Na Suleiman Abeid,Timesmajira Online Tv, Shinyanga
MJUMBE wa mkutano mkuu wa mkoa wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Shinyanga, Khamis Mgeja amewatahadharisha wanachama wenzake wa CCM kutahadhari na michezo michafu inayofanywa na baadhi ya watu wasioitakia mema nchi ya Tanzania.
Amesema wapo baadhi ya watu wachache hapa nchini hivi sasa wamepania kwa kila namna kutaka kuichafua Serikali ya CCM inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kukwamisha utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ili watanzania waone hakuna kinachofanyika.
Mjumbe huyo wa mkutano mkuu wa CCM wa mkoa ametoa kauli hiyo kwenye harambee ya kuchangia ujenzi wa Ofisi ya kisasa ya Chama cha Mapinduzi na ukumbi wa mikutano ya kijiji cha Wame kata ya Kilago wilayani Kahama mkoani Shinyanga ambapo amechangia shilingi 100,000 na tofali 200.
Mgeja ambaye ni miongoni mwa makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Shinyanga amesema katika siku za hivi karibuni amebaini kuwepo mchezo mchafu unaotekelezwa na wasioitakia mema Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ikiwemo wale wanaopinga uwekezwaji wa bandari.
Amesema mchezo unaofanywa na watu hao una lengo la kuwagombanisha watanzania na Serikali yao iliyopo madarakani kwa kuwaaminisha habari zisizo na ukweli kuonesha Serikali imeshindwa kutimiza wajibu wake kikamilifu mfano upotoshaji mkubwa unaofanyika hivi sasa kuhusu suala la bandari.
Kada huyo wa CCM amefafanua kwa kutoa mifano kadhaa ambayo amesema ina lengo la kuwatoa watanzania katika kufikiria mambo muhimu ya kimaendeleo na badala yake wabaki wakiishutumu Serikali kwa madai haina jambo lolote la maana inalolitekeleza katika kuwaletea wananchi wake maendeleo tarajiwa.
“Nichukue nafasi hii kuwaomba na kuwatahadharisha watanzania wenzangu na wana CCM kwa ujumla, kwa sasa tunapita kwenye kipindi kigumu sana, hivyo lazima tuwe makini tuwaepuka na kuwaogoma kama ukoma wale wanaotutengenezea michezo michafu kwa lengo la kutaka kuichafua Serikali iliyoko madarakani hivi sasa,”
“Yapo baadhi ya mambo yanapotoshwa sana, mfano suala hili la bandari, limekuzwa ili tu lionekane halifai na Serikali imefanya “kituko” kikubwa kutaka kuibinafsisha, hadi watu wamefikia hatua ya kutoa lugha zisizokuwa za staha, kwa mfano kudai suala la bandari watu walitumia akili za matope, hii haikubaliki,” ameeleza Mgeja.
Ameendelea kueleza kitendo cha kuendeleza mashambulizi dhidi ya Serikali na Bunge ni kutaka kumchafua Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na mhimili wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huku wakijitahidi kuhamisha mawazo ya watanzania wajikite zaidi kwenye malumbano yasiyokuwa na maana badala ya kuwaza maendeleo.
“Sasa ndugu zangu niwaulize jambo moja hivi kweli kuna Serikali yoyote duniani inayoweza kudiriki kuuza nchi yake? Inashangaza kabisa wenzetu hawa suala la bandari ndiyo wamelivalia njuga, wanapiga kelele wakidai eti bandari imeuzwa, bandari imeuzwaaa, niwaombe watanzania na wana CCM wote wenye nia njema wapuuze kauli hizi za upotoshaji,”
“Haiwezekani wala haitatokea, Serikali hii ya CCM kuamua kuuza hata kipande kimoja cha ukubwa wa sentimeta moja ya ardhi kwa mtu ye yote asiyekuwa mtanzania, zipuuzeni hizi kelele za bandari imeuzwa, siyo kweli, na Serikali imetoa ruhusa kwa ye yote mwenye mawazo zaidi ya kuiendesha vizuri basi ajitokeza na apeleke ushauri wake,” ameeleza Mgeja.
Amewaomba watanzania wote wenye nia njema na nchi yao waendelee kuiunga mkono Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ili iendelee kuwaletea maendeleo badala ya kuiwekea vikwazo mbalimbali huku wakiikosoa pasipo utaratibu kwa kutumia maneno yasiyokuwa na staha dhidi ya viongozi wake wa Chama na Serikali.
Hata hivyo Mgeja amesema kwa hali ilivyo hivi sasa kuna kila sababu ya wanachama wa CCM kuwa mabalozi wazuri wa kuwaelimisha watanzania wengine juu ya kazi nzuri zinazotekelezwa na Rais Samia katika nyanja mbalimbali ikiwemo sekta ya afya, barabara, elimu, huduma za kijamii na uwekezaji wa bandari ya Dar es Salaam.
Akizungumzia kuhusu ujenzi wa Ofisi ya kisasa na ukumbi wa mikutano katika Tawi la CCM wa kata ya Kilago, amesema ni muhimu hivi sasa wanachama wa CCM wajikite zaidi katika ujenzi wa ofisi zao za chama katika matawi na kata zao ili ziwe ni za majengo mazuri na ya kisasa.
“Niwapongeze viongozi wetu wa CCM wa Tawi hili la Wame, kwa kweli wameona mbali kuitisha harambee hii, maana Tawi hili limo ndani ya kata ya Kilago ambayo mimi ndiye mwakilishi wake katika mkutano mkuu wa CCM wa mkoa, hivyo lazima Ofisi zetu za chama ziwe ni zile zenye ubora, na iwe mfano kwa wengine,” ameeleza.
More Stories
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa