November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jokate atoa mitungi ya gesi 506 kwa viongozi wa vijiji

Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online Korogwe

MKUU wa Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga Jokate Mwegelo ametoa mitungi ya gesi 506 kwa viongozi wa vijiji na kata wa wilaya hiyo huku matumaini yake itakuwa chachu ya kulinda mazingira ikiwa ni pamoja na kutokata miti ovyo.

Amesema anataka kuona viongozi hao wa vijiji wanakuwa mabalozi wa wananchi kwa kuwataka waache kutumia kuni badala yake watumie nishati safi ya gesi katika matumizi yao ya kila siku ili kuilinda dunia na kutozalisha hewa ukaa.

Mkuu wa Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga Jokate Mwegelo akizungumza na viongozi wa vijiji, watendaji, madiwani na UWT wilayani humo (hawapo pichani) kwenye hafla ya kugawa mitungi ya gesi.

Ameyasema hayo Julai 4, 2023 kwenye hafla ya kukabidhi mitungi hiyo ya gesi yenye uzito wa kilo sita kwa kila mmoja iliyofanyika mjyini Korogwe, ambapo wanufaika ni madiwani wote wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe,Halmashauri ya Mji Korogwe, watendaji wa kata, vijiji, mitaa, wenyeviti 20 Mamlaka ya Mji Mdogo Mombo, na viongozi wa UWT ngazi ya Wilaya na kata.

“Lengo kuu la kuweza kutoa mitungi ya gesi hasa kwa viongozi wa vijiji ni kuona tunatunza mazingira,imani yangu kuwa Mwenyekiti na Mtendaji wa Kijiji wakianza kutumia nishati safi, wananchi nao watahamasika kutumia nishati hiyo,”amesema Jokate na kuongeza kuwa

“Mimi natimiza yale maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuona kama mazingira yataharibika, waathirika wa uharibifu huo wanakuwa ni wanawake na watoto hiyo ni kutokana na moshi unavyoathiri afya zao, huku watoto wakiwa hawaendi shule ama kusoma vizuri kwa ajili ya kutafuta kuni,”amesema Mwegelo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Oryx Gas Tanzania Ltd Araman Benoite (wa pili kushoto) akimkabidhi mtungi wa gesi, Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Korogwe Vijijini Hadija Mshahara (kulia) wengine ni Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Jokate Mwegelo (katikati), na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Sadick Kallaghe (kushoto).

Mwegelo amesema mitungi hiyo ya gesi inakwenda kuponyesha mambo mengi kwenye familia ikiwemo wanawake kutokulaumiwa kwa kuchelewesha upikaji wa chakula kwa familia.

Lakini pia kwa watendaji kufanya kazi zao kwa weledi na haraka kwa vile hakuna kitu cha kuwachelewesha nyumbani.

“Kwa kupata majiko haya ya gesi, tunakwenda kutibu mambo mengi kwenye familia ikiwemo ugomvi,tuachane na matumizi mabaya ya kuni,sisi tukiamua, sisi tukiweza, jambo hili litawezekana. Tunataka Korogwe iwe kinara wa matumizi ya nishati safi ya kupikia,”.

Pia amesema anataka wanaopewa mitungi hiyo waitumie kupikia huku matumaini yake ni kuwa watendaji hawatakwama kwa kuhangaika kupika kwa muda mrefu, hivyo kushindwa kusimamia miradi kwa weledi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Oryx Gas Tanzania Ltd Araman Benoite akizungumza na viongozi wa vijiji, watendaji, madiwani na UWT wilayani humo (hawapo pichani) kwenye hafla ya kugawa mitungi ya gesi.

Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe Neema Isaka, amesema kuwa Mkuu huyo wa Wilaya ni kiongozi mwenye maono na ubunifu mwingi, kwani amekuwa mtu wa matukio ya kuwaletea wananchi wa Korogwe maendeleo.

“Wewe ni mbeba maono na Mungu hatakuacha,maana umekuwa mtu wa matukio, likitoka hili linakuja hili,una marafiki wengi, ukaona uwalete waisaidia Wilaya ya Korogwe,maana yake huna uchoyo,sisi wana Korogwe ambao tumekusanyana hapa wakiwemo watendaji wa vijiji, mitaa, na watendaji wa kata na madiwani, tunakuahidi tutaendelea kutunza mazingira”amesema Isaka ambaye ni Diwani wa Kata ya Kwamndolwa.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Sadick Kallaghe amesema Mwegelo amekwenda Korogwe kuwaonesha wananchi kuwa kiongozi anatakiwa kuwaunganisha watu kuanzia viongozi waliopo chini yake na wananchi wanaowaongoza, jambo linaloweza kusukuma maendeleo kwa haraka.

“Jokate amekuja Korogwe kutufuta machozi,tumeona tofauti kati ya kiongozi na mtawala,shida kubwa iliyokuwa inatukabili Korogwe ni kukosa kiongozi wa kuwaunganisha viongozi wote na wananchi wote wa Korogwe ili waweze kufanya shughuli za maendeleo pamoja.

Viongozi wa UWT na Watendaji wa Kata Wilaya ya Korogwe wakiwa kwenye hafla ya kugawa mitungi ya gesi bure.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Oryx Gas Tanzania Ltd Araman Benoite amesema kampuni yake ikiwa kinara wa soko katika usambazaji wa gesi ya nyumbani (LPG) nchini Tanzania, inaendelea kufanya uwekezaji mkubwa nchini hapa kwa makundi mbalimbali ya wananchi ili kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhamasisha matumizi ya gesi safi ya LPG ambayo ni suluhisho la kuondoa matumizi ya kuni na mkaa.

Hivyo wanachofanya ni kuboresha afya ya jamii na kulinda mazingira sambamba na ahadi ya Rais Dkt. Samia ya kutoa nafasi ya matumizi ya nishati safi ya kupikia kufikia asilimia 80 ya Watanzania hadi kufikia mwaka 2032 .

“Katika muendelezo ule ule wa juhudi za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa wananchi wote, kampuni ya Oryx Gas Tanzania safari hii imesimama na wananchi wa Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga kupitia kwa viongozi wao kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa wote pamoja na kusaidia kuwabadilisha viongozi wa wananchi kuachana na kuni na mkaa na kuhamia kwenye nishati ya gesi za kupikia (LPG),”.

Oryx Gas imewezesha viongozi mbalimbali wa Serikali ya Kijiji na makundi mengine kwa kutoa bure mitungi ya gesi na majiko 500.