November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mabula:Ipo haja ya kufanya mapitio sheria ya usalama barabarani

Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Mbunge wa Jimbo la Ilemela,Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt.Angeline Mabula amesema vifo vya wanariadha vilivyotokea Julai 22,2023 baada ya kugongwa na gari wilayani Ilemela vimeishtua serikali,hivyo ipo haja ya kufanya mapitio ya sheria ya usalama barabarani.

Dkt. Angeline amesema hayo wakati akiongoza mamia ya wakazi wa Mkoa wa Mwanza waliojitokeza kuaga miili ya watu watano kati ya sita waliofariki kwa kugongwa na gari wakifanya mazoezi ya kukimbia eneo la Lumala wilayani Ilemela mkoani hapa.

Ambapo amesema vifo hivyo vimeishtua serikali hivyo kama Mbunge na mtunga sheria anaona kuna haja kufanya mapitio ya sheria ya usalama barabarani ili wanaosababisha ajali na kusababisha vifo kwa makusudi washtitakiwe kwa kesi ya mauaji badala ya kesi ya trafiki.

Pia amevitaka vikundi vya wafanya mazoezi ya kukimbia(jogging club) kuongeza umakini wanapofanya mazoezi hayo huku kuzitaka mamlaka husika kuhakikisha aliyesababisha ajali hiyo anachukuliwa hatua.

Katika ajali hiyo iliyohusisha gari aina ya Hilux Double Cabin ilitokea jana Jumamosi Julai 22,2023 kwenye barabara ya Kiseke eneo la Lumala wilayani Ilemela ambapo dereva wa gari hiyo akiendesha kwa mwendokasi aliwagonga wana kikundi hicho cha wakimbiza cha Adden Palace ambao walikuwa zaidi ya 30 na kusababisha vifo 6 na majeruhi 16.

Zoezi la kuaga miili hiyo imefanyika Jumapili Julai 23,2023 katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza ya Sekou Toure ambapo mwili ulioagwa ni wa Makorongo Manyanda ambao utasafirishwa kwenda Kahama mkoani Shinyanga, Peter Fredrick (Kigoma), Shedrack Safari (Kilimanjaro), Selestine Daudi (Mwanza) na Hamis Waziri (Geita).

Mwili wa marehemu mmoja, Amani Magabe (24) ulitambuliwa jana na ndugu zake kisha kuchukuliwa na kusafirishwa kuelekea wilayani Tarime mkoani Mara kwa ajili ya maziko.