Na.Suleiman Abeid,Timesmajira Online, Shinyanga
HALMASHAURI ya Manispaa ya Shinyanga imepongezwa kwa kazi nzuri za maendeleo inazozitekeleza katika kuwaletea wananchi wake maendeleo ya haraka na kuifanya Manispaa hiyo kuwa katika mandhari inayovutia.
Pongezi hizo zimetolewa na Madiwani kutoka Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ambao ni Wajumbe wa Kamati ya Fedha wakiambatana na Watendaji wa Halmashauri hiyo ambao wameitembelea Manispaa ya Shinyanga kwa ajili ya kujifunza utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Omary Kumbilamoto amesema katika ziara yao wameweza kujifunza mambo mengi na kubaini kwamba ipo miradi mingi imetekelezwa kutokana na fedha za mapato ya ndani ikitumia mafundi wa kawaida (Local Fundi).
Kumbilamoto amesema lengo la ziara yao ni kujifunza mambo mbalimbali ambayo wao kama Jiji wanaweza kubadilishana uzoefu ipo miradi pacha inayotekelezwa na halmashauri hizo mbili hivyo kuona Manispaa ya Shinyanga imeitekelezaje na jinsi wanayoondoa changamoto zinazotaka kukwamisha.
“Niwapongeze wenzetu wa Manispaa ya Shinyanga kwa jinsi ambavyo mmeweza kutekeleza miradi mingi ya maendeleo kwa ufanisi tena kwa kutumia mfumo wa ‘Local fundi’ na kufanikisha, mfano sisi tuna mradi wa machinjio ya kisasa na wao wanayo, hivyo tumejifunza na sisi tunakwenda kutekeleza kama wao,”amesema na kuongeza kuwa
“Tumeangalia masoko ambayo wenzetu wameyajenga kwa gharama nafuu kabisa, na nimefarijika kwamba masoko mengine ama majengo mengine yametumia zaidi ya milioni 500 bila kuwatumia wakandarasi, wametumia local fundi, ambaye yeye hukabidhiwa tu vifaa na kujenga chini ya usimamizi wa wahandisi wa Manispaa,” ameeleza Kumbilamoto.
Amesema moja ya mambo ambayo wao wanayachukua na kwenda kufanyia kazi ni utaratibu wa kutumia Local fundi na kwamba moja ya changamoto ambayo wamebaini inachelewesha utekelezaji wa miradi mingi katika Jiji lao la Dar es Salaam ni kuwatumia Wakandarasi.
Ameendelea kufafanua kuwa siri nyingine ya mafanikio ambayo wameyabaini ni ushirikiano wa karibu kati ya madiwani, watendaji na wananchi wa Manispaa na kwamba aliyekuwa Mkurungezi wa Manispaa hiyo na sasa amehamishiwa Jiji la Dar es Salaam amechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio yanayopatikana Manispaa ya Shinyanga.
“Tumejifunza mambo mengi na tunayachukua kwenda kuyafanyia kazi kwetu, wenzetu Manispaa ya Shinyanga kasi yao ni kubwa, nimpongeze aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa, Jomaary Satura ambaye sasa kahamishiwa Jiji la Dar es Salaam kwa kweli nimeona utendaji na ubunifu wake ni mkubwa,”.
Amesema pamoja na kwamba bajeti ya Manispaa ya Shinyanga haizidi bilioni tano ama sita wakati wao hukusanya zaidi ya bilioni 81 lakini Manispaa wamefanya miradi inayoonekana hivyo wameona kuna umuhimu wa Wajumbe wa Kamati yake ya Fedha na wale wa Menejimenti kujifunza mafanikio hayo na watakaporejea Dar es Salaam waweze kufanya maamuzi mazuri.
Kumbilamoto ametoa mfano wa ujenzi wa majengo kwenye kituo cha afya cha Kambarage Manispaa ya Shinyanga mradi ambao upo pia katika Jiji na wote walipewa fedha kiwango kinacholingana, lakini wenzao wamekamilisha ujenzi na kubaki na ziada ya fedha huku upande wa Jiji la Dar es Salaam fedha zikiwa zimemalizika na majengo hayajakamilika.
“Walichotuzidi ni kitu kimoja, kwenye mradi huu fedha tulizopewa wao na sisi ni kiwango sawasawa, lakini sisi za kwetu zimekwisha majengo hayajakamilika, wao majengo yamekamilika na fedha zimebaki ziada ambayo wametekeleza miradi mingine, nimewaambia wataalamu wangu wajifunze ili tukirudi kwetu tukafanye mabadiliko makubwa,” ameeleza.
Kwa upande wake mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Fedha ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mchafukoge, Mariamu Lulida ameelezea kuridhishwa kwake na utaratibu unaotumiwa na Manispaa ya Shinyanga katika utekelezaji wa miradi yake ya maendeleo kwa ajili ya wananchi wake.
“Tumekuja Shinyanga kujifunza, japokuwa sisi ni Jiji na wao ni Manispaa lakini wameonesha jinsi gani wanavyotekeleza miradi yao kwa ufanisi, tumejifunza pamoja na kwamba fedha zao siyo nyingi sana kama Jiji la Dar es Salaam, lakini uwazi na uwajibikaji wao umewezesha wafanye makubwa, tumejifunza na sisi tunaenda kutekeleza,” ameeleza Lulida.
Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Elias Masumbuko na Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Alexius Kagunze wamesema wamefarijika kutembelewa na ugeni kutoka Jiji la Dar es Salaam ambao wamekuja katika manispaa yao kujifunza utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
“Hawa wageni wetu kutoka Jiji la Dar es Salaam wamekuja hapa kujifunza kuona jinsi gani tunavyoendesha shughuli mbalimbali za kuwajenga wananchi katika maendeleo yao ya kila siku na kusudi lao ni kujifunza namna tunavyotekeleza miradi mbalimbali kwa kutumia mapato ya ndani na fedha zinazotoka Serikali Kuu,” ameeleza Elias.
More Stories
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja