November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

‘Wengi wanaishi na maradhi ya moyo bila kujua’

Mwandishi Wetu

JAMII nyingi za kiafrika hazina utaratibu wa kwenda hospitali kuchunguza afya yao ya jumla hadi pale wanapojikuta wana matatizo ya kiafya.

Wengi huamini kuwa kama hujihisi tatizo mwilini huna haja ya daktari lakini ukweli ni kwamba kuna maradhi ambayo huanza bila kutoa dalili na yanapojitokeza wazi hali huwa ni mbaya.

Ili kufahamu kwa undani hali hiyo, soma kwa undani makala haya yaliyoandaliwa na Chama cha Waandishi Wanaopambana na Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza (TJNCDF) kwa kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza (TANCDA).

Kwa mujibu wa TANCDA, magonjwa ya moyo yanasababisha asilimia 48 ya vifo vyote duniani. Hapa nchini magonjwa ya moyo yanaendelea kuwa tishio kwa wananchi wengi na matibabu yake yamekuwa yakifanyika nje ya nchi kwa gharama kubwa.

Mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Profesa Mohamed Janabi moja wapo ya sababu za magonjwa ya moyo ni kuziba kwa mishipa ya damu inayosambaza damu kwenye misuli ya moyo.

Kuziba huko,Profesa janabi anasema kunaweza kusababishwa na mafuta mazito, hasa ya wanyama ambayo muathirika aliyatumia kwenye chakula alichokula.

Mafuta haya huganda katika kuta za mishipa hiyo,hali ambayo hutokea polepole na huchukua muda mrefu hadi mishipa kuziba kabisa.

Sababu nyingine,anazitaja kuwa ni shinikizo la damu lisilodhibitiwa,uvutaji wa sigara,ugoro,matumizi makubwa ya pombe na dawa za kulevya.

Vitu hivi hudhuru mishipa ya damu inayohudumia moyo na kudhoofisha misuli ya moyo. Sababu nyingine ni pamoja na kunenepa kupita kiasi,ongezeko kubwa la uzito unaozidi kiwango cha kawaida na kutokufanya mazoezi.

Mambo mengine, anaeleza yanachangiwa na umri mkubwa na ndiyo maana tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa matatizo ya moyo huwaathiri zaidi watu wazima kuliko watoto.

Ulaji usiofaa ni moja ya visababishi vikubwa vya maradhi haya mfano kula chakula kisichokuwa na viinilishe vya kutosha, chenye mafuta mengi hasa yenye asili ya wanyama.

Vyakula hivyo ni kama maziwa, nyama yenye mafuta mengi, siagi na mayai, sukari nyingi na chumvi kwa wingi ni tatizo.

Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza (TANCDA), Profesa Andrew Swai anasema tafiti za kisayansi zinapendekeza kuwa chumvi ailayo mtu isizidi gramu tano kwa mtu mmoja kwa siku nzima, hii ni sawa na kijiko kimoja kidogo cha chai.

Anaonya pia juu ya ulaji wa vyakula vilivyokobolewa huku akihimiza ulaji kwa wingi mboga za majani na matunda kila siku kama moja ya njia za kukabiliana na tatizo.

TANCDA inapendekeza mboga zisipikwe sana kiasi cha kupoteza rangi yake ya kijani ambayo ni muhimu kwa afya.

Pia inapendekeza ulaji wa aina mbalimbali za matunda kama vile zabibu, ndizi mbivu, matopetope, embe, pera, parachichi, peasi na tofaa (apples) angalau mara tano kwa siku.

Ni vizuri pia kula vitunguu saumu, vitunguu maji, njegere, karoti, broccoli, maboga, korosho na maharage ya soya.

Profesa Swai anaeleza kuwa kinachosikitisha kuhusu dalili za maradhi ya moyo ni kwamba, mtu anaweza kukaa na maradhi haya kwa muda mrefu bila kuona dalili zozote za moja kwa moja hadi mishipa na misuli ya moyo inapokuwa katika hali mbaya.

Kwa sababu hiyo, anaeleza mtu anaweza kupata shambulio la ghafla la moyo kutokana na moyo kushindwa kufanyakazi zake kama inavyotakiwa.

Dalili kuu za maradhi ya moyo zinapojitokeza,anazitaja ni kama vile maumivu ya kifua na mgongo hasa pale mhusika anapojishughulisha, moyo kwenda mbio kuliko kawaida, hali ya kuishiwa pumzi na kukosa usingizi.

Dalili zingine anazitaja kuwa ni kikohozi kisichokwisha, kichefuchefu na mwili kuishiwa nguvu za kufanya kazi.

Kutokana na ukweli kwamba dalili za maradhi haya hazijitokezi haraka na kwa uwazi, anashauri kuwa ni muhimu kubadilisha mtindo wa maisha kwa kuepuka visababishi na kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara.

Ikiwezekana ni vizuri kumuona daktari angalau mara moja kila mwaka kwa ajili ya kupata vipimo vya shinikizo la damu, kiwango cha mafuta kwenye damu.

Endapo utahisi maumivu ya kifua hasa baada ya kufanya mazoezi au kazi ngumu, ni muhimu kupata ushauri na uchunguzi wa kitabibu haraka.

Njia sahihi ya kukabili ya moyo ni kufanya uchunguzi wa mara kwa mara hasa kwa watu wenye umri zaidi ya miaka 40.

Wasiliana na daktari wako na ushauriane naye juu ya namna sahihi na hasa juu ya namna ya kufanya uchunguzi wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama vile kisukari, shinikizo la damu, macho, figo na maradhi ya moyo.