi barabara,madaraja,bomba la mafuta na kadhalika na tunawekeza kwenye viwanda na kujenga nyumba wasipotumia mafundi wenye leseni kunaweza kusababisha miundombinu kupata moto na kupelekea uharibifu na wakati mwingine vifo,”ameeleza Mhina.
Kwa upande wake Mhandisi wa Umeme kutoka EWURA Kanda ya Ziwa Jonathan Elizeus, ameeleza kuwa leseni wanazo zitoa zipo katika makundi mawili ikiwemo leseni za kawaida za ufundi umeme ambazo zipo katika madaraja manne A,B,C na D, huku kundi la pili ni leseni ya kazi maalumu za ufundi umeme ambayo ina madaraja matatu ikiwemo daraja S1, S2 na S3.
“Tunatoa leseni ili kuhakikisha watumiaji wa hizi huduma wanakuwa salama,mifumo inayofungwa inakuwa salama na inalinda mali pamoja na maisha yao,”.
Nao baadhi ya wanafunzi wa fani ya umeme akiwemo Zuhura Mashaka, ameishukuru EWURA kwani imewapatia elimu ambayo wengi wao walikuwa hawana kuwa wakimaliza masomo yao wanapaswa kuwa na leseni kabla ya kuanza kazi huku akihadi kuwa balozi kwa wengine ambao hawajapata fursa hiyo.
Sadiki Juma,meeleza kuwa baada ya mafunzo hayo amegundua kuwa ni muhimu kuwa na leseni ya ufundi umeme ambao itawasaidia kuwatofautisha wao na mafundi wengine wasiokuwa na leseni(vishoka) pamoja na kumsaidia kujiamni na kuaminiwa katika fursa za kazi.
Mwalimu Mwandamizi wa VETA Mussa Domma,ameiomba EWURA kutoa elimu endelevu kwa jamii ili iwe na uelewa juu ya kutumia mafundi umeme wenye leseni pia wanafunzi wapatie elimu ili wakimaliza masomo kabla ya kuanza kazi wawe na leseni kwanza.
More Stories
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â