December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

‘PASS LEASING’ yawezesha kiuchumi wanawake Mil 1.7

‘PASS LEASING’ YAWEZESHA KIUCHUMI WANAWAKE MIL 1.7

Na Allan Vicent, Tabora

KAMPUNI ya PASS Leasing imewezesha wanawake wapatao milioni 1.7 ambao wamenufaika kupitia miradi mbalimbali katika sekta ya viwanda na kilimo

tangu kuanzishwa kwake miaka zaidi ya ishirini iliyopita.

Hayo yamebainishwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo Killo Lusewa alipokuwa akiongea na vyombo vya habari katika banda lao lililopo kwenye viwanja vya maonesho ya ushirika yanayoendelea mjini hapa.

Alisema tangu kuanzishwa kampuni hiyo jumla ya wana ushirika wapatao mil 3.4 wamenufaika na kampuni hiyo ikiwemo wanawake mil 1.74 sawa na asilimia 51 ya wanufaika wote.

Aidha kampuni hiyo ambayo ni kampuni dada ya PASS Trust tangu ianzishwe mwaka 2000, imewezesha jumla ya vyama vya msingi (Amcos) vipatavyo 634.

Lusewa aliongeza kuwa Amcos hizo zimepata mikopo yenye thamani ya sh. bil 212.3 ambayo imewekewa dhamana na PASS Leasing ya kiasi cha sh bil 84.8 ambapo jumla ya wanawake na wanaume 91,669 wamenufaika.

Alibainisha kwamba katika Amcos hizo zaidi ya 91, 000,fursa za ajira zilizozalishwa ni 49,419 ambapo wanawake ni 8,325 ni miongoni mwa wanufaika.

Killo akiongea kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni mama ya PASS Trust alisema kampuni hiyo imekuwa daraja muhimu sana la kuwezeshwa wakulima, wavuvi, wadau wa mazao ya misitu,wafugaji pamoja na wajasiriamali.

Alifafania kuwa pamoja na shughuli zote hizo pia wanatoa mafunzo ya kilimo, biashara, ufugaji na uvuvi kupitia vituo vyao vya ubunifu wa kilimo ni biashara

Aidha aliongeza kuwa wamefanikiwa kuongeza dhamana ili kukidhi uwezeshaji miradi na wadau mbalimbali kunufaika huku wakiweka dhamana ya asilimia kati ya 20 na 60 hadi 80 kwa biashara za vijana na wanawake.

Naye Katibu Tawala wa Mkoa huo Dkt John Mboya ameipongeza kampuni hiyo na kuitaka kuendelea kusimamia utoaji mikopo hiyo ili kuinua wanaushirika na taifa kwa ujumla.