Na Penina Malundo
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imesema imejipanga kuhakikisha wanatokomeza dawa za kulevya nchini ili kujenga uchumi imara.
Akizungumza na waandishi wa habari leo katika Maonesho ya 47 ya Kimataifa ya Biashara yanayoendelea kwenye Viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo alisema wamegundua vijana wengi wanaingia kwenye mkumbo wa matumizi ya dawa za kulevya kwa tamaa za kupata fedha huku wanafunzi wanajiingiza wakiamini wakitumia wataweza kusoma zaidi.
“Na ndio maana kazi yetu kubwa ni kuhakikisha tunawapa elimu ili waondokane na dhana hizi potofu. Hata hivyo tumeandaa pia muongozo wa ufundishaji ambao kupitia NGO’s na wadau mbalimbali na Wizara ya elimu utawasaidia wanafunzi na jamii watakuwa wanafundishwa juu ya uelewa dawa za kulevya, matumizi, madhara na jinsi ya kuepukana nazo kwasababu wengi wanaingia bila kujua madhara yake.
“Pia kupitia Wizara ya elimu kuna mchakato unaendelea ili kuingiza somo la elimu ya dawa za kulevya kwenye mitaala ya serikali ili kuhakikisha linafundishwa kuanzia shule za msingi mpaka vyuo,” amesema.
Amesema wamewasiliana na Wizara ya Kilimo ili kufanya utafiti kwenye maeneo ambayo yamekithiri na ukulima wa bangi na mirungi ili kuweza kutafuta mazao mbadala.
“Iko mikoa inayoongoza sana kwa kilimo cha bangi ikiwemo Arusha, Mara, Morogoro, Ruvuma na Iringa, lakini pia inayolima mirungi kama Tanga na Kilimanjaro na kote tunaenda kutoa elimu lakini wizara ya kilimo itafanya utafiti ili kuja na mazao mbadala ili waepukane na kilomo hicho,” amesema Lyimo.
Amebainisha kuwa lengo la kushiriki katika maonesho hayo ni kuhakikisha wanatoa elimu kwa wananchi juu ya athari za dawa za kulevya, aina pamoja na sheria zinazoongoza mamlaka na zile ambazo zinatolewa kwa watumiaji wa dawa za kulevya pamoja na hukumu zake ili kuwafanya wananchi kuzielewa.
“Lengo lingine ni kuhakikisha wananchi wanapata uelewa wa kutosha na wanakua elimu mitaani na kuwaelimisha wenzao ili watu wote waweze kujiepusha na dawa za kulevya kwani zina athari kubwa na kupoteza nguvu kazi ya Taifa.
More Stories
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake