November 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Usawa kijinsia katika uongozi ngazi mbalimbali bado ni changamoto

Na Joyce Kasiki,timesmajira online,Dodoma

IMEELEZWA  kuwa bado makundi maalum likiwemo la walemavu, vijana na wanawake yapo nyuma kupata fursa za uongozi hasa katika vyama vya siasa  kutokana na baadhi ya sheria ya vyama hivyo kupitwa na wakati na hasa katika wakati huu unaotaka uwepo wa usawa wa kijinsia wa asilimia 50 kwa 50 katika uongozi.

Hayo yamesemwa na  Wataalamu wa sayansi ya siasa, wanasiasa na mashirika yasiyo ya kiserikali kwenye kikao cha pamoja kilichofanyika Jijini Dodoma kilicholenga kujua changamoto wanazokutana nazo  kuhusu ushiriki jumuishi wa makundi mbalimbali katika jamii.

Kikao hicho pia kililenga kuangalia changamoto ya kisheria, na kiuchumi huku wataalam hao wakitaka kufanyiwa marekebisho kwa baadhi ya vifungu vya sheria ya vyama vya siasa virekebishwe ili kuweka usawa wa kijinsia kuelekea uchaguzi wa serikali za miaka 2024 na uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge 2025.

Mmoja wa washiriki wa kikao hicho mtaalam wa Sayansi na Siasa Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam Profesa Alexander Makuliko  alisema, idadi ya makundi hayo hasa ya wanawake kushiriki kama viongozi katika vyama lakini pia katika nafasi za kidola bado ni  mdogo sana .

“Suala la hamsini kwa hamsini  ambalo tumeliangazia tumejiuliza ni nini tangu mfumo wa vyama vingi ulipoanza mpaka leo hii ukiangalia idadi ya makundi haya kushiriki kama viongozi katika vyama lakini pia katika nafasi za kidola ni mdogo sana .”alisema Profesa Makuliko     

Hata hivyo alisema,sababu mojawapo ni mfumo wa kisheria uliopo hapa nchini ambapo unamtaka mtu kushiriki katika uongozi lazima uwe umepitia katika chama cha siasa.

“Kwa hiyo  tukafikiri kwamba chama cha siasa ni muhimu tukiangazie ili kuweza kuona ni maboresho gani  wanaweza wakafanya ndani ya vyama na kuhakikisha ushiriki wa haya makundi unaongezeka,

“Kwa hiyo tulikua tunaangalia changamoto ambazo zimekuwepo kisheria lakini pia mfumo dume ,pamoja na masuala ya ukatili wa kijinsia wakati wa chaguzi zetu za ushiriki wa kisiasa na mambo kama ya namna hayo.., na waheshimiwa wabunge wameonekana ni watu ambao haya mambo wameyatilia mkazo lakini wametueleza”. Alisema

Kwa mujibu wa Profesa Makuliko  ,hivi karibuni katika Bunge la Bajeti tayari imetengwa bajeti kwa ajili ya kufanya maboresho ya sheria mbili sheria ya vyama vya siasa na sheria ya uchaguzi, huku akisema ni matarajio ya kikao hicho kwamba  mchakato chaguzi mbali mbali utakapoanza utatoa fursa kwa ajili kuweza kuona namna gani ya kuboresha siasa zetu katika nchi”,amesisitiza

Prof.Makuliko alisema mabadiliko hayo usawa wa kijinsia  hayawezi kutokea ghafla huku akisema lazima kuwe na msukumo wa jitihada mbalimbali ikiwemo kuweka sheria ambayo itaweka ulazima ili kiondoa dhana ya kimtazamo kwamba mwanamke hawezi kuongoza.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba  na Sheria Frolent Kiyombo alisema Tanzania inaongozwa na Katiba na Sheria ambayo ina utashi wa dhati ambayo inakua na fursa ya wanawake kuwa katika nafasi za uongozi kwa kuwa na 50 kwa 50 lakini mpaka sasa kupitia takwimu kuanzia mwaka 2015 mpaka 2023 ni asilimia 23 tu ya wanawake ndiyo wapo katika nafasi za uongozi.

“Suala la msingi ambalo sasa tunaendelea kutoa hamasa ili wanawake waendelee kupata nafasi ni kuangalia tafiti zilizofanyika kwamba zilibaini kosa ni nini lakini pia tunawasihi akina mama wenyewe kwamba  watambue wanayo fursa yakupata uongozi na nchi yetu imetoa nafasi katika Katiba lakini na vyama mbalimbali katika Katiba zao za vyama zimeanisisha fursa ya mwanamke.”alisema Kiyombo na kuongeza kuwa

“Kwa hiyo kwanza wanawake wenyewe wajitambue na waone kwamba wao wanaweza kuwa viongozi  na wajitokeze sasa fursa za uchaguzi zinapotokea wawe mstari wa mbele kujitokeza kwa wingi .”

Akizungumza kwa niaba ya wabunge ,Mbunge wa Viti Maalum Ester Matiko alisema, bado kuna changamoto nyingi za kimfumo, kijinsia na za kisheria vitu vinavyochangia kushindwa kufikia azma ya uwepo wa usawa wa kijinsia na hivyo wanawake kuendelea kuonekana hawana uwezo katika nafasi za uongozi.