November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tuunge mkono ustawi wa wanawake wakulima wadogo

Na Alice Musetti

KAMA umekula tunda au mboga leo hii, basi kuna uwezekano kubwa mwanamke ndiye amezalisha. Inakadiriwa na Shirika la Kimataifa la Chakula na Kilimo (FAO) na Benki ya Dunia kuwa zaidi ya asilimia 60 ya wanawake wa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara Afrika wanajihusisha na ukulima mdogo mdogo, ambapo huzalisha mpaka asilimia 80 ya chakula kwenye eneo husika. Pia, mchango wao kwenye nguvu kazi katika sekta ya kilimo duniani ni mkubwa.

Kilimo huleta maendeleo na hupunguza umaskini. Serikali na taasisi za maendeleo wamewekeza zaidi katika kuleta ujumuishi katika uvumbuzi na maendeleo ya kilimo, na usalama wa chakula.

Bado sekta hii inafanya kazi chini ya viwango, kwa sehemu ni kwa sababu wanawake, watu ambao ni muhimu katika sekta hii, hukumbana na vikwazo katika kupata rasilimali kitu ambacho hudhoofisha michango yao.

Lakini, kuunda mifumo endelevu ya chakula ni jambo la lazima jambo ambalo kwa serikali ya Tanzania linastawi sana, kama ilivyo elezewa katika mwongozo wa Awamu ya Pili ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Kilimo (ASDP II) ya Novemba 2017.

Waraka huo unaelezea kilimo kuwa ni eneo la msingi kwa serikali kuwekeza ili kuhamasisha uendeshaji wa sekta ambazo huongeza uzalishaji na mfumo endelevu wa chakula.

Hususani, mwongozo huu unaelezea kuhusu “Kubadilisha sekta ya kilimo kwa kuboresha uzalishaji, biashara na kipato cha wakulima wadogo ili kuboresha maisha, usalama wa chakula, na lishe.”

Hivi karibuni, Rais John Pombe Magufuli, katika hotuba yake ya April 10,mwaka huu alitoa wito kwa watanzania kufanya kazi kwa bidii kuongeza uzalishaji wa chakula, ili kuzuia uwezekano wa uhaba wa chakula katika kipindi hiki cha mlipuko wa virusi vya corona.

Aidha, kuondoa utofauti wa kijinsia, ni lazima tuanze kwa kuwapatia wanawake zana ambazo zitawawezesha kuitikia wito wa kuzalisha zaidi kwa gharama kidogo endelevu. Kwapatia wanawake rasilimali za kutosha za uzalishaji ni muhimu ili kuondoa utofauti katika uzalishaji. Hizi ni pamoja na ufadhili na pembejeo za kilimo.

One Acre Fund hutoa mtindo wa kufanya kazi endelevu katika suala hili. Kwa mradi wa Tanzania pekee shirika linahudumia zaidi ya wakulima 25,000, huwapatia wakulima wadogo ndani ya Afrika Mashariki pembejeo za kilimo-mbegu, mbolea kwa mkopo, na huduma ya mafunzo ya kilimo, ili kuwawezesha kustawi zaidi.

Wakulima hufurahia mfumo rahisi wa urejeshajii ambao unawaruhusu kufanya malipo ya mikopo yao kwa kiasi chochote kwa kipindi chote cha mkopo.

Mbali ya kuwa kiasi cha mkopo ni kamili- hakuna riba itolewayo kipindi chote cha msimu-wakulima pia hufaidika kwenye uwezeshaji wa masoko kwa kuwapatia suluhu za uhifadhi wa mazao na mafunzo juu ya hali ya masoko.

Watoa huduma za kifedha wenye uwepo katika maeneo ya vijijini wanaweza kusaidia kazi ya wakulima walio katika mazingira magumu kwa kupanga huduma zao kwa hali ya kipekee kwa wakulima wanawake.

Kwa mfano, huduma za mkopo zinaweza kutolewa katika kazi, kama vile biashara, badala ya ardhi.

Namna kipato kinapoongezeka, haya yanaweza kupitiwa tena ili kuwezesha wanawake kuhamia katika hali ya maisha tofauti, ikiwa na uwezekano wa kupata kipato zaidi.

Nyakati nyingine, mashirika ya maendeleo na taasisi zisizo za kiserikali huwa zinatoa huduma za ufadhili zinazowalenga wanawake , ili kuwaboreshea upatikanaji wa pembejeo za kilimo.

Katika hali nyinginezo, wanawake wa Kiafrika wanasaidiana wenyewe kwa kuunda vikundi vidogo vya vyama vya ushirika ambapo wao huweka na kujikopesha kati yao.

Vile vile, idadi kubwa ya taasisi za wanawake, kama vikundi vidogo vya kifedha, zinafanya kazi kuboresha upatikanaji wa huduma za kifedha, mafunzo, na taarifa. Hatua hizi zinapaswa kutiwa moyo na kuungwa mkono.

Rasilimali za uzalishaji haziishii tu kwenye upatikanaji wa fedha; zinajumuisha pia upatikanaji wa taarifa, ujuzi, na elimu.

Wanawake huwa wanakabiliwa na ukosefu wa haya yote, lakini sio lazima iwe hivyo. Katika mfumo wa mafunzo wa One Acre Fund, wakulima waliojiunga na mradi wanapata mambo yalioundwa kuwawezesha kupata taarifa, ujuzi, na mbinu za kuboresha ubora na kiwango cha mazao.

Faida za kuwekeza kwa mwanamke: Bila shaka, wanawake sio wakulima pekee wenye umuhimu. Lakini, kuwawezesha kunatoa baadhi ya faida kubwa, kama vile kuongeza kasi ya maendeleo ya uchumi wa vijijini na kitaifa, pia kukidhi mahitaji makubwa yanayoibuka ya chakula.

Aidha, wanawake ambao wanafanikiwa huwa wanawekeza zaidi katika nyumba zao na jamii zao na kudumisha afya za familia zao.

FAO inaonesha ya kuwa kama wanawake wangepata fursa sawa za rasilimali za uzalishaji kama wanaume, yamkini wangeweza kuongeza mavuno kwenye mashamba yao kwa kati ya asilimia 20 hadi 30, ambayo ingetafsiriwa kama punguzo la asilimia 15 la njaa duniani.

Kuhakikisha wanawake wanayo fursa sawa kama wanaume katika kushiriki katika uzalishaji wa chakula kutaongeza nafasi za kufaulu kwa maana ya kubadilisha na kushinikiza kilimo kama sehemu muhimu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Tukitazama nyuma hatua ambazo tumezifanya hadi sasa katika kufafanua na kutambua sehemu ya wanawake katika kilimo, lazima pia tujizatiti kufanyia kazi kuongeza ufikiaji wa usawa ili kuwawezesha wanawake kujikuza wenyewe, kaya zao na jamii zao katika kuendelea.